Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi, imetoa hukumu kwa mfanyabiashara Marijani Abubakar, almaarufu Papaa Msofe, Alex Massawe na Makongoro Nyerere kwa kosa la kughushi hati ya umiliki wa nyumba iliyopo Mikocheni jijini Dar, mali ya marehemu Onesphory Kituly aliyeuawa kwa kupigwa risasi na majambazi mwaka 2011.
Kesi hiyo iliyounguruma kwa takribani miaka saba tangu 2007, ilifikia tamati Desemba 22, mwaka huu na kuwakuta na hatia washtakiwa hao baada ya upande wa utetezi kushindwa kuwasilisha vielelezo vinavyowapa uhalali wa kumiliki nyumba hiyo.
Akisoma hukumu hiyo, jaji wa mahakama hiyo, John Nchimbi mbele ya wakili wa Msofe na wenzake, Majura Maghafu alisema kuwa baada ya kupitia hoja zilizowasilishwa na pande zote mbili, mahakama imeamua kumtangaza mke wa marehemu Onesphory, Mary Kituly kuwa mmiliki halali wa nyumba hiyo.
“Pia mahakama imewatoza fani ya shilingi milioni 300, Papaa Msofe, Massawe na Nyerere pamoja na asilimia 12 ya fedha hizo kama fidia ya gharama za uendeshwaji wa kesi hiyo,” alisema Jaji Nchimbi.
Mara baada ya kusomwa hukumu hiyo, mke wa marehemu, Mary aliangua kilio cha furaha na nduguze mbele ya jaji baada ya kuona haki imetendeka, kitu ambacho hakuwa akikitarajia.
“Yaani siamini macho yangu, maana jinsi kesi ilivyonisumbua kwa miaka saba, nimefarijika sana kwa haki kutendeka maana nilikuwa nikishindana na watu wenye pesa, damu ya mume wangu haijapotea bure, namshukuru Mungu kwa kweli,” alisema Mary alipokuwa akizungumza na waandishi ambapo alimshukuru pia Rais John Magufuli kwani serikali yake inajali haki.
Msofe na wenzake walifunguliwa kesi katika mahakama hiyo mwaka 2007 baada ya kudaiwa kughushi hati ya nyumba kwa kuhamisha umiliki wa nyumba namba 288 iliyopo Mikocheni, Dar iliyokuwa ya marehemu Kituly na kuweka jina lake kisha kumuuzia Masawe kinyume cha sheria.
Ilidaiwa kuwa kabla ya kufariki dunia, marehemu Kituly alimkopa shilingi milioni 30 Msofe kwa dhamana ya hati ya nyumba hiyo kwa makubaliano ya kumrudishia kiasi hicho kwa muda wa miezi sita.
Inadaiwa kuwa baada ya miezi mitano, marehemu alipata kiasi hicho cha fedha na kurudisha kwa Msofe na kutaka hati yake, lakini alianza kuzungushwa kuanzia kipindi hicho hadi alipokufa kwa kuuawa na watu wasiojulikana mwaka 2011.
Oktoba 30, 2007, Msofe aliwatoa kwa nguvu marehemu, mke wake na watoto kwa madai kuwa nyumba hiyo imeuzwa kwa Massawe.
0 comments:
Post a Comment