Charles Ekelege
Mashahidi wa Jamhuri katika kesi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekelege, ya matumizi mabaya ya madaraka kwa kutoa asilimia 50 ya punguzo la tozo ya utawala kwa kampuni mbili na kusababishia hasara ya Dola 42,543 za Marekani, wamedai mshtakiwa alitoa msamaha huo bila kibali cha Baraza la Utendaji (kwa sasa Bodi ya Wakurugenzi).
Shahidi wa kwanza, Mwansheria Batista Bitao na wa pili, Mhandisi Joshua Katabwa, walitoa ushahidi huo jana mbele ya Hakimu Mkazi, Augustina Mmbando, anayesikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Akiongozwa na Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Janeth Machulya, shahidi wa kwanza alidai kuwa katika kipindi cha mwaka 2007 na 2009, kwa mujibu wa mikataba ya TBS na kampuni ya Jaffar Mohamed Ali Garage ya nchini Dubai na Quality Motors ya Hongkong walipaswa kulilipa shirika hilo asilimia 25 baada ya kufanya ukaguzi.
Alidai kuwa kati ya mwaka 2007 na 2009, Baraza la Utendaji (kwa sasa Bodi ya Wakurugenzi) kilikuwa ni chombo pekee chenye dhamana ya kusimamia shirika hilo.
“Mwaka 2007 na 2009 nilikuwa naalikwa katika baraza la utendaji (Bodi ya Wakurugenzi) lakini hatukuwahi kujadili suala la kusitisha tozo ya ada ya utawala… suala hilo liliibuka mwaka 2011 baada ya menejimenti kuwasilisha taarifa ya kutolewa msamaha kwa kampuni hizo mbili na iliambatanisha na maelezo ya kuomba radhi kuhusu kosa la kutoa msamaha huo bila kibali cha baraza hilo na kwamba halitajirudia,” alidai Bitao.
Naye shahidi wa pili, Katabwa alidai kuwa, kampuni hizo ziliingia mkataba na shirika la TBS kwa mkataba wa kulilipa asilimia 25 na kampuni hizo kubaki na asilimia 75 kama wakala wao.
Alidai kuwa, Machi 28, mwaka 2008 aliagizwa na Ekelege kuandaa barua ya kutoa msamaha wa asilimia 50 kwa kampuni ya Jaffar Mohamed Ali Garage. “Ekelege aliniagiza niandae barua ya kuwakubalia msamaha huo na aliisaini tarehe hiyo waliyowasilisha maombi yao…utaratibu huo ulitumika kwa kampuni ya Quality Motors kupokea majibu ya msamaha huo” alidai Katabwa.
Katika kesi ya msingi, inadaiwa kuwa, Machi 28 mwaka 2008 na Agosti 7, mwaka 2009, katika ofisi za TBS jijini Dar es Salaam, kwa nia ovu Ekelege alitumia madaraka yake vibaya.
Inadaiwa kuwa, mshtakiwa huyo alitoa punguzo la asilimia 50 ya ada ya utawala kwa kampuni hizo bila idhini ya Baraza la Utendaji la TBS kinyume cha sheria namba mbili kifungu kidogo cha (3) ya TBS ya mwaka 2005.
Ilidaiwa kuwa kitendo hicho kiliziongezea kampuni hizo faida ya Dola 42,543 za Kimarekani sawa na (kwa wakati huo) Sh. 68,068,800.
Mshtakiwa amekana mashitaka yote mawili na yuko nje kwa dhamana na kesi hiyo itaendelea kusikilizwa mfululizo Februari 5, 6 na 7, mwaka huu.
SOURCE:
NIPASHE
By Hellen Mwango
0 comments:
Post a Comment