SERIKALI imetangaza kuwachunguza waganga na wauguzi, wanaomiliki hospitali, kliniki na maduka ya dawa baridi ili kubaini kama wanahusika na upotevu wa dawa kwenye hospitali za Serikali.
Akizungumza ofisini kwake juzi, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alisema Desemba 26 alipotembelea Hospitali ya Ocean Road, aliamua kuunda kamati ya watu watano kuchunguza kama wanahusika na upotevu wa dawa hospitalini hapo na sehemu nyingine.
Alisema bodi ya hospitali hiyo aliyoiunda wiki mbili zilizopita, nayo imeshaanza kufanya kazi ya kubaini chanzo cha uhaba wa dawa hospitalini hapo.
“Hata ukisoma tamko langu, hatukatazi watumishi wa umma wa sekta ya afya kumiliki hospitali, kliniki au maduka ya dawa, lakini tunachoangalia ni namna gani tunaondoa mgongano wa kimasilahi,”alisema.
“Nimeenda Ocean Road, wagonjwa wanakufa kwa kukosa dawa, tusubiri kamati itoe taarifa.”
Alisema katika ziara yake aligundua madudu mengi ikiwamo pia fedha za bajeti ya dawa zilizokuwa zikipangwa kwa ajili ya hospitali hiyo, kutofika kwa wakati.
Waziri Mwalimu alisema asilimia kubwa ya wagonjwa wanaotibiwa hospitalini hapo ni maskini,na kwamba watu wenye uwezo hutibiwa katika hospitali kubwa za kulipia na wengine wanatumia bima ya afya.
“Kwa kuwanyima dawa wanaokuja hospitali hizi ni sawa na kuwanyanyasa,” alisema Waziri Mwalimu.
“Bajeti ya dawa inayopangiwa hospitali hiyo imeonekana nyingi zilikuwa hazifiki kwa wakati. Nimeshamuagiza katibu mkuu wa wizara yangu ahakiki kila fedha zinazopelekwa kwa ajili ya kununua dawa wizarani.”
0 comments:
Post a Comment