.
Bara la Afrika linasherehekea hivi
sasa miaka 50 ya Umoja wa Afrika kwa ufanisi tangu wa kisiasa mpaka wa
kiuchumi. Bara hilo linajitokeza kama eneo lenye fursa kubwa ya
kuwavutia wawekezaji. Baada ya "Chui wa Asia" sasa Simba wa Afrika
wananguruma.
Takwimu zinadhihirisha uchumi utakuwa
mwaka huu kwa 7% au zaidi katika robo ya mataifa yote ya eneo la kusini
mwa jangwa la Sahara. Wakati huo huo, mengi ya mataifa hayo yamo katika
lile kundi la mataifa ambayo uchumi wake unakuwa haraka kupita kiasi.
Waafrika wawili kati ya watano wana
simu ya mkononi au Smartphone. Nguvu za ununuzi zinazidi kukuwa barani
Afrika na masoko yanaongezeka, huku matajiri wakizidi kuongezeka barani
humo. Huu ni ufanisi wa kusisimua ambao watu wanapenda kuuzungumzia –
naiwe wanasiasa, wanauchumi na pia vyombo vya habari.
"Afrika inajikwamua", anasema
mwandishi habari wa masuala ya kiuchumi Anver Versi. Mkenya huyo
anaemiliki jarida la kiuchumi la African Business Magazine
linalochapishwa mjini London anasema: "Kuna sababu nzuri za kuhoji
kwamba Afrika itageuka kuwa soko muhimu la ukuaji wa kiuchumi katika
miaka 50 inayokuja .Kwa sababu Afrika ina mali ghafi na nguvu kazi. Mtu
anaweza kusema Afrika ni mahala pa kuvutia kabisa kuwekeza hivi sasa -
Wachina wameitambua hali hiyo tangu miaka 10 au 15 iliyopita. Na sasa
wajasiriamali wa Kijerumani na wazungu kwa jumla wanabidi wazindukane na
kuitambua fursa hiyo."
Kwa mujbu wa makadirio ya Benki Kuu ya
Dunia, uchumi katika eneo la kusini mwa jangwa la Sahara utakuwa kwa
kadiri ya 5% katika kipindi cha mwaka 2013 na 2015. Uchumi wa dunia
katika kipindi hicho hicho utakuwa kwa kadiri ya 3% tu.
"Viwango hivyo ni vya juu vya ukuaji
wa kiuchumi, lakini hiyo bado si sababu ya kushangiria," anasema Robert
Kappel. Mtaalam huyo wa Kijerumani anayeshughulikia masuala ya utafiti
wa masuala ya Afrika katika taasisi ya GIGA mjini Hamburg, amechunguza
makadirio ya ukuaji wa kiuchumi katika mataifa 42 ya kusini mwa jangwa
la Sahara. Mengi ya mataifa hayo hayatofua dafu kwa mlinganisho wa
kimataifa.
Robert Kappel anasema: "Ukuaji
unatokana zaidi na ile hali kwamba mahitaji ya mali ghafi na bidhaa za
mashambani yameongezeka sana katika kipindi cha miaka iliyopita na kwa
namna hiyo bei nazo zimepanda. Kwa hivyo, inamaanisha biashara ya nje
inachangia sana katika ukuaji wa kiuchumi barani Afrika na huo ni
udhaifu mkubwa."
Taasisi kuu za fedha duniani, Shirika
la Fedha la Kimataifa na Benki Kuu ya Dunia, zote zinaonya juu ya bara
la Afrika inategemea sana biashara na nchi za nje. Naye Katibu Mkuu wa
zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, aliyataka mataifa ya viwanda
katika Kongamano la Kiuchumi la Kimataifa hivi karibuni mjini Cape Town
nchini Afrika ya Kusini yawekwe sheria kali katika biashara ya mali
ghafi pamoja na Afrika. "Rushwa na kukwepa kulipa kodi za mapato,"
anasema Kofi Annan, "ndio chanzo cha kudhoofika neema barani Afrika."
Shughuli za viwanda zinazorota barani
Afrika na kilimo hakitoshi hata kukidhi mahitaji ya wakaazi wa bara
hilo. Hata katika soko la ajira hakuna ishara ya kuongezeka nafasi za
kazi. Hata katika nchi inayonyanyukia kiuchumi ya Afrika ya Kusini,
zaidi ya 25% ya wakaazi wake hawana kazi na wanaoathirika zaidi ni
vijana wanaoishi mashambani.
Kwa hivyo, nini cha kufanya ili ukuaji
wa kiuchumi barani Afrika utuwame katika msingi imara? Mwandishi habari
wa masuala ya kiuchumi, Anver Versi, anahisi panahitajika vitega uchumi
zaidi katika miundo mbinu. Naye Robert Kappel wa Taasisi ya Uchunguzi
wa Masuala ya Afrika anahisi mageuzi ya kiuchumi pia yanahitajika pamoja
na sheria bora za uwekezaji ili kuwavutia wateja tangu wa ndani mpaka
wa kimataifa.












0 comments:
Post a Comment