Wasaliti hao wametangazwa jana na Katibu Itikadi na Uenezi wa CCM Mkoa wa Iringa, Dk Yahaya Msigwa ikiwa ni wiki moja tu tangu vijana wa chama hicho waifungie kwa zaidi ya saa mbili kamati hiyo, akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza, katika ofisi za CCM mkoa wa Iringa, mjini Iringa.
Vijana hao zaidi ya 50 wanaotarajiwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Manispaa ya Iringa, Kaunda Mwaipyana, waliifungia kamati hiyo wakishinikiza Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa Jesca Msambatavangu ajiuzulu kwa madai ya kukisaliti chama hicho katika uchaguzi wa Jimbo la Iringa Mjini.
Msambatavangu mwenyewe amenukuliwa mara kadhaa akikanusha tuhuma hizo huku akidai kwamba zinasukwa na vigogo wenzake wa chama hicho mkoani hapo ili kulinda maslai yao na kuficha ukweli halisi wa sababu zilizopelekea wapoteze jimbo hilo na kata 14 kati ya 18 kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Akizungumza na wanahabari jana, Msambatavangu ambaye alikiri jina lake kuwemo katika orodha ya makada wa CCM wanaotuhumiwa kukisaliti chama hicho iliyopokelewa na kamati aliyoiongoza yeye mwenyewe alisema pamoja na kwamba tuhuma hizo dhidi yake hazina ukweli yupo tayari kuhojiwa na kutoa utetezi wake katika vikao vitakavyofanya kazi hiyo.
“Najua na wanajua kwamba tuhuma hizo dhidi yangu hazina ukweli wowote na ikithibitika ni za kweli nitajiuzulu vinginevyo niwahakikishie wana CCM mkoani hapa kwamba nitawania tena nafasi hii ya uenyekiti katika uchaguzi ujao kwasababu sifa ninazo,” alisema.
Akizungumza na wanahabari, Dk Msigwa alisema taarifa iliyopokelewa katika kamati hiyo inaonesha Iringa Mjini inaongoza kwa kuwa na wasaliti wengi, ikiwa na jumla ya wasaliti 32.
Pamoja na kukataa kutaja majina ya wasaliti hao kwa madai kwamba watajulikana watapoanza kuitwa kwenye vikao vya maadili vya ngazi mbalimbali za chama hicho mkoani hapa, alijikuta akilazimika kuwataja vigogo wawili waliohusishwa katika tuhuma hizo Iringa Mjini baada ya wanahabari kumbana kwa maswali.
Mbali na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Iringa kutajwa rasmi katika orodha ya watuhumiwa hao, Dk Msigwa alimtaja kigogo mwingine aliyepo katika orodha hiyo kuwa ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa anayewakilisha Manispaa ya Iringa, Mahamudu Madenge.
Katika mchakato wa chama hicho wa kumpata mgombea ubunge wa jimbo la Iringa Mjini uliofanyika Agosti mwaka huu, Msambatavangu na Madenge walikuwa ni miongoni mwa wana CCM 13 waliojitosa kuwania nafasi hiyo ambayo mshindi wake alikuwa Frederick Mwakalebela.
Wakati Mwakalebela alishinda kura hizo za maoni kwa kupata kura 4,388, Msambatavangu alikuwa mshindi wa pili kwa kupata kura 2,077 na Madenge alikuwa wa tano kwa kupata kura 423, nyuma ya Dk Yahaya Msigwa aliyepata kura 1,097 na Dk Augustine Mahiga ambaye Rais Dk John Magufuli amemteua kuwa mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje, aliyepata kura 745.
Kama tuhuma hizo zilivyokanushwa na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa; Madenge naye amekanusha kuhusika na tuhuma hizo akisema; “Baada ya kushindwa kura za maoni nilirudi kijijini kwangu Image wilayani Kilolo na kufanya kampeni za kata ya Image na za jimbo la Kilolo ambako CCM na wagombea wake walipata ushindi mkubwa.”
Madenge alisema mbali na Kilolo, aliombwa pia kufanya kampeni katika majimbo ya uchaguzi ya wilaya ya Mufindi ambako pia CCM ilipata ushindi mnono.
“Naomba waniache kwasababu wanajua mimi nilishindwa vibaya kura za maoni kwa kupata kura 423 tu; kura ambazo hata kama ningewaambia walionipigia wakawapigie hao Chadema zisingeathiri matokeo hayo,” alisema.
Katika uchaguzi, huo Mchungaji Peter Msigwa wa Chadema alichaguliwa kuongoza jimbo hilo baada ya kupata kura 43,154 dhidi ya kura 32,406 za Frederick Mwakalebela wa CCM.
Akitaja orodha ya wasaliti wengine, Dk Msigwa alisema katika majimbo ya wilaya ya Mufindi kuna wasaliti 26 wakiwemo watumishi wanne halmashauri hiyo ambao hata hivyo hawakutajwa majina.
Kwa upande wa wilaya ya Kilolo, alisema taarifa waliyopokea inaonesha kuna wasaliti 23, huku Jimbo la Kalenga ikiwataja wasaliti saba na jimbo la Isimani wasaliti 14 wakiwemo watumishi wanne.
Alisema katika kuzishughulikia tuhuma hizo, watuhumiwa hao wataitwa kwenye vikao vya maadili vya ngazi mbalimbal ili wapate fursa ya kujitetea na watakaothibitika kutenda makosa hayo watachukuliwa hatua kwa kuzingatia kanuni, taratibu na Katiba ya chama.
“Wale ambao maamuzi dhidi yao hayawezi kufanywa na vikao vya ngazi ya kata, wilaya na mkoa, taarifa zao zitapelekwa taifani na tuombe vikao hivyo vya taifa vitende haki kwa kuzingatia ushahidi na mapendekezo yatakayotolewa na vikao vyetu ili kushughulikia tatizo hili la usaliti,” alisema.
Wakati huo huo, Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Elisha Mwampashi ambaye pia ni Katibu wa CCM Manispaa ya Iringa amekanusha uvumi unaonezwa na baadhi ya wa CCM kwamba chama hicho kilitumia zaidi ya Sh Milioni 600 kwa ajili ya uchaguzi wa jimbo la Iringa Mjini.
“Sio kweli hata kidogo, hatukuwa na fedha hizo, na nataka mjue CCM ilizingatia sana sheria ya gharama za uchaguzi wakati tukifanya kampeni. Niwashukuru CCM Makao Makuu, Mkoa na wana CCM na wapenzi wetu kwa jinsi walivyojitolea katika kampeni hizo,” alisema.
Chanzo; frankleonard blog
0 comments:
Post a Comment