Amri hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mfawidhi, Isaya Arufani, kwa ajili ya usalama wa mashahidi hao wa upande wa Jamhuri.
Hata hivyo shahidi wa pili wa upande
wa Jamhuri, alidai washitakiwa hao ambao ni Huang Gin, Xu Fujie na Chen
Jinzha, walitoa hongo ya Sh milioni 30.2 kwa polisi na askari wa Wanyama
Pori ili wasipekue nyumba waliyokuwa wakiishi iliyopo mtaa wa Kifaru,
Mikocheni Dar es Salaam.
Wanadaiwa walikutwa na nyara za
Serikali, ambazo ni vipande 706 vya meno ya tembo vyenye uzito wa
kilogramu 1,880, vyote vikiwa na thamani ya Sh bilioni 5.4.
Shahidi huyo alidai wakati wakiendelea
kufanya upekuzi kwenye nyumba waliyokuwa wakiishi washtakiwa hao,
mshtakiwa Huang Gin alivuta droo na kutoa bahasha iliyokuwa na fedha
ndani, ambazo walipozihesabu zilikuwa ni Sh milioni 30.2, kama
kishawishi cha kuwataka wasiendelee kuipekua nyumba hiyo.
“Tuliendelea kufanya upekuzi kwenye
nyumba hiyo, tukakuta kuna makontena yamepangwa chini manne, juu yake
matatu, tuliyafanyia upekuzi na mojawapo lilikuwa na vipande 706 vya
meno ya tembo ambayo yalikuwa yamehifadhiwa kwenye mifuko ya viroba 54,”
aliieleza Mahakama.
Aliongeza kudai kuwa mbali na meno
hayo ya tembo, pia walikamata mizani tatu, kompyuta mpakato na magari
matatu, yaliyokuwa yakihusishwa kutumika kwenye biashara hiyo haramu.
Shahidi huyo aliieleza Mahakama kuwa
wakati yote hayo yakiendelea mshtakiwa wa kwanza na wa pili, walikuwa
wakizungumza Kiswahili huku mshtakiwa wa tatu alikuwa akizungumza
Kiingereza.
Alidai baada ya kuwaweka washtakiwa
hao chini ya ulinzi na kuwapeleka katika kituo cha Polisi cha Oysterbay
kwa ajili ya mahojiano, walibadilika na kuwa hawawezi kuongea Kiswahili
wala Kiingereza, kitu ambacho kiliwalazimu kumtafuta mkalimani.
Walimtafuta mkalimani, wakahojiwa na
hatimaye wakafunguliwa mashtaka yanayowakabili na kwamba meno hayo ya
tembo yamehifadhiwa kwenye ghala la Hifadhi ya Taifa ya Meno ya Tembo.
Kukamatwa kwa washtakiwa hao ni baada
ya timu ya shahidi huyo ya polisi, akishirikiana na askari kutoka Idara
ya Wanyama Pori kupata taarifa ya siri, iliyowaeleza kuwa kuna raia
watatu wa China, wanajihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo na
kwamba walikuwa wakitumia magari matatu kwa nyakati tofauti. CHANZO:HABARILE












0 comments:
Post a Comment