Thursday, 28 November 2013

WAKILI ATAFUTWA NA POLISI BAADA YA KUMTUSI BALOZI KWENYE MITANDAO

Picture
(image: blogs.emich.edu)
POLISI Jumatano waliagizwa kumkamata wakili Douglas Mango kwa kukosa kufika mahakamani ili kesi ya kuandika jumbe za kuudhi katika anwani zake za Twitter ianze kusikilizwa.

Hakimu Mkuu Mwandamizi Bi Juma Osoro alitoa kibali cha kumkamata Bw Mango aliyeshtakiwa kwa kuandika jumbe akimchafulia jina balozi wa Kenya nchini Somalia, Bi Yvonne Khamati.

Wakili wa serikali Bw Elizaphus Ombati aliomba kesi iahirishwe kwa sababu Bw Mango hakufika mahakamani. “Naomba pia 
kibali cha kumkamata mshtakiwa kwa kukosa kufika mahakamani,” akasema Bw Ombati.

Bi Osoro alitoa kibali hicho na kuagiza polisi wamfikishwe wakili huyo mahakamani Disemba 11 mwaka huu kesi itakapotajwa.

Hii ilikuwa mara ya pili kwa Bi Osoro kutoa kibali cha kumkamata Bw Mango kwa kukataa  kufika mahakamani.

Mnamo Agosti 28, aliagiza wakili huyo akamatwe na kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kukiuka kanuni za Tume ya Mawasiliano ya Kenya.

Katika kesi hiyo, inadaiwa kwamba siku tofauti kati ya Agosti 14 na 20 mwaka huu, katika eneo lisilojulikana nchini Kenya, Bw Mango aliandika jumbe katika anwani zake ya Twitter na Facebook akijua kwamba madai aliyotoa dhidi ya Bi Khamati yalikuwa ya uongo.

Kulingana na shtaka mshukiwa alinuia kumfadhaisha Bi Khamati na kumuudhi bila sababu yoyote kwa kuandika jumbe hizo.

Katika jumbe hizo, Bw Mango aliye wakili wa mahakama kuu anadai kwamba Bi Khamati amekuwa akihusika na vitendo visivyo vya heshima ili kujipendekeza kwa wanasiasa. Katika jumbe hizo 20, Bw Mango ametoa madai mbalimbali dhidi ya Bi Khamati.

Kesi hiyo ilikuwa ianze kukikilizwa Septemba 20, ambapo Bi Khamati alikuwa mahakamani lakini ikaahirishwa Bw Mango alipodai hakuwa tayari kuendelea na kesi kwa kukosa taarifa za mashahidi na ndipo ikatengwa kusikilizwa Jumatano.

via SwahiliHub

 

0 comments: