Saturday, 23 November 2013

UHUSIANO WA TANZANIA NA MALAWI BADO MGUMU


Rais wa Malawi, Joyce Banda

Uhusiano kati ya Tanzania na Malawi umezidi kuingia katika wakati mgumu baada ya kufahamika kuwa Rais Joyce Banda anatumia vyombo vya habari vya nchi yake kutangaza wananchi wa ukanda wa Ziwa Nyasa ni mali yake.

Pia ameondoa meli ya nchi hiyo ya MV Illala iliyokuwa ikitoa huduma ya kusafirisha wananchi wa Wilaya ya Nyasa na maeneo mengine katika ukanda wa ziwa hilo.

Akizungumza jana, Mbunge wa Mbinga Magharibi, John Komba (CCM), alisema kuwa Banda amekuwa mkorofi kutokana na mambo anayofanya.

Akifafanua zaidi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mbambabay mbele ya Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana, alisema imefika hatua Banda anapotosha ukweli wa mpaka kati ya nchi hizo mbili.


Alisema kuwa Wilaya ya Nyasa wanasikiliza zaidi redio za Malawi, hivyo anapoamua kuupotosha umma kuwa wananchi wa Ukanda wa Ziwa Nyasa ni mali yake baadhi ya wananchi wanaamini, kitu ambacho si kizuri.


“Banda anatangaza kupitia vyombo vyake vya habari ambavyo husikika zaidi huku kwetu kutokana na Wilaya ya Nyasa kutokuwa na mawasiliano ya redio na televisheni za nchini kwetu.


“Wanakosa hata kusikiliza hotuba za viongozi wetu. Huku hawasikii hotuba ya Rais Kikwete wala Waziri Mkuu. Hivyo Banda anatumia nafasi hiyo kutangaza kuwa tuko kwake na uongozi wote wa wilaya na mkoa ni mali yake,” alisisitiza Komba.


Aliongeza kuwa waliokuwa kwenye mkutano huo wa hadhara ukiondoa Kinana waliobaki wote hadi Dk.Asha Rose Migiro ni mali ya Banda.


Rais Banda mbali ya kutumia vituo vyao vya redio, pia ameamua kuondoa meli yake ya Mv Ilala iliyokuwa ikisafirisha wananchi wa maeneo hayo ya ukanda wa Ziwa Nyasa.


“Banda alikuwa na meli yake katika Ziwa Nyasa ambayo ilikuwa inatoa huduma ya usafiri katika ukanda huu, ilikuwa inatusaidia sana lakini sasa ameamua kuiondoa, hivyo tunaomba ahadi ya Rais Jakaya Kikwete ya kuleta meli itekelezwe ili kuwepo uhakika wa usafiri kwa wananchi hao,” alisisitiza.


Alisema kukosekana kwa huduma hiyo, baadhi ya wananchi wa wilaya ya Nyasa wanalazimika kwenda Malawi kutafuta matibabu, jambo ambalo linapaswa kutazamwa kwa aina yake kwa kujengwa hospitali kubwa ya wilaya.


Hata hivyo, Kinana alisema ahadi ya meli ya Rais hiyo ana uhakika itakelezwa na kufafanua kuwa meli tatu zinatengenezwa Korea Kusini na zitakapokamilika ya Ziwa Nyasa itapelekwa.


Mgogoro kati ya Tanzania na Malawi umetetereka baada ya Rais Banda kudai kuwa mipaka ya nchi yake inaishia ufukweni mwa Ziwa Nyasa , madai ambayo yamepingwa na Serikali. 
SOURCE:NIPASHE
23rd November 2013

0 comments: