
Dar es Salaam.Tukio la
Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Temeke, Joseph Yona kutekwa nyara,
kupigwa na kutupwa katika vichaka eneo la Tegeta na watu aliodai kuwa ni
wafuasi wa chama hicho, limekichanganya Chadema baada ya jana kudai
kuwa tukio hilo limefanywa na Jeshi la Polisi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa
Chadema Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Henry Kilewo alitolea mfano
matukio kadhaa yaliyowakuta wanachama wa chama hicho waliopigwa na
polisi, kisha kulazimishwa kukiri kuwa walitumwa na viongozi wa Chadema
kutekeleza matukio ya uhalifu.
Alisema kutokana na kitendo hicho, polisi
inatakiwa kuchunguza na kutoa majibu sahihi huku akisisitiza kuwa hakuna
mwanachama wa Chadema mkoani Dar es Salaam anayeweza kufanya tukio la
aina hiyo.
Kilewo alitolea mfano matukio ya aina hiyo
aliyodai kuwa yalifanywa na jeshi la polisi, yaliyowakuta aliyekuwa
Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari, Dk Stephen Ulimboka, kifo cha
mwandishi wa habari Channel Ten, Daudi Mwangosi na sakata la Mhariri
Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006), Absalom Kibanda.
Yona ambaye ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Chadema kwa
sasa amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), alikamatwa
juzi na kisha kupigwa na baadaye kutupwa eneo la Tegeta Ununio na watu
aliodai kuwa ni wafuasi wa Chadema.
Alisema watu hao walimtaka aache kuishambulia
Kamati Kuu ya chama hicho iliyomvua madaraka aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu
wa chama hicho, Zitto Kabwe na kuwafukuza uanachama Dk Kitila Mkumbo
(aliyekuwa Mjumbe Kamati Kuu) na Samson Mwigamba (aliyekuwa Mwenyekiti
Chadema-Arusha).
Katika ufafanuzi wake Kilewo alisema: “Mwaka jana
na mwaka juzi yalitokea matukio mengi ya aina hii. Kama mtakumbuka
polisi waliwahi kumkamata mwanachama wa Chadema, Evodius Justinian na
wenzake na kuwatesa, baadaye kuwashinikiza wakiri kuwa viongozi wa
Chadema ndiyo waliwatuma kutekeleza matukio ya uhalifu.”
Aliongeza: “Kanda ya Dar es Salaam tunakijua chama
vizuri, kimekuwa mstari wa mbele kutetea haki za binadamu, kupinga
ukatili na uhuni hivyo hakiwezi kumtuma mtu yeyote kufanya vitendo kama
hivyo vya utekaji, utesaji ama udhalilishaji wa aina yoyote.”
Chadema kipo tayari kuwachukulia hatua kali
wanachama wake wasaliti na wanafiki na kwamba hakiwezi kumvumilia mtu
yoyote anayehusiana na chama hicho endapo kitabaini kuwa amehusika
katika tukio la kupigwa kwa Yona.
Alisema kuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar
es Salaam, Suleiman Kova anatakiwa kuacha kulitumia jeshi hilo kama
kitengo cha propaganda za kisiasa, baada ya kamanda huyo kueleza kuwa
Yona alidai kuwa amepigwa na wafuasi wa Chadema.
Katika maelezo yake ya juzi, Kamanda Kova alisema
kufuatia tukio hilo ameunda jopo la wapelelezi wanane watakaoongozwa na
Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi
wa Polisi (ACP), Jaffari Mohamed kuchunguza tukio hilo.
Chanzo Na Fidelis Butahe, Mwananchi
Posted
Alhamisi,Januari9
2014
0 comments:
Post a Comment