Friday, 25 December 2015

ANGALIA Mapya Yaibuka Mauaji ya Wafanyabiashara Walio Pigwa Risasi na Polisi Dar


Mapya yameibuka kuhusiana na tukio la kuuawa kwa wafanyabiashara Yasin Rashid na Samson Michael ‘Ngosha’ wanaodaiwa kupigwa risasi jijini Dar es Salaam na askari wa kikosi maalum cha kudhibiti ujangili kufuatia taarifa zinazodai kuwa mmoja wa marehemu hao alikuwa akitumiwa na askari kuwapa taarifa za mauziano ya meno ya tembo kwenye hoteli moja maeneo ya Sinza saa chache kabla ya kifo chake.

Kwa mujibu wa Polisi, mauaji ya wafanyabiashara hao yalitokea Jumamosi iliyopita (Desemba 19), huku baadhi ya watu wanaodai kushuhudia tukio la kuuawa kwa Michael ‘Ngosha’ wakieleza kuwa lilitokea Sinza majira ya saa 7:45, karibu na Shule ya Msingi Reginald Mengi.

Hata hivyo,  chanzo kimoja kiliiambia Nipashe katika taarifa ya jana kuwa Rashid aliuawa katika eneo jingine, maeneo ya fukwe ya Bahari ya Hindi na siyo Sinza kama ilivyokuwa kwa mwenzake (Ngosha).

Chanzo kimoja kiliiambia Nipashe kuwa sababu kubwa ya kuuawa kwa wafanyabiashara hao ni fedha kiasi cha Sh. milioni 168 alizokuwa nazo Ngosha (Michael), ambaye aliuza meno kadhaa ya tembo aliyoyafikisha jijini Dar akitoka nayo kwenye mkoa usiotajwa, lakini safari yake ikihusisha Mikumi mkoani Morogoro.  

Hata hivyo, taarifa mpya ambazo Nipashe imezipata zinaeleza kuwa kabla ya kuuawa, Rashid alikuwa mtu wa karibu na baadhi ya askari wa kikosi cha kuzuia ujangili na kwamba, kama siyo yeye (Rashid) kuwaeleza kuhusu mauzo ya meno ya tembo aliyofanya Ngosha katika hoteli moja iliyopo Sinza, isingekuwa rahisi kwa askari hao kufika eneo la tukio.

Awali, akizungumza na waandishi wa habari Jumatatu wiki hii, Kamanda wa Polisi katika Kanda Malaum ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Suleiman Kova, alisema jeshi lake linawashikilia askari sita wakiwamo wanne kutoka katika kikosi maalum cha Kukabiliana na Ujangili nchini kuhusiana na utata uliojitokeza kuhusiana na vifo vya wafanyabiashara hao.

Kamanda Kova alisema kuwa taarifa zilizofikishwa awali zilidai kuwa Rashid na Ngosha wanaodaiwa kuwa ni majangili, waliuawa wakati wakirushiana risasi na askari hao wa kikosi maalum cha kukabiliana na ujangili kwenye maeneo ya Sinza.

Alisema wanaoshikiliwa ni askari sita wakiwamo polisi wa kawaida wawili na wengine wanne wa idara ya wanyamapori. Polisi wa kawaida wanaoshikiliwa kwa tuhuma hizo ni Bonny Mbange na Philibert huku wale wa wanyamapori wakiwa ni Emmanuel Mbaga, Deogratias Mwageni, Joseph Jimmy na Asbile Mwakyusa. Mwingine aitwaye Issa Kazimoto bado anatafutwa na polisi baada ya kukimbilia kusikojulikana.


KUHUSU RASHID
Chanzo kimoja kiliiambia Nipashe kuwa licha ya Rashid kuwa rafiki wa Ngosha (Michael), ndiye pia aliyekuwa akiwasiliana na baadhi ya askari wa kikosi cha kudhibiti ujangili na kuwaleza kila hatua aliyokuwa akipita kutoka mkoani alikokuwa hadi Sinza ambako ndiko biashara ilifanyika na Ngosha kulipwa kiasi kikubwa cha fedha kinachotajwa kuwa ni Sh. milioni 168.

Inaelezwa kuwa mpango uliokuwapo ni kwa askari kutumia taarifa walizokuwa wakizipata kutoka kwa Rashid tangu Ngosha alipokuwa Mikumi kuelekea Dar es Salaam hadi Sinza ili wavamie eneo la mauziano na kuwakamata wahusika (Ngosha na mnunuzi wa meno yake) pamoja na vielelezo vingine kama ushahidi.

“Licha ya Rashid kuwapa maelezo yote kuhusu biashara hiyo, bado askari hawakufika kwa wakati. Na hili halikufanyika kwa bahati mbaya, ni kwa sababu kinachoonekana ni kwamba walijichelewesha kwa nia ya kusubiri biashara ikamilike ili wakute fedha zikiwa tayari,” chanzo kiliiambia Nipashe.

Aliongezea kuwa, “Rashid aliendelea kuwasiliana na askari hao na kuwajulisha wafanye haraka kwa kuwa wameanza kuhesabiana fedha, lakini bado hawakuwahi eneo hilo.”

Chanzo kinaeleza kuwa baada ya askari kufika kwenye hoteli hiyo huku wakijua kuwa tayari biashara imeshafanyika, ndipo palipoibuka malumbano yaliyomlazimu Rashid kujaribu kukimbia eneo hilo, kama ilivyokuwa kwa Ngosha (Michael) ambaye naye aliiwahi gari yake aina ya Toyota Platz na kuondoka.

Hata hivyo, ilielezwa zaidi kuwa Rashid hakufika mbali baada ya kupigwa risasi ya mguu na kukamatwa akiwa majeruhi, hiyo ikiwa ni baada ya wananchi waliokuwa jirani kutoa msaada wakidhani kuwa ni jambazi.

Kadhalika, jitihada za Ngosha ziligonga mwamba pia kwani watu wanaodaiwa kuwa ni askari waliokuwa kwenye gari linalotajwa kuwa ni Toyota GX 110 (likiwa halina namba rasmi bali za ‘cheses’), walilipiga risasi gari lake na yeye kumjeruhi kwa risasi iliyompata maeneo ya bega.  

Ilielezwa na baadhi ya watu waliodai kushuhudia tukio hilo kuwa baada ya kuona amezidiwa, Ngosha alisimamisha gari, akateremka na kujaribu kunyoosha juu mikono yake kuashiria kujisalimisha. Ni hapo ndipo mmoja wa watu wanaodaiwa kuwa askari alimfuata na kummiminia risasi za kifuani zilizomuangusha chini na kufariki dunia.

Taarifa zaidi kutoka kwa waliojitambulisha kama mashuhuda zilidai kuwa baadaye, waliomuua walitwaa mfuko mkubwa wa rangi ya khaki na bahasha kubwa, vyote vikidaiwa kuwa na fedha ambazo chanzo kingine kiliiambia Nipashe kuwa ni Sh. milioni 168.

Ilielezwa zaidi kuwa watu hao wanaodaiwa kuwa askari walikabidhi mifuko hiyo inayodaiwa kuwa na fedha kwa mtu aliyefika mahala pa tukio na bodaboda, kisha akaondoka nazo.

Chanzo kingine kiliiambia Nipashe kuwa Rashid aliuawa na watu hao wanaodaiwa kuwa askari ili kufanikisha mpango wa kugawana fedha zilizotwaliwa kutoka kwa Ngosha.

Chanzo kingine kiliiambia Nipashe kuwa kabla ya kuwa mtu wa karibu na askari wa kikosi cha kupambana na ujangili, Rashid alikuwa akijihusisha na biashara zinazohusiana na ujangili kabla ya kuacha na kujiunga katika vita hiyo.

KOVA ASEMA UCHUNGUZI UNAENDELEA
Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana, Kamanda Kova alisema uchunguzi unaendelea na wakati muafaka ukifika wataeleza kila kitu kwa umma.

"Uchunguzi unaendelea. Hatuwezi kuzungumza kila siku na mwandishi mmoja… nitafanya kikao na waandishi wote pindi upelelezi utakapokamilika," alisema.
CHANZO: NIPASHE

0 comments: