Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila ameeleza namna alivyoibua sakata la uchotwaji wa Sh306 bilioni kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow na kudokeza kuwa kitendo cha baadhi ya watuhumiwa kugoma kujiuzulu, kinaonyesha kuna watu zaidi wanahusika.
Kafulila (32), ambaye alikuwa akiulizia suala hilo kila mara bungeni hadi uamuzi wa kulijadili ulipofikiwa, amesema ataendelea kulifuatilia hadi aone mwisho wake.
Akaunti hiyo ilifunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuhifadhi fedha za malipo ya tozo ya ufuaji umeme baada ya Tanesco kuingia kwenye mgogoro na Kampuni ya IPTL na suala hilo kupelekwa mahakamani.
Kwa mujibu wa masharti ya uendeshaji wa akaunti za escrow, fedha hizo zilitakiwa zitolewe baada ya Mahakama kutoa uamuzi wa mgogoro huo, lakini wakati ilitaka pande hizo mbili zikutane na kukokotoa viwango vya tozo hizo, fedha hizo zilitolewa na kulipwa kwa mmiliki mpya wa Kampuni ya Pan African Power Solutions (PAP), jambo lililosababisha kuibuka kwa kashfa hiyo.
Akizungumza kwenye mahojiano maalumu na gazeti hili jana, Kafulila alisema alilinasa suala hilo kwenye vyombo vya habari na baadaye kupewa kurasa nne za maelezo ya sakata hilo, lakini baada ya kuliingiza kwenye chombo hicho cha kutunga sheria, wabunge wenzake waliendelea kumwongezea nyaraka hadi zikafikia kurasa 604.(P.T)
"Lilikuwa ni jambo la furaha kwangu kuona kwamba wabunge wenzangu wamenipa nyaraka nyingi pamoja na kwamba walishakuwa nazo awali, lakini hawakuwa wametaka kuzitoa hadi nilipoingiza suala hili bungeni," alisema Kafulila ambaye aliingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2010... "Nyaraka hizi zilinisaidia sana."
Kupata ufahamu wa suala hilo kulikuwa kama bahati kwa mbunge huyo. "Nilianza kulifahamu suala la escrow nikiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wakati nikienda Uswisi. Lilikuwa limeandikwa katika gazeti (jina tunalo) ambalo katika ukurasa wake wa kwanza walikuwa wamechora skendo mbalimbali za IPTL, kuanzia mwaka 1995 hadi 2014," alisema.
Aliongeza kuwa alipotoka safari aliikuta habari hiyo ikiwa imeandikwa kwa kina katika gazeti The Citizen na hivyo kumfanya ajenge hamu ya kutaka kujua undani wake. Alisema alianza kulifuatilia suala hilo kwa kuwasiliana na mmoja wa mawaziri wa Wizara ya Nishati na Madini ambaye awali alikuwa na utaratibu wa kumjulisha kila jambo linalofanywa na wizara hiyo.
"Nilimweleza mambo ambayo wizara inatakiwa kuyajibu kuhusu wizi wa fedha hizo ambao unaandikwa katika magazeti. Alinijibu kuwa wanaoandika habari hizo ni wababaishaji na wanaandika vitu wasivyovijua," alisema.
Alisema kutokana na unyeti wa suala hilo na sifa walizokuwa wakipewa watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini, hakukata tamaa na kuamua kulipeleka suala hilo bungeni ili litolewe ufafanuzi wa kina.
"Kabla ya mkutano wa Bunge kuanza nilimtafuta mtu mmoja (anamtaja jina) ambaye alinipa kurasa nne tu kuhusu IPTL na escrow tena kwa siri kubwa. Nilipozisoma nilielewa suala hilo. Mei mwaka huu wakati nikichangia hotuba ya Waziri Mkuu bungeni niliibua sakata hilo na kutaja majina ya wahusika," alisema.
Chanzo: Fidelis Butahe, Mwananchi
0 comments:
Post a Comment