Thursday, 21 November 2013

TAARIFA YA HOSPITALI YA MUHIMBILI KUHUSU HABARI YA GAZETI LA RAI KUMHUSU DK MVUNGI

Awali ya yote Hospitali ya Taifa Muhimbili inapenda kutoa salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki wa Dkt. Sengondo Mvungi aliyefariki katika Hospitali ya Millpark, Johanesburg nchini Afrika Kusini.  Mwenyezi Mungu aiweke mahali pema peponi, roho ya marehemu Dkt. Sengondo Mvungi, Amina.

Katika gazeti la Rai Nguvu ya Hoja Toleo Na. 1092 la Jumatano Novemba 20, 2013 lilichapisha habari ukurasa wa tatu ikisomeka “Maisha ya Dkt. Mvungi yangewezwa kuokolewa”

Gazeti hilo lilidai kwamba baada ya marehemu Dkt. Mvungi kufikishwa Hospitali ya Taifa Muhimbili ilichukua zaidi ya saa sita 
kabla ya kupatiwa  huduma ya dharura aliyokuwa akihitaji na kwamba ni jambo la kawaida katika Hospitali hii ya Taifa.

Tunapenda kuwafahamisha umma wa Tanzania kuwa Idara ya  Huduma za Dharura ya Hospitali ya Taifa (EMD) imeimarika sana na huchukua takribani kati ya dakika 30-45 tu kwa  mgonjwa wa ajali kuhudumiwa na kupelekwa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa matibabu zaidi. Na hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Marehemu Dr. Sengondo Mvungi.

Tunaomba radhi kwa huduma ya kwanza ya CT Scan kutofanyika Hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na tatizo lililosababishwa na mawasiliano. Hata hivyo, huduma ya CT Scan ya mara ya pili ilifanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na ilisaidia kwa kiwango kikubwa katika kuimarisha tiba aliyokuwa anapatiwa na madaktari wa MOI.

Tunaendelea kusisitiza kuwa uandishi wa habari za afya unahitaji kuzingatia maadili ya sekta ya afya ili kutosababisha usumbufu usio wa lazima kwa wananchi.

Ni matumaini yetu kuwa Waandishi wa Habari watazingatia maadili ya kazi zao kama tunavyoshauri mara kwa mara katika matoleo yanayohusu Hospitali ya Taifa Muhimbili.


Imetolewa na;

Ofisi ya Uhusiano
Hospitali ya Taifa Muhimbili
Novemba 21, 2013

 

0 comments: