Vinara wa ligi kuu Tanzania Bara, Mtibwa Sugar wameingia kambini kuanza upya ujenzi wa timu yao baada ya mwezi mmoja wa kusimama kwa ligi kuu kuelekea ukingoni. Mtibwa chini ya kocha, Mecky Mexime imeanza mazoezi wiki hii katika uwanja wake wa Manungu Complex huku kiungo wa zamani wa Simba SC na Kongsvinger ya Norway, Henry Joseph Shindika akiwepo.
Shindika ambaye alimaliza mkataba wake na Simba mara baada ya kumalizika kwa msimu wa 2013/14 yuko katika mazungumzo ya mwisho ya kusaini mkataba wa kazi na mabingwa hao wa zamani wa Tanzania Bara. Mexime amemuita kiungo huyo ambaye alimuachia beji ya unahodha wa timu ya Taifa, Taifa Stars wakati alipostaafu soka la kimataifa mwaka 2009.
” Naendelea vizuri na mazoezi katika timu ya Mtibwa. Mungu akijalia nitafanya kazi na Mtibwa Sugar. Wao ndiyo wameniita, nami nahitaji kufanya kazi katika klabu hii, nashukuru kwa kuniita kwao, napenda namna wanavyoishi na wachezaji wao, ni sehemu ambayo nahitaji
kufanya kazi” anasema, Shindika ( 28 ) mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania.
Mtibwa inawakosa wachezaji wake watano ambao wameitwa katika kikosi cha timu ya pili ya Taifa ‘ Stars Maboresho’, na jambo hilo halijampendeza Mexime kwa sababu wachezaji hao wamechukuliwa wakati muhimu wa maandalizi na wanakwenda timu ya Taifa kucheza nje ya kalenda ya FIFA.
” Ndiyo kwanza tunaanza maandalizi ya kutengeneza tena timu, lakini mtu anakuja na kuchukua wachezaji watano, sitazungumzia sana kuhusu hilo ni jambo la kuachana nalo” anasema, mwalimu Mexime. Nahodha wa timu hiyo Shaaban Nditti amekuwa akitajwa kuhitajika na Marcio Maximo kocha wa Yanga SC, na mshambulizi, Ame Ally na mlinzi Salim Mbonde wamekuwa wakitajwa kutakiwa na Simba SC, lakini Mexime anapigilia msumali na kusema; ” Hakuna mchezaji atakayeuzwa, hatufanyi biashara”
0 comments:
Post a Comment