Thursday, 21 November 2013

MWAKYEMBE ASHANGAA RAHCO KUKODISHA ENEO KWA TSH 500,000

 
Waziri wa Uchukuzi,Dk Harrison Mwakyembe. Picha na Maktaba. 

Ni eneo la Shesheni ya Shirika la zamani la Reli Tanzania (RTC) jijini Arusha, ambalo sasa limekodishwa kwa mwekezaji binafsi
Arusha. 

Waziri wa Uchukuzi,Dk Harrison Mwakyembe, ameelezea kushtushwa na uamuzi wa Kampuni Hodhi ya Mali za  Shirika la zamani la Reli Tanzania (Rahco), kukodisha  kwa mwekezaji, eneo la Stesheni ya Arusha kwa Sh500,000 kwa mwezi.
 Akizungumzia na watendaji wa Rahco na mwekezaji, aliyekodishwa eneo hilo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Monaban , Phillemon Mollel, Dk Mwakyembe alisema kwa mtu yeyote mwenye akili timamu haingii  akilini mtu kukodishwa eneo kubwa kiasi hicho kwa Sh500,000 kwa mwezi katika Jiji la Arusha.
 Mollel pia amekodishwa kinu cha Shirika la zamani la Usagishaji la Taifa (NMC) jijini hapa.
“Ndio sababu kuna maneno maneno, hapa lakini pia huyu mliyemkodisha anajenga ukuta unaogharimu kiasi cha Sh 500 milioni kuzunguka eneo hili na mnasema mkataba wake ni wa miaka miwili, kweli hapa tukitaka hili eneo litatoka au ndio tutafikishana mahakamani,” alisema Dk Mwakyembe.
 Waziri huyo,  aliagiza kusitishwa kuendelea kujengwa kwa ukuta katika eneo la kuzunguka stesheni ya Arusha hadi hapo, suala hilo litakaposhughulikiwa na ofisi yake.
Hata hivyo, Mollel alisema amekodishwa eneo hilo, kwa ajili ya kuhifadhi magari   yanayofika Kiwanda cha NMC kuchukuwa unga na kupeleka nafaka mbalimbali katika maeneo mengine ndani na nje ya nchi.
 “Mheshimiwa mkataba upo wazi, mimi   sintakuwa na kuzuizi kwa Serikali kama ikitaka eneo hili, nilikuwa najenga ukuta ili niweze kununua vichwa viwili vya treni ya mizigo  ili viweze kuniletea ngano kutoka Tanga,” alisema Monoban.

Alisema tayari ana mkataba wa  benki wa kupewa mkopo wa Dola 10,000 za Marekani kwa ajili ya ununuzi wa vichwa vya treni na mabehewa kutoka Afrika Kusini.

\Mapema Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, alimuomba Waziri Mwakyembe, kufuatilia kwa makini mkataba huo, kwa madai kuwa kuna ‘dili’ imechezwa.
Alisema haiwezekani mtu apewe mkataba wa miaka miwili, halafu  ajenge ukuta wa Sh 500 milioni.
“Kuna utata kwa kuwa hata Jiji la Arusha, halikutoa kibali kwa kufuata taratibu na tayari tumewahoji wahusika akiwapo mwekezaji” alisema Lema.

 Na Mussa Juma, Mwananchi GAZETI

0 comments: