Monday, 15 December 2014

Aliye mchapa mtoto wa mwajiri wakeafungwa jela miaka ...........


Jolly Tumuhirwe apatikana na hatia ya kumtesa mtoto mdogo na kufungwa jela miaka 4

Yaya wa Uganda aliyejipata pabaya kwa kumchapa mtoto wa mwajiri wake, amehukumiwa jela miaka minne kwa kosa la kumtesa mtoto.
Kisa cha yaya huyu kilizua hasira miongoni mwa watu wengi katika mitandano ya kijamii pale kanda ya video iliibuka mitandaoni ikimwonyesha yaya huyo akimchapa na kumkanyaga mtoto mwenye mwaka mmoja unusu.
Jolly Tumuhirwe, mwenye umri wa miaka 22, alinaswa kwa kamera ya siri akionekana akimchapa na kumkanyaga mtoto huyo pamoja na kumzaba kofi.
Mnamo siku ya Ijumaa, Jolly alikiri kumshambuilia mtoto akisema alikuwa analipiza kisasi kwani mamake mtoto huyo naye alikuwa amezoea kumchapa.
Hata hivyo mama huyo alikanusha madai ya Jolly ambaye polisi walikuwa wamesema wangemshitaki kwa kosa la jaribio la mauaji ila kiongozi wa mashitaka akasisitiza kuwa ingekuwa vigumu kuthibitisha hilo.
Hakimu mkuu Lillian Buchan aliambia Tumuhirwe kwamba alitenda uhalifu ambao hauna hata kisingizio.
Alisema adhabu aliyompa inamtosha kulingana na makosa yake kwa kumtesa mtoto ambaye hana hatia.
Babake mtoto huyo, Eric Kamanzi alisema aliweka kamera ya siri nyumbani kwake baada ya kuwa na shauku kumhusu mfanyakazi huyo.
Kanda ya video iliyomuonyesha Jolly akimtendea unyama mtoto, ilitoka kwenye kamera ambayo Bwana Kimanzi aliweka nyumbani kwake baada ya kushuku kuwa mtoto wake alikuwa anatendewa unyama na pia baada ya kumapata mtoto wake akiwa na alama za majeruhi mwilini mwake.
Alimshitaki mwanamke huyo kwa polisi na kisha kuisambaza kanda hio kwenye mitandao ya kijamii.
Baada ya hukumu kutolewa,Kamanzi alisema: "sio juu yetu kuamua adhabu anayofaa kupewa Jolly. ''
"tunatumai kuwa hili ni funzo kwa wafanyakazi wengi wa nyumbani kwamba huwezi tu kwenda kwa nyumba ya mtu na kumtesa mtoto na kutarajia kuondoka tu kama ulivyoingia. ''

0 comments: