Katika
hali ya kushangaza wenyeji timu ya Al Ahly mpaka sasa wameshindwa
kuwadhibitishia viongozi wa Young Africans pamoja na Ubalozi wa Tanzania
nchini Misri juu ya Uwanja utakaotumika kwa ajili ya mchezo wa
marudiano Klabu Bingwa Barani Afrika siku ya jumapili.
Sheria za mashindano ya CAF zipo wazi na zinaelekeza timu mwenyeji
wanapaswa kuwajulisha wageni uwanja utakaotumika kwa mchezo takribani
siku 10 kabla ya mchezo, huku mpaka leo siku ya jumatano takribani siku
nne kabla ya mchezo wakishindwa kutabanaisha mchezo utakapofanyika.
Mapema jana mchana Afisa Ubalozi wa Tanzania nchini Misri Bw Idrisa
Juma alifika makao makuu ya Al Ahly kuweza kujua taratibu za mchezo huo
lakini hakufanikiwa kupata majibu kamili zaidi ya kuahidiwa kufikia leo
mchana kwamba watakua wameshapata majibu juu ya ni sehemu gani mchezo
utafanyika.
Afisa Habari wa Young Africans Bw Baraka Kizuguto leo asubuhi
aliambatana na maofisa Ubalozi mpaka makao makuu ya klabu ya Al Ahly na
kukutana na meneja Said Abdoulaziz na meneja usalama Morgan na katika
mazungumzo hayo walisema mpaka muda huo walikuwa hawajapata maamuzi ya
serikali juu ya uwanja utakaotumika kwa mchezo.
“Tumeomba mchezo ufanyike kati ya Uwanja wa Cairo au mji wa
Alexandria lakini Serikali imekataa kutoa Viwanja yake pamoja na ulinzi
katika mchezo wetu kutokana na washabiki wetu kufanya vurugu kwenye
mchezo wa Super Cup dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia” alisema Said.
Katika kikao hicho kilichofanyika kwa zaidi ya masaa mawili Uongozi
wa Young Africans uliomba mchezo wake ufanyike jijini Cairo kwani ndo
sehemu waliyojiandaa kwa mchezo kufuatia taarifa ya Al Ahly walipokuja
Tanzania kwenye mchezo wa awali.
Mara baada ya mazungumzo hayo waliahidi kuongea na waziri mwenye
dhamana ya michezo kuruhusu mchezo ufanyike jijini Cairo na kwamba
mchezo huo kama iliyoamuriwa tangu awali na mamlaka husika ya ulinzi na
usalama hautakua na washabiki wowote kwa uwanja wowote utakaochezewa.
Akiongea na mtandano rasmi wa klabu ya Young Africans Kizuguto
amesema wamekaa kusubiria majibu ya Uwanja utakaotumika kwa mchezo zaidi
ya masaa 6 bila majibu huku viongozi hao wa Al Ahly wakipigiwa simu na
kutopokea.
“Tuliwaambia jiji la Cairol lina Viwanja zaidi ya 10 vyote vyenye
hadhi ya kimataifa sio lazima tucheze Cairo International, wajaribu
kuomba viwanja vingine lakini walionekana kutokua tayari na zaidi
kusisitiza watamuomba waziri wa michezo aruhusu mchezo ufanyike Cairo
bila washabiki” alisema Kizuguto
Kutokana na mazingira hayo ya ucheleweshwaji kutangaza sehemu
utakaofanyika mchezo Ubalozi wa Tanzania nchini Misri kupitia Balozi
wake Bw Mohamed Hamza na maafisa wake na uongozi wa Young Africans
umeendelea kufanya maandalizi kwa njia zote kuhakikisha timu inafika
salama na kupata huduma zote muhimu ikiwa ni pamoja na malazi, chakula,
uwanja wa mazoezi na ulinzi kwa kipindi chote timu itakapokuwa nchini
Misri.
Msafara wa watu 30 unatarajiwa kuwasili kesho alfajiri jijini Cairo
kwa shirika la Ndege la Egypt Air na kupokelewa Uwanja wa Ndege na
Balozi Hamza, pamoja na maafisa Ubalozi kisha kuelekea sehemu maalumu
ambayo timu ndipo itakapokua imeweka kambi mpaka siku ya mchezo.
0 comments:
Post a Comment