MSHABIKI MBARONI KWA MADAI YA TIKETI FEKI
Mshabiki mmoja anashIkiliwa
na Jeshi la Polisi akidaiwa kukutwa na tiketi bandia kwenye mechi ya
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Yanga na Simba iliyochezwa jana
(Februari 2 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Matei
Cosmas (28) ambaye ni mkazi wa Buza Njiapanda Kitunda, Dar es Salaam
amefunguliwa jalada namba CHA/IR/900/2014 kwenye Kituo cha Polisi
Chang’ombe akidaiwa kupatikana na tiketi bandia.
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) leo asubuhi (Februari 3 mwaka huu)
limeamkia Kituo cha Polisi Chang’ombe kusaini hati ya maelezo dhidi ya
mtuhumiwa.
Ni imani ya Shirikisho kuwa mtuhumiwa atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za nchini.
Tunatoa
mwito kwa washabiki wa mpira wa miguu kuepuka kununua tiketi kutoka
mikononi mwa watu, kwani kufanya hivyo ni kosa. Tiketi zinauzwa kwenye
sehemu maalumu zenye chapa ya TFF.
RAIS WA TFF ATEMBELEA RUANGWA
Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi
ametembelea Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.
Katika
ziara hiyo aliyoifanya jana (Februari 2 mwaka huu), pia alikuwa mgeni
rasmi mechi ya kugombea Kombe la Majaliwa kati ya Hull City na Mbagala
City, na kuahidi kuwa TFF itaandaa kozi za awali za ukocha na uamuzi kwa
Wilaya ya Ruangwa.
RAMBIRAMBI MSIBA WA OMARI CHANGA
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha
aliyekuwa mchezaji wa Vijana, Moro United na Yanga, Omari Changa
kilichotokea juzi (Februari 1 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
Msiba
huo ni mkubwa katika familia ya mpira wa miguu kwani Changa wakati wake
uwanjani akichezea timu mbalimbali alitoa mchango mkubwa ambao
tutaukumbuka daima.
TFF
tunatoa pole kwa familia ya marehemu Changa, klabu ya Moro United na
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na kuwataka kuwa
na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Katika maziko TFF itawakilishwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Kidao Wilfred, na imetoa rambirambi ya sh. 200,000.
0 comments:
Post a Comment