1 RAMBIRAMBI MSIBA WA MCHEZAJI BONIFACE NJOHOLE
2 YAHYA KUFUNGA SEMINA YA WAAMUZI, MAKAMISHNA
3 VITAMBUSHO KWA WAANDISHI WA MPIRA WA MIGUU
SOMA ZAIDI:
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Januari 13, 2014
MALINZI KUTEMBELEA KITUO CHA ALLIANCE
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), Jamal Malinzi atafanya ziara ya siku moja kutembelea
kituo cha mpira wa miguu wa vijana cha Alliance cha jijini Mwanza.
Lengo la ziara hiyo ni kuangalia jinsi
Alliance inayoendesha shughuli zake ili Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) liweze kushirikiana na kituo hicho kwa karibu.
Rais Malinzi katika ziara hiyo
atakayoifanya keshokutwa (Januari 15 mwaka huu) atafuatana na Mwenyekiti
wa Kamati ya Mpira wa Miguu kwa Vijana, Ayoub Nyenzi na mjumbe wa
Kamati ya Utendaji ya TFF, Ramadhan Nassib.
Alliance inatarajia kufanya mashindano
yatakayoshirikisha vituo vyote vya kuendeleza mpira wa miguu kwa vijana
(academy) wiki ya tatu ya Februari mwaka huu jijini Mwanza.
Mashindano hayo yatashirikisha timu za
umri wa miaka 13, 15 na 17 ambapo Alliance itagharamia malazi, chakula
na usafiri wakati timu hizo zikiwa jijini Mwanza.
RAMBIRAMBI MSIBA WA MCHEZAJI BONIFACE NJOHOLE
Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa zamani wa timu ya
Reli Morogoro, Boniface Njohole kilichotokea jana (Januari 12 mwaka huu)
mkoani Morogoro.
Njohole ambaye alikuwa mjumbe wa Kamati
ya Ufundi na Mashindano ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro
(MRFA) hadi umauti unamkuta anatarajia kuzikwa kesho (Januari 14 mwaka
huu) kijijini kwao Mngeta wilayani Ifakara.
Msiba huu ni mkubwa kwa jamii ya mpira
wa miguu kwani alitoa mchango akiwa mchezaji, kocha na kiongozi kwa
nyakati tofauti, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.
TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu
Njohole, klabu ya Reli na MRFA na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu
katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito. Pia TFF itatoa ubani wa
sh. 200,000 kwa familia ya marehemu kama rambirambi zake.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. Amina
YAHYA KUFUNGA SEMINA YA WAAMUZI, MAKAMISHNA
Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu ya
Tanzania (TPLB) ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Hamad
Yahya atakuwa mgeni rasmi katika ufungaji wa semina ya waamuzi na
makamisha.
Semina hiyo ya siku mbili itafungwa
kesho (Januari 14 mwaka huu) saa 4 asubuhi kwenye ukumbi wa mikutano
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Waamuzi zaidi ya 100 na makamishna 50
wanashiriki katika semina hiyo. Makamishna hao ni baadhi ya wale
wanaosimamia mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza
(FDL).
Kwa upande wa waamuzi ni wale wa daraja la kwanza (class one) ambao ndiyo wanaochezesha mechi za VPL na FDL.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) linatarajia kuandaa semina nyingine baadaye mwaka huu kwa
makamishna wapya wanaotaka kusimamia mechi za VPL na zile za FDL.
VITAMBUSHO KWA WAANDISHI WA MPIRA WA MIGUU
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) linatoa vitambulisho vipya kwa waandishi wa habari za mpira wa
miguu kwa ajili ya kuripoti mechi mbalimbali inayoziandaa na
kuzisimamia.
Kila chombo cha habari kupitia Mhariri
wake au Mhariri wa Michezo kinatakiwa kuwasilisha majina ya waandishi
wake kwa barua maalumu ya ofisi pamoja na picha (soft copy) kwa ajili ya
vitambulisho hivyo.
Orodha ya majina ya waandishi wakiwemo wapiga picha wanaoombewa vitambulisho hivyo iwekwe kwa umuhimu.
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari na Mawasiliano
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 comments:
Post a Comment