Saturday, 23 November 2013

TANZANIA BARA NA ZANZIBAR KUWA NA VIWANGO VIPYA VYA ELIMU


Dk. Shukuru Kawabwa, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi wa Tanzania

Wizara ya Elimu na Ufundi na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali zimekubaliana kuandaa viwango vipya vya mitihani wa kidato cha nne utakaoanza kutekelezwa mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari visiwani hapa, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi wa Tanzania, Dk. Shukuru Kawabwa, alisema mfumo huo wa viwango vya ufaulu wa mitihani hautokuwa tofauti bali hakutokuwa na kiwango cha daraja sifuri na badala yake kutakuwa na division sifuri.


“Hakuna utofauti wowote ni sawa sawa na mtu kuitwa Juma na badala yake kujibadili jina na kujiita Ali hivyo ni sawasawa na division zero kuitwa division sifuri,” alisema Dk Shukuru.


Alisema tayari wameshakubaliana baina ya wizara yake na wizara ya elimu ya Zanzibar ambapo leo alikuwa na mazungumzo na waziri Ali Juma Shamuhuna kwa ajili ya kufikia muafaka na tayari wameshakubaliana na mfumo huo.


Alisema maksi zitakazo tumika kwa kiwango cha division sifuri ni maksi 48 hadi 49 na hakutakuwa na division 5 kama walivyopanga awali.


Kuhusu somo la dini na Kiarabu alisema halijaondoshwa lipo kama kawaida hivyo wanafunzi kutokuwa na hofu yoyote kuhusiana na masomo hayo.

“Somo la dini na Kiarabu litatumika kama linavyotumika awali wala halijaondolewa au kuwekwa masomo ya hiyari,” alifahamisha waziri huyo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Abdallah Juma Abdallah, alisema asilimia 98 ya wanafunzi wa Zanzibar wanafanya mtihani wa somo la dini na amefurahishwa na uamuzi waliofikiana baina ya Dk. Shukuru Kawabwa na Waziri Ali Juma Shamuhuna ya kuwa somo la dini na Kiarabu litaendelea kuwa la lazima.


Alisema serikali inamkakati wa kuboresha sekta ya elimu na kuajiri walimu wapya wa Sayansi katika shule za sekondari na kuboresha maslahi ya walimu kwa manufaa ya Taifa.  
SOURCE: NIPASHE

23rd November 2013

0 comments: