Wednesday, 23 December 2015

MUNGU WANGU MITANDAOO HATARI Jela kwa kupongeza majambazi yaliyovamia Polisi Stakishari

  

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu Bruno Kimaryo, kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia ya kusambaza ujumbe katika mtandao wa kijamii wa kuyapongeza majambazi yaliyovamia Kituo cha Polisi cha Stakishari na kuua polisi.  Aidha, mshtakiwa huyo ametakiwa ama kulipa faini ya Sh. 600,000 kwa kosa hilo.

Katika tukio la Stakishari lililotokea Julai 12, mwaka huu, majambazi yalivamia kituo hicho na kuua polisi wanne na raia watatu pamoja na kupora bunduki 20 aina ya Sub Machine Gun (SMG).
 
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Waliarwande Lema, baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi watano wa upande wa mashtaka. Alisema vielelezo vitano na utetezi wa mshtakiwa vinaonyesha kuwa Bruno alifurahia kitendo kilichofanywa na majambazi hao na alitamani kila kituo cha polisi kivamiwe.

Alisema mshtakiwa huyo katika ujumbe wake huo alitumia viunganishi vya maneno yasiyokuwa ya kibinadamu ya auawe, avamiwe na kuwa utetezi wake unaungana na maelezo ya onyo aliyoyatoa polisi hayaonyeshi kusikitishwa wala kuhurumia polisi.

Hakimu Lema alisema kama mshtakiwa angekuwa anapeleka ujumbe kwa polisi wachukue tahadhari, angeupeleka katika mamlaka husika, lakini kutokana na lugha aliyoitumia, mahakama hiyo inamtia hatiani.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo alifanikiwa kulipa faini na kukwepa adhabu ya kifungo.

Awali, ilidaiwa kuwa Julai 13, mwaka huu, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa huyo anadaiwa kusambaza machapisho ya uchochezi kinyume cha Sheria ya Magazeti kwa nia kuleta ushawishi na kueneza chuki katika mtandao wa kijamii wa facebook.

0 comments: