Unapoingia katika nyumba ya familia ya Salehe Saidi, macho na masikio yako hayawezi kukwepa ucheshi wa kijana wa miaka 13, Jumbe Salehe. Ni kijana anayeipa tabasamu familia hiyo.
Jumbe ni mwenye nguvu, afya, akili darasani na uchangamfu ambao kila mzazi angependa kuuona kwa kijana wake. Lakini Jumbe Salehe, hakuzaliwa kama watoto wengine. Alipatikanaji katika mchakato mrefu, uliohusisha teknolojia ya hali ya juu na majaribio yaliyohitaji werevu. Jumbe alizaliwa kwa njia ya upandikizaji wa mbegu ambao kwa jina la kitaalamu unajulikana kama In-Vitro Fertilization (IVF). Mchakato huo ulisimamiwa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake, Profesa Malise Kaisi.
Kwa nini Jumbe alizaliwa kwa njia ya IVF?
Mwanaidi Kombo, mama mzazi wa Jumbe, hakuwa na tatizo la uzazi hapo awali. Alifanikiwa kupata mtoto wake wa kwanza mwaka 1986.
Mwaka 1988 alipata ujauzito mwingine
lakini kwa bahati mbaya, uliharibika na kuanzia hapo ikawa ni vigumu
kwake kushika mimba nyingine.
"Baada ya kuhangaika kwa muda mrefu
nikajaribu kupata mtoto, lakini tatizo jingine likaanza. Mwaka 1990.
Nilianza kupata maumivu makali ya tumbo," anasema Mwanaidi.
Kutokana na maumivu hayo, alianza
kusaka msaada wa kitabibu na alishauriwa kwenda kwa daktari wa magonjwa
ya wanawake, Dk. Malikiti wa Hospitali ya MM.
Safari yake kwenda kwa daktari
ilimsaidia kung'amua ukweli, kwani aliambiwa kuwa ana uvimbe mkubwa
kwenye kizazi ambao unaweza kuhatarisha maisha yake na kuwa ndicho
chanzo cha kushindwa kupata mtoto.
Hata hivyo, Dk. Malikiti alimuelekeza aende kuonana na Profesa Kaisi kwa kuwa ndiye mtaalamu wa masuala ya uzazi kwa wanawake.
"Nilipofika kwa Dk. Kaisi,
nilimshangaa baada ya kuisoma picha ya Xray. Aliniambia niache kabisa
kunywa dawa nilizoandikiwa za maumivu na kuambia ninywe panadol endapo
nitakuwa na maumivu," anasema.
Ingawa Mwanaidi alishangaa, aliendelea na kliniki ya Dk. Kaisi akihudhuria kila wiki kwa zaidi ya miezi miwili.
Siku moja Dk. Kaisi akaamua kumfanyia
kipimo cha CT Scan kuangalia mirija ya uzazi na ndipo alibaini kuwa
pamoja na uvimbe, mrija wake mmoja umepinda.
"Aliniambia niende nyumbani na nirudi
baada ya mwezi mmoja kwa ajili ya upasuaji, lakini wakati huo alinipa
masharti mengi kama nisinywe kabisa chai," anasema.
Baada ya mwezi mmoja, Mwanaidi alirudi
kwa Dk. Kaisi ambaye alimwambia ni lazima amfanyie upasuaji mdogo
kwanza kwa ajili ya kurekebisha mirija ya uzazi.
Katika upasuaji huo, ambao kitaalamu
unaitwa 'ovary re-implantation', madaktari walirekebisha mirija hiyo kwa
kufunga kifaa maalumu.
Mwezi mmoja baadaye Mwanaidi alirudi
kwa daktari ambaye aligundua kuwa bado mwanamke huyo ana uwezo mkubwa wa
kuzaa kwani alikuwa na mayai ya kutosha kumuwezesha kushika ujauzito.
"Aliniambia nina mayai ya kutosha,
lakini tatizo ni hilo la uvimbe na kupinda kwa mirija ya kusafirisha
mayai ya uzazi na mbegu," anasema.
Baada ya hapo, Mwanaidi alifanyiwa
upasuaji mwingine mkubwa kwa ajili ya kuondoa uvimbe. Zoezi hilo
lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa ingawa siyo kuondolewa kizazi.
Baada ya hatua hii, Profesa Kaisi
alimshauri Mwanaidi kuendelea kutafuta mtoto mwingine kwa sababu anao
uwezo wa kubeba mimba ingawa itakuwa vigumu kwa yeye kupata ujauzito huo
kwa njia ya kawaida.
Profesa Kaisi anasema aliwashauri kuwa
wanaweza kupata ujauzito kwa njia ya upandikizaji jambo ambalo
lilikubaliwa mara moja na wazazi hao. Disemba 2012, Mwanaidi alifanikiwa
kushika ujauzito kwa njia ya IVF. Iliwezekana baada ya mbegu za mume
wake na mayai yake (Mwanaidi) yaliyopevushwa, kutolewa na baadaye
kupandikizwa katika nyumba ya uzazi ya Mwanaidi.
"Baada ya mchakato huo kumalizika
nilitakiwa kuhudhuria kliniki kila wiki kwa ajili ya kuangaliwa jinsi
mimba inavyokua," anasema Mwanaidi.
Mwanaidi anasema katika ujauzito ule
hakuwa akiumwa au kupata matatizo yoyote kama ilivyokuwa kwenye ujauzito
wake wa kwanza. Alikuwa na hali ya kawaida kabisa kuliko alivyotarajia.
Anasema Profesa Kaisi alimwambia kuwa
huenda angejifungua Agosti 17, mwaka 2000 na ikawa hivyo. Alijifungua
siku hiyo saa 2:00 usiku kwa njia ya upasuaji.
"Namshukuru Mungu kuliko kawaida. Huu
kwangu ni muujiza na ninamshukuru sana Profesa Kaisi kwa uwezo ambao
Mungu amempa," anasema Mwanaidi.
Mwananidi anamwelezea mtoto wake kuwa ni mwenye nguvu, mwili mkubwa, na mcheshi.
"Ni mtoto wa kawaida kabisa, ana uwezo
mkubwa darasani na alifaulu vizuri mtihani wa darasa la saba. Ni mtoto
mwenye kumbukumbu za ajabu," anasema mama huyo wa Jumbe.
Mwanaidi anasema kwa kuwa sasa ana
watoto wawili, bado anatamani mtoto mwingine na anasema iwapo Profesa
Kaisi angekuwa hajapooza, angeomba apate mtoto mwingine kwa njia ya IVF.
"Kuugua kwa Prof. Kaisi ni pigo kwa
kila mtu. Wapo mamia ya wanawake wanaohitaji huduma za uzazi... kwa
kweli sijui itakuwaje," anasema.
Si hivyo tu. Mwanaidi anasema Profesa
Kaisi hakuwahi kuwalipisha hata senti tano ya matibabu tangu
alipofanyiwa upasuaji wa uvimbe hadi alipopata ujauzito kwa njia ya IVF.
Profesa Kaisi anasema hakuweza
kuwalipisha fedha katika mchakato huo kwa sababu matibabu hayo yalikuwa
chini ya programu iliyodhaminiwa na watu kutoka nje, ambao walilipia
gharama zote.
IVF hufanyikaje?
Profesa Kaisi anasema yai la mama
hupevushwa kwa kutumia dawa maalumu na hufuatiliwa kwa kutumia mashine
ya uchunguzi wa ndani ya mwili(Ultrasound).
"Baada ya yai kukomaa, sindano maalum
yenye wembamba mithili ya unywele huingizwa ukeni hadi kwenye mirija na
yai lililopevuka huchukuliwa na kutolewa nje," anasema.
Yai au mayai hayo huwekwa kwenye
chombo maalumu (test tube) kabla ya kuhamishwa kwenye beseni maalumu
ambalo hufanya yai liendelee kuwa hai licha ya kutoka nje ya mwili wa
binadamu.
"Beseni hilo halina budi kuwa na
mazingira kama ya mwilini. Kwa mfano joto, mwanga na kusiwepo na sauti,
kwani yai huweza kuharibika kwa kasoro ndogo ndogo sana," anasema.
Anasema wakati huo mbegu za mwanaume
hupimwa kama hazina walakini na hutolewa kwa mwanaume kujichua au kama
hawezi kujichua basi hutakiwa kufanya tendo la ndoa na mke wake na kisha
mbegu kukingwa kabla ya kuwekwa kwenye chombo maalumu.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment