Thursday, 9 January 2014

MADUKA YAFUNGWA TENA KARIAKOO JIJINI DAR

 
Baadhi ya wafanyabiashara wakionyesha mabongo yenye ujumbe wa kupinga matumizi ya mashine ya kutolea risiti ya Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kwenye mkutano na Waziri Dk. Abdallah Kigoda.
Baadhi ya maduka yaliyopo katika eneo la Kariakoo jijiji Dar es Salaam jana yalifungwa kwa siku nzima kutokana na wafanyabiashara wake kuhudhuria mkutano kati yao na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda.

NIPASHE lilishuhudia maduka yaliyopo mitaa ya Msimbazi, Aggrey, Tandamti, Swahili na Kongo yakiwa yamefungwa kwa siku nzima na hivyo kusababisha usumbufu kwa wateja waliofika kupata huduma.


Dereva teksi katika Mtaa wa Msimbazi, ambaye hakutaja jina lake, alisema wafanyabiashara hao hawakufungua maduka yao jana kwa sababu walikwenda katika mkutano uliohusu kupata ufumbuzi wa mfumo wa ulipaji kodi kwa kutumia mashine za kielektroniki (EFDs).


Alisema wafanyabiashara hao waliungana kwa pamoja kutofungua maduka yao siku nzima ili kupata suluhisho la tatizo la mashine hizo.

Alisema taarifa zilizokuwapo asubuhi jana ni kuwa endapo wasingeridhika na kikao hicho wasingefungua maduka leo.

Katika mkutano huo na Waziri Kigoda, wafanyabiashara hao waliitaka serikali kurekebisha mfumo wa ulipaji kodi, ambao hautawanyonya.


Wafanyabiashara hao kutoka sehemu mbalimbali nchini, walifika katika mkutano huo wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe unaopinga mfumo huo wa ulipaji kodi.

Baadhi ya mabango yalisomeka: “Kodi bila mashine inawezekana”.

“Tupo tayari kulipa kodi na mfumo wa ulipaji kodi wa nchi yetu urekebishwe na ujenge urafiki kati ya mlipakodi na mfanyabiashara. Na sisi leo tumeamua kufunga maduka ili kuja kuwasilisha kilio chetu,” alisema Mwenyekiti wa Wafanyabiashara hao, Philemon Chonde.


Katika madai yao, wafanyabiashara hao wanaiomba serikali iangalie namna ya kudai kodi na siyo mpango ulioandaliwa na watu wachache wa kuwakandamiza wanyonge. Walidai mashine hizo zinaua mitaji yao.


Mwenyekiti wa Chama cha Mlipakodi Tanzania, Lutieno Kigogo, alisema sheria za ulipaji kodi zinakiukwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).


Alidai TRA imeweka sheria zinazowakandamiza Watanzania wanyonge.

Alisema sheria ya ulipakodi kwa mashine iliyoingizwa na TRA ina kasoro, hivyo inatakiwa wakae meza moja na kujadiliana juu ya ulipaji wa kodi na matumizi ya mashine hizo.

Alisema kuna kero ya polisi wanaoitwa ‘tigo’, ambao wanafanya mashine hizo kuwa mradi wao. Minja alisema askari hao wamekuwa wakiwasumbua wafanyabiashara wa mikoani na jijini Dar es Salaam kwa kuwaomba rushwa.


Aliomba tume itakayoundwa ijumuishe watu wanaohusika na uchumi, jumuiya ya wafanyabiashara, Wizara ya Fedha, TRA pamoja na Wizara ya Viwanda na Biashara.

Dk. Kigoda aliwaomba waendelee kuwa wavumilivu na kuwaahidi atahakikisha anaweka mazingira wezeshi kwao. Alisema mambo ya uchumi hayamalizwi kisiasa, kwani yakimalizwa kwa njia hiyo hugonga mwamba.

Kwa mujibu wa Dk. Kigoda, suala la uchumi linatakiwa kumalizwa kiuchumi.

Alisema atahakikisha haki za mfanyabiashara mdogo na mkubwa zinapatikana na ziwe sawa kwa wote.

Dk. Kigoda alisema wafanyabiashara wadogo wana mchango mkubwa kuliko wakubwa, hivyo akasisitiza uvumilivu. 
SOURCE: NIPASHE
10th January 2014

Related Posts:

0 comments: