Friday, 18 December 2015

(CAG) Akaidi Agizo la Rais Magufuli....... Aenda Nairobi, Kenya Kwa Fedha za Serikali Bila Kibali Cha Ikulu

 

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Juma Assad, amekiuka agizo la Rais Dk. John Magufuli, baada kusafiri nje ya nchi bila kibali cha Ikulu.

Kwa mujibu wa gazeti la Mtanzania, CAG aliondoka nchini Jumamosi (Desemba 12, 2015) kwenda jijini Nairobi, Kenya na kurejea nchini Jumanne wiki hii.

Taarifa hizo, zimesema CAG alikwenda kutoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha Nairobi, kazi ambayo haina uhusiano na ofisi yake, lakini alilipiwa gharama zote na ofisi yake.

“Bosi wetu aliondoka kwenda Nairobi Jumamosi iliyopita na kurejea Jumanne, alikwenda kutoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha Nairobi bila kibali cha Ikulu, alipaswa kupata kibali kwa sababu ofisi yake ndio ililipa gharama zote.

“Jumla ya gharama zinafika Sh milioni 15, ambazo ni pamoja na posho, tiketi ya ndege, hoteli na gharama nyinginezo,” kilisema chanzo cha gazeti hilo.

Alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu safari hiyo, Profesa Assad hakuthibitisha wala kukanusha taarifa hizo, zaidi ya  kutishia kwenda mahakamani.

“Wewe si umesema umepata taarifa kutoka vyanzo vyako na umenipigia ‘for validation’, sasa mimi nakwambia hizo taarifa si za kweli na mkiandika tutachukua hatua,” alijibu CAG.

Baada ya muda, Profesa Assad alipiga simu kwa  mhariri akimtaka afike ofisini kwake akachukue nyaraka za kuthibitisha kuruhusiwa na kusafiri nje ya nchi na ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.

Kutokana na mhariri huyo kuwa nje ya Dar es Salaam, alimtuma  mwandishi mwingine kwenda katika ofisi ya CAG ili kuchukua nyaraka hizo. Mwandishi alipofika, CAG alikataa kumpa wala kumwonesha nyaraka hizo.

Juhudi za kumpata Balozi Sefue kuzungumzia suala hilo hazikuzaa matunda. Baada ya kupigiwa muda mrefu aliandika ujumbe mfupi wa simu ukisema. “Nimebanwa na majukumu siwezi kupokea simu yako,” ulisomeka ujumbe huo.

Tukio hilo la CAG limekuja siku mbili baada ya Rais Dk. John Magufuli kuagiza kusimamishwa kazi kwa watumishi wanne wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kosa la kusafiri nje ya nchi bila kibali cha Ikulu.

Watumishi wa taasisi hiyo waliosimamishwa kazi ni Ekwabi Mujungu (Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu), Doreen Kapwani, Rukia Nikitas na Mary Mosha.

Profesa Assad aliteuliwa kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Novemba 5, 2014.

Kabla ya uteuzi wake, alikuwa Profesa Mshiriki, Idara ya Uhasibu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na alichukua nafasi ya Ludovick Utouh ambaye alistaafu kwa mujibu wa sheria.

0 comments: