Wednesday, 8 January 2014

MWENYEKITI WA CHADEMA ATEKWA NA KUJERUHIWA VIBAYA


                             Joseph Yona

Mwenyekiti wa Wilaya ya Temeke wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Joseph Yona, ametekwa, kupigwa, kuumizwa na kisha kutupwa katika eneo la Ununio Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam na watu wasiojulika usiku wa kuamkia jana.

Yona anadaiwa kutupwa katika eneo la Maghorofa ya Wasomali, Kawe, na watu ambao amedai kutofautiana nao kimawazo kuhusiana na mvutano uliopo kati ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, na uongozi wa chama hicho.


Yona, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) Mkoa wa Dar es Salaam na Mjumbe wa Baraza Kuu la chama hicho Taifa, alikumbwa na masaibu hayo baada ya kutekwa akiwa nyumbani kwake, eneo la Kwa Azizi Ally, Temeke, saa 5:00 za usiku.


Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, alithibitisha Yona kukumbwa na masaibu hayo.


Katika tukio hilo, Yona ametobolewa na kitu chenye ncha kali juu ya jicho la kulia na kuchubuliwa sehemu mbalimbali za mwili.


Anapatiwa matibabu katika Taasisi ya Magonjwa ya Mifupa na Fahamu (MOI) Muhimbili.


KAULI YA YONA

Akizungumza na waandishi wa habari jana akiwa Moi, Yona alisema watu hao walimteka akiwa na wenzake wanne, na kusalimu amri.

Alisema watu hao walifika katika eneo alilokuwa wakiwa ndani ya gari linalofanana na la polisi na kumwambia wanampeleka kituo cha kati cha polisi.

Yona alidai watu hao walimchukua na kisha kumfunga uso kwa kutumia nguo yake na kuanza kumpiga.

“Niliomba wasiniue. Wamenipiga sana. Wamenichukua saa tano nyumbani kwangu Kwa Aziz Ally. Walikuwa na gari kama la polisi, lakini inaonekana siyo ya polisi. Wakasema tunakupeleka Central,” alisema Yona, ambaye alizungumza kwa tabu.


Aliongeza: “Tulikuwa wanne na hawakuhangaika na mtu mwingine. Wakanichukua mimi moja kwa moja. tulipopanda kwenye gari, wakachukua nguo yangu wakanifunga uso. Wakaanza kunipiga wakisema nisiwajibu na hawakuniambia chochote. Baadhi yao ninawajua.”


Aliyewahi kuwa mgombea ubunge Jimbo la Kibaha Mjini kupitia Chadema, Habib Mchange, ambaye ni jamaa wa karibu na Yona alidai taarifa za kutekwa kwa rafiki yake alizipata saa 9.45 usiku wa kuamkia jana.


Alisema muda huo alipigiwa simu na mtu mwenye lafudhi ya Kisomali kwa kutumia simu ya Yona, ambaye alimpa taarifa za kujeruhiwa kwa rafiki yake na kutupwa eneo la tukio.

Alidai baada ya kupata taarifa hizo, alikwenda eneo hilo kwa kutumia gari lake na kumkuta Yona akiwa hajiwezi kutokana na suluba aliyoipata.

“Baada ya kufika, nilizungumza na Yona akanieleza ilivyokuwa. Alinitajia hadi majina ya watu waliomteka, kumpiga, kumjeruhi na kumtupa eneo hilo. Alinieleza pia kuwa watu hao walimlazimisha awaonyeshe niliko ili wanifuate kunidhuru na mimi pia,” alidai Mchange.



MOI WANENA

Afisa Habari wa Moi, Patrick Mvungi, alisema kabla ya kupelekwa Moi, Yona alipokelewa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jana asubuhi, ambako alifanyiwa kipimo kikubwa cha kichwa cha CT-Scan.

Mvungi alisema baadaye alihamishiwa MOI, ambako anaendelea kupatiwa matibabu.

“Tumempokea leo (jana) kwenye saa 5:00 akitokea Muhimbili baada ya kufanyiwa kipimo cha CT- Scan. Kwa sasa anaendelea na matibabu,” alisema Mvungi.

CHADEMA YALAANI

Nayo Chadema imesema imepokea kwa mshtuko taarifa za tukio la kutekwa, kuteswa na kuumizwa kwa Yona na kuliita kuwa ni la kihuni.

“Chama kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano na Uhusiano, mbali ya kukemea kwa nguvu zote tukio hilo la kihuni na mengine ya namna hiyo yenye lengo ya ukatili dhidi ya binadamu,” ilieleza sehemu ya taarifa ya Chadema kwa vyombo vya habari jana.


Kutokana na hali hiyo, Chadema imelitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi juu ya tukio hilo ili ukweli ujulikane na haki itendeke kwa sheria kuchukua mkondo wake.

Pia imewataka wanachama na Watanzania kwa jumla kutulia, hasa pale watu wenye hila na malengo yao wanapoanza kukihusisha chama na tukio hilo.

“Watambue kuwa pamoja na mtu yeyote kuwa kiongozi wa chama, bado anayo maisha yake na uhusiano na watu wengine katika jamii,” ilieleza taarifa hiyo ya Chadema na kuongeza:


“Jeshi la Polisi linapaswa kuyachukulia uzito mkubwa na unaostahili matukio ya namna hii, ambayo yanaanza kuota mizizi kutokana na watu waovu wanayoyatekeleza kutochukuliwa hatua za kisheria, ambazo zingesaidia kuzuia yasitokee tena.”


“Watanzania bado wanakumbuka kwamba, hadi sasa Jeshi la Polisi limeshindwa kutoa taarifa za kina na kuchukua hatua za kisheria, ambazo zingesaidia ukweli kujulikana na haki kutendeka katika matukio ya kutekwa na kuteswa kwa kiongozi wa madaktari Dk. Steven Ulimboka na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda. Hivyo ingesaidia kuzuia matukio mengine kutokea.”


“Ni kutokana na jeshi hilo kushindwa kuwajibika ipasavyo katika matukio mengine ya namna hiyo, watu waovu wanaweza kutumia mwanya wa kinachoendelea ndani ya Chadema kwa chama kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wanachama wasio waadilifu, kufanya matukio ya namna hiyo ili kujenga taswira ya kukihusisha chama na uhuni huo unaobeba kila sifa ya kuitwa ukatili dhidi ya binadamu.”



ZITTO ALAANI

Zitto alisema kupitia mtandao wa kompyuta kuwa siku zote vurugu kamwe haziwezi kuwa suluhisho katika siasa.

Alisema siku zote vurugu husababisha hofu kwa watu.

“Ninalaani kwa nguvu zangu zote kitendo hiki cha kihalifu kilichofanywa dhidi ya Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Temeke, Yona,” alisema Zitto, na kuongeza kuwa yaliyompata Yona ni kutokana na kupinga maamuzi ya kamati Kuu ya kuwavua uongozi baadhi ya wanachama.


KOVA AZUNGUMZA

Kamanda Kova alisema watu sita waliojitambulisha kama maaskari polisi, walimkuta Yona akinywa katika grosari ya Mgumbini na kumtaka kwenda kituo cha polisi wakidai anahitajika.

Lakini alisema baada ya Yona kuwatilia shaka watu hao, ambao mmoja alikuwa akimfahamu kama mwanachama wa Chadema, alipouliza ndipo walipomkamata na kumpandisha kwenye gari aina ya Land-Cruser na kumfunga kitambaa cheusi usoni.


Alisema katika mahojiano na polisi baada ya kupata fahamu majira ya saa 9:00 usiku jana, Yona alidai watu hao walikuwa wakimuuliza kwanini anaendelea kumshabikia Zitto wakati ni msaliti katika chama na pia kumtaka awaonyeshe alipo rafiki yake, aitwaye Habibu Mchange.


Alisema Yona alipohoji kuwa “mbona polisi hawafiki” ndipo walipompiga hadi kupoteza fahamu na kumtupa katika pori la Ununio.


Alisema baada ya kupata fahamu, aliomba msaada kwa mlinzi aitwaye, Ismail Swalehe, ambaye alimpeleka kwa Mwenyekiti wa serikali ya Mtaa Ununio.


“Ndipo walipotoa taarifa polisi na kufika Kamanda wa Kinondoni, Camilius Wambura, kumhoji na kueleza yaliyomkuta,” alisema Kamanda Kova.


Alisema Yona amejeruhiwa, ikiwa ni pamoja na kutobolewa na kitu chenye ncha kali juu ya jicho la kulia na kuchubuliwa sehemu mbalimbali za mwili na sasa anapatiwa matibabu MNH.


“Matendo kama haya hayawezi kuvumilika. Yeyote anayehusika ajue kuwa atachukuliwa hatua bila kujali cheo wala wadhifa wake katika jamii,” alisema Kamanda Kova.


Aidha, Kamanda Kova alisema Jeshi la Polisi tayari limeunda jopo la wapelelezi wanane linaloongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu, Jaffari Mohamed, kushughulikia suala hilo.


Imeandikwa na Muhibu Said, Samson Fridolin na Loveness Massero. 
SOURCE: NIPASHE
8th January 2014

0 comments: