Saturday, 1 March 2014

MKULIMA AKAMTWA NA BANGI MISOKOTO 888 YENYE UZITO GRAMU 44 MKOANI SINGIDA

DSC001791
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Singida,SACP Geofrey Kamwela.
Na Nathaniel Limu, Singida
JESHI la Polisi mkoa wa Singida linamshikilia Mariamu Songeraeli (32) mkulima mkazi wa kijiji cha Nselembwe wilaya ya Iramba kwa tuhuma ya kumiliki madawa ya kulevya aina ya bhangi misokoto 88 yenye uzito wa gramu 44.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Singida,SACP Geofrey Kamwela amesema mtuhumiwa Mariamu amekamatwa juzi saa 11.30 jioni nyumbani kwake katika kijiji cha Nselembwe kata ya Shelui wilaya ya Iramba.
Amesema askari polisi waliokuwa kwenye doria siku ya tukio,walipata taarifa kutoka kwa raia wema kwamba mtuhumiwa Mariamu anajihusisha na biashara haramu ya kununua na kuuza bhangi.
Kamwela amesema askari hao waliweza kwenda nyumbani kwa mtuhumiwa na kuipekua na kisha kuikuta misokoto hiyo ya bhangi ikiwa chumbani kwake,imefichwa kwenye mfuko wa rambo.
“Tunamshikilia mtuhumiwa kwa uchunguzi zaidi,ili kujua ni wapi anakoitoa bhangi hiyo na watu anaoshirikiana nao katika bishara hiyo haramu,baada ya uchunguzi huo kukamilika,atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma inayomkabili”,amesema.
Aidha,Kamwela ametumia fursa hiyo kuwashukuru na kuwapongeza raia wema kwa kutoa taarifa sahihi za uhalifu na wahalifu,na kuwaomba waendelee na moyo huo huo,kwa madai kwamba suala la usalama ni la wananchi wote kwa ujumla.

0 comments: