....................................................
Na Mwandishi maalum Dodoma
*Ni maandalizi ya Bunge la Katiba
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema
ameridhishwa na kazi ya ukarabati inayoendelea kwenye maeneo mbalimbali
ya jengo la Bunge ikiwa ni maandalizi kwa ajili ya Bunge la Katiba.
“Maendeleo ni mazuri na kazi
inayofanywa ni nzuri, kikubwa ni kuhakikisha mnaikamilisha hii kazi
katika muda uliopangwa,” alisisitiza.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo
asubuhi (Jumamosi, Januari 18, 2014), wakati akipokea maelezo ya
ukarabati kutoka kwa Mhandisi Mkuu wa Ofisi Bunge, Eng. Dk. Philemon
Mzee ambaye alikuwa akimtembeza kwenye maeneo mbalimbali yanayofanyiwa
ukarabati.
Kwa mujibu wa Dk. Mzee, kazi hiyo
inatarajiwa kukamilika Januari 30, mwaka huu.
Ndani ya ukumbi wa Bunge, Waziri Mkuu alikuta viti vyote vya zamani
vimekwishaondolewa na akaonyeshwa sehemu moja ya mfano iliyopangwa viti
vinane kuashiria muonekano utakavyokuwa mara baada ya kazi hiyo
kukamilika.
Dk. Mzee alimweleza Waziri Mkuu kwamba
wanatarajia kuweka viti 670 vya wajumbe wa kawaida pamoja na viti 24 kwa
ajili ya wajumbe wenye mahitaji maalum.
“Kule nyuma tutaweka viti vya kuzunguka
ili hata kama mjumbe mmoja ana ulemavu wa miguu na amekuja na baiskeli
yake aweze kutoka na kukaa kwenye kiti chake kwa urahisi,” alisema.
Alimweleza Waziri Mkuu kwamba viti vya
Spika na Makatibu wa Bunge vipo tayari, mfumo wa vipaza sauti uko sawa
na kwamba kila kipaza sauti kimoja kitakuwa kinatumiwa na watu wawili
kulingana na mpangilio wa ukaaji ulivyo.
Alipoulizwa na Waziri Mkuu kuhusu sehemu ya kukaa waandishi wa habari, Eng. Mzee alisema sehemu zao zitaendelea kubaki zilivyo.
Alipohoji endapo kutakuwa na kazi za
Kamati, zitafanyikia wapi, Waziri Mkuu alijibiwa kwamba kuna kumbi tisa
za kutosha watu 25-30 zinaandaliwa katika jengo la utawala Annex.
Waziri Mkuu pia alikagua sehemu ya
mgawaha kwa ajili ya wajumbe wa bunge hilo na kuonyeshwa sehemu ya
basement ambayo alikuta inafanyiwa matengenezo ili iweze kuchukua watu
500 kwa wakati mmoja.
Pia alikagua mgahawa wa zamani wa
bungeni na kuelezwa kwamba utatumiwa na watumishi tu na hivi sasa
unafanyiwa ukarabati ili uweze kutosha watu 120 kwa wakati mmoja.
Waziri Mkuu alikagua pia chumba cha
Hansard ambako alielezwa kuwa kimeongezwa ili kiweze kutosha watumishi
80 ikilinganishwa na watumishi 25 waliokuwepo zamani. Pia alikagua
server room ambayo imehamishiwa eneo yalipokuwa matawi ya benki na
zahanati.
Alipouliza kuhusu eneo la kuegeshea
magari, Waziri Mkuu alielezwa kwamba limetengwa eneo la kutosha magari
400 ambalo hivi sasa linafanyiwa maandalizi.
Katika jengo la Utawala Annex, Waziri Mkuu alielezwa jengo hilo litakuwa
na ofisi, vyumba vya mazoezi (gym), zahanati na ofisi za kutolea huduma
za kibenki.
Akitoa maelezo kuhusu kazi ya ukarabati
inayoendelea, Kamishna Msaidizi wa Magereza ambaye ni msimamizi wa
ujenzi wa jengo la Utawala Annex, Eng. Salum Omari alisema walianza kazi
hiyo Januari 2, mwaka huu na wanatarajia kuikamilisha ifikapo Februari
2, mwaka huu.
Alipoulizwa kama watamudu kuikamilisha
kazi hiyo katika tarehe iliyopangwa, Eng. Omari alimhakikishia Waziri
Mkuu kwamba wataikamilisha katika muda huo.
Waziri Mkuu amerejea jijini Dar es Salaam mchana huu.
0 comments:
Post a Comment