Walemavu wakiwa katika maandamano yao leo
Askari wa usalama barabara Iringa aliyefahamika kwa jina la Sarehe Mollel akiongoza maandamano ya watu wenye ulemavu leo wakati wa maadhimisho ya siku ya walemavu duniani yaliyofanyika kitaifa katika viwanja vya kichangani mjini Iringa na kuhudhuriwa na waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu sera na uratibu wa bunge Bw Wiliam Lukuvi kwa niaba ya waziri mkuu Mizengo Pinda
Waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu sera na uratibu wa bunge Bw Wiliam Lukuvi akimkabidhi cheti cha ushiriki Tumain Mdegella kwa niaba ya ofisi za Neema Crafti mjini Iringa wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya walemavu duniani iliyofanyika kitaifa mjini Iringa
Na MatukiodaimaBlog
SERIKALI imeziagiza mamlaka za usafiri wa majini na nchi kavu (SUMATRA ) nchini kuanza mchakato wa kukaa na wamiliki wa vyombo hivyo ili kuanza uangizaji wa vyombo vya usafiri yakiwemo mabasi ambayo ni rafiki na walemavu nchini huku ikipiga marufuku majengo ya serikali kujengwa bila kuwepo kwa mchoro unaoonyesha mazingira yanayozingatia makundi yote ya jamii likiwemo la walemavu wa viungo .
Agizo hilo limetolewa na waziri mkuu Mizengo Pinda wakati wa maadhimisho ya siku ya walemavu duniani yaliyofanyika kitaifa katika viwanja vya kichangani mkoani Iringa jana.
Akiwahutubia walemavu hao na wananchi waliofika katika viwanja hivyo waziri mkuu ,aliyewakilishwa na waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu (sera na uratibu wa bunge) ,Wiliam Lukuvi ambae ni mbunge wa jimbo la Isimani mkoani Iringa alisema kuwa kimekuwepo kilio cha muda mwingi kutoka kwa walemavu juu ya kusaulika katika ujenzi wa majengo mbali mbali ambayo yamekuwa yakijengwa bila kuzingatia kundi la watu wenye ulemavu jambo ambalo ni sawa na kuwabagua watu hao.
Hivyo alisema katika kuona kilio hicho cha walemavu kinafanyiwa kazi kuanzia sasa majengo yote ya serikali zikiwemo shule na taasisi nyingine kabla ya kuanza ujenzi wake lazima wasimamizi wa ujenzi huo kujiridhisha kwa mchoro ambao utaonyesha mazingira yatakayomuwezesha mlemavu kutumia jingo hilo bila usumbufu tofauti na ilivyo sasa ambapo idadi kubwa ya majengo mazingira yake si lafiki kwa walemavu.
” Ni siku nyingi watu wenye ulemavu wamekuwa wakilalamika juu ya mazingira yasiyo rafiki katika majengo mbali mbali …..sasa leo naomba kuagiza kuwa michoro yote inayochorwa katika majengo ya huduma za kijamii ni marufuku kupitishwa ama wasimamizi wa ujenzi husika kuruhusu ujenzi iwapo mchoro hauonyeshi kama utayajali makundi yote wakiwemo walemavu…..wasimamizi wote msikubali kusimamia wala kutangaza tenda ya ujenzi kama ramani yake si rafiki kwa walemavu…..lakini pia hata kwenye mabasi hivi unamtegemea mtu mwenye ulemavu wa miguu ataingia vipi na baiskeli yake katika gari iwapo hakuna mazingira yanayomwezesha kuingia …. hivi sasa teknlojia imezidi kukua na baadhi ya nchi wameanza muda mrefu kuwajali walemavu kwa kuwa na mabasi ambayo mlemavu anaingia na baiskeli yake na kushuka nayo bila usumbufu ni vema hata Sumatra kuangalia uwezekano wa kuwajali walemavu hao . pia ni vizuri hata nyumba za ibada nazo ningeshauri baba askofu kuangalia kuweka mazingira ” alisema Lukuvi.
Kuhusu ombi la walemavu hao hasa wale wasio sikia kuomba serikali kuwa na wakalimani katika kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC) na vituo vingine vya luninga ili kuwawezesha walemavu hao nao kuweza kufuatilia hotuba ya Rais mwisho wa mwezi na mambo mengine badala ya kutengwa ,alisema kuwa suala hilo ni wajibu wa serikali kuwajali watu wake hivyo tayari imeuagiza uongozi wa TBC na mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA) kulitafutia ufumbuzi suala hilo la mkalimani hasa katika TBC .
Katika hatua nyingine Lukuvi aliwataka walemavu hao ili ombi lao la kutazamwa katika nafasi za uongozi liweze kuzingatiwa ni vema wao wenyewe kujitokeza kwa wingi kuipigia kura katiba iliyopendekezwa pindi itakapokuja kwa wananchi kwa madai kuwa katika katiba hiyo imezingatia mambo mengi ya kijamii likiwemo la kuwajali watu wenye ulemavu kwa kuwatengea nafasi nyingi zaidi na iwapo katiba hiyo itapitishwa kazi ya msuguano wa rushwa unaweza kuhamia kwa walemavu kwa kila mmoja kutaka kupewa nafasi.
” Hadi hivi sasa ni chama cha mapinduzi (CCM) pekee ambacho kina wabunge wa viti maalum wa kuteuliwa kutoka kundi la walemavu huku vyama vingine vyote havijawakumbuka kabisa watu wenye ulemavu ukiacha mbunge wa jimbo la Lindi mjini pekee ambae hakupendelewa katika ubunge wake bali alishindwa kihalali kwa kuchaguliwa na wananchi wake..nafikiri tushirikiane kuhakikisha katiba hii iliyopendekezwa inapita ili tuungane pamoja katika kujenga nchi yetu “
Katika salam za walemavu waziri wa Afya na ustawi wa jamii Dkt Seil S. Rashid zilizotolewa kwa niaba yake na mwenyekiti wa baraza la watu wenye ulemavu nchini na Dunford Makala alisema kuwa wizara inaendelea kuimarisha ushirikiano na vyama vya watu wenye ulemavu na shirikiasho la vyama vya watu wenye ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) katika kuhakikisha utekelezaji wa uwekaji wa fursa na haki sawa kwa watu wenye ulemavu nchini .
Alisema katika kuhakikisha ushirikiano unakuwepo wizara yake imezindua baraza la ushauri la Taifa la watu wenye ulemavu toka mnamo 1 Novemba 2014 na katika hilo kamwe hawataacha kumpongeza Rais Dkt Jakaya Kikwete kwa kumteua mwenyekiti wa baraza hilo
Aidha alisema kuwa ni ukweli usiopingika kuwa nchi hii chini ya Rais Dkt Kikwete imefanya mambo mengi zaidi ya kuwajali watu wenye ulemavu katika Nyanja za kiuchumi ,kiutamaduni na kisiasa ambavyo vyote hivyo kumwezesha mlemavu kujikwamua kimaisha
Hata hivyo alisema ushahidi wa yote hayo ni pamoja na kuridhia mikataba ya kimataifa juu ya haki za watu wenye ulemavu , kutungwa kwa sharia Na.9 ya mwaka 2010 ya watu wenye ulemavu na kanuni zake ,kuwashirikisha watu wenye ulemavu katika tume ya mabadiliko ya katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania pamoja na kuteuliwa kwa wajumbe 20 wenye ulemavu katika bunge maalumu la mabadiliko ya katiba la mwaka 2014.
Awali walemavu hao katika risala yao iliyosomwa na makamu mwenyekiti wa SHIVYAWATA Amina Mollel pamoja na kuishukuru serikali kwa jinsi kwa kuendelea kuwa karibu zaidi na watu wenye ulemavu kwa kushiriki shughuli mbali mbali za walemavu ,bado waliweza kuishukuru serikali kwa kuandaa sera ya maendeleo ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2004, kutambuliwa kwa watu wenye ulemavu katika MKUKUTA,kuwezesha kuongezeka kwa idadi ya watu wenye ulemavu wanaopata elimu kuanzia shule za msingi hadi elimu ya juu na mambo mengine mengi ambayo wao kama walemavu wamekuwa wakiona serikali yao ipo pamoja nao.
Sanjari na mema hayo bado waliiomba serikali kuzingatia kuwapatia walemavu mambo muhimu katika maisha ya kila siku ikiwa ni pamoja na kuwa na vyombo vya usafiri rafiki kama magari moshi.vyombo vya usafiri majini ,angani ,miundo mbinu katika majengo na viwanja vya ndege ambavyo vitamwezesha mlemavu pia kuwa huru .
Mkuu wa mkoa wa Iringa Amina Masenza alisema kuwa maadhimisho hayo yaliyofanyika chini ya kauli mbiu isemayo ” Maendeleo endelevu ;Ahadi ya Teknolojia huku mkoa wa Iringa ukiendelea kuwa bega kwa bega na walemavu ikiwa ni pamoja na kufanya kazi karibu na vyama hivyo vya watu wenye ulemavu na kuwa mkoa huo kwa sasa una jumla ya walemavu zaidi ya 179 ,000 na wote serikali imeendelea kuwalinda na kuwa nao pamoja.
|
0 comments:
Post a Comment