Monday, 25 November 2013

MFANYABIASHARA MAARUFU MKOANI TABORA AJIPIGA RISASI KWA WIVU WA MAPENZI


MFANYABIASHARA maarufu mjini Tabora, Hakimu Hamdun, mkazi wa Kata ya Kanyenye anashikiliwa Polisi akituhumiwa kujaribu kujiua kwa kujipiga risasi kutokana na wivu wa mapenzi.

Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Kamishna Msaidizi, Peter Ouma, alisema jana kuwa Hamdun alijaribu kujiua kwa risasi wiki iliyopita saa kumi na mbili jioni nyumbani kwake eneo la Kanyenye mjini hapa.

Alisema kuwa Hamdun ambaye kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Mkoa Kitete kwa matibabu, alijipiga risasi baada ya
 mkewe aliyempa talaka mbili, kumtaka afuate utaratibu wa ndoa ili warudiane.

Inadaiwa Hamdun alimpa talaka mbili mkewe huyo, Joha binti Sudi, lakini baadaye alibadilisha mawazo na kumtaka warudiane huku akimtishia kumuua kama asipokubali.

Kwa mujibu wa madai ya Kamanda Ouma, wanandoa hao waliotalikiana walikuwa wanaishi nyumba tofauti na Hamdun aliamua kumfuata mkewe alipokuwa akiishi akiwa na gari lake na kumtaka warudiane. Hata hivyo, alidai mkewe huyo alikataa kurudiana kienyeji na kumtaka Hamdun kama kweli anampenda, afuate utaratibu wa Dini ya Kiislamu ndipo watimize azma yao hiyo ya kurudiana.

Utaratibu Utaratibu huo kwa mujibu wa dini ya Kiislamu, talaka moja na mbili zinaitwa talaka rejea, ambapo mume aliyotoa talaka hizo, anapaswa kumpa chumba mkewe pale pale nyumbani wanakoishi na chakula kwa miezi mitatu (eda). Ndani ya hiyo miezi mitatu, ikiwa watataka kurudiana, mume huyo ataruhusiwa kwenda katika chumba cha mkewe na kumtaja kwa jina lake na kutamka nimeamua kukurejea. Kwa taratibu za imani ya Kiislamu, mke hatakiwi kukataa na hilo linapofanyika halihitaji shahidi wala shehe. Ikiwa mke atapewa talaka tatu, atakaa eda akila na kuhudumiwa kila kitu mpaka miezi mitatu iishe, ambapo mwanamke atasafiri kurudi kwao. Kama mume atataka kumrejea, mke huyo atapaswa kuolewa kwanza, aachike ndipo utaratibu wa kufunga naye ndoa uanze.

Badala ya kufuata utaratibu, inadaiwa Hamdun alienda kwenye gari lake na kuchukua bunduki aina ya Shot gun na kwenda nyumbani kwake ambapo alifunga milango, akajipiga risasi katika ubavu wa kushoto.

Kwa mujibu wa Kamada Ouma, mtuhumiwa huyo hali yake inaendelea vizuri lakini amepoteza sifa ya kumiliki bunduki na hivyo hatapewa tena.

Aidha, Hamdun atakapomaliza matibabu atafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yake ikiwemo ya kutishia kuua na jaribio la kutaka kujiua. 
CHANZO  HabariLeo

 

0 comments: