Friday, 15 November 2013

HOSPITALI YA MUHIMBILI YAKOSA MAJI KWA WIKI MOJA

 

Dar es Salaam. 

Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, haina huduma za maji kwa wiki moja sasa, jambo linalowalazimisha ndugu wa wagonjwa kuingia wodini wakiwa na vidumu vya maji.

Tatizo hilo limekuja baada ya Mamlaka ya Majisafi na Majitaka jijini Dar es Salaam (Dawasco ), kusitisha huduma hizo ili kuruhusu uunganishaji wa mtambo mpya wa maji katika hospitali hiyo. Mwandishi wa habari hii, jana alishuhudia ndugu wa wagonjwa waliolazwa katika hospitali hiyo kubwa nchini, wakiwa na madumu ya maji wakiwapelekea wagonjwa wao.

Kwa upande wao, baadhi ya wagonjwa walisema maji yalikatwa Novemba 7 mwaka huu na kwamba hatua hiyo imesababisha mazingira kuwa machafu na hasa vyooni, jambo linalohatarisha maisha yao.
Mmoja wa wagonjwa hao, Subira Ahmed, alisema tatizo hilo ni kubwa na kwamba linawalazimisha ndugu kubebewa maji kutoka nyumbani.

Alisema hata hivyo maji wanayoletewa na ndugu hayatoshelezi mahitaji.
“Sijaoga na leo (jana) nina siku ya tatu na hii inatokana na ukweli kwamba maji tunayotumia tunanunua maana sisi ni wageni kutoka Tabora”alisema Subira

Mgonjwa Lemeck Isaya, alisema vyoo wanavyotumia viko katika hali mbaya kutokana na kukosa maji. Aliishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kuchimba visima virefu katika hospitali hiyo ili kumaliza kero ya maji.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa hospitali hiyo, Aminiel Aligaesha, alisema walitangaziwa kuwa Dawasco itakata huduma za maji.

Alisema hata hivyo maji kidogo yanapatikana kutoka katika kisima kilichopo katika hospitali hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Dawasco, Jackson Midala alisema maji yalikatwa Novemba 9 mwaka huu kwa sababu walikuwa wanatengeneza mtambo mpya wa maji.

Chanzo Na Pamela Chilongola, Mwananchi gazeti
Posted  Ijumaa,Novemba15  2013

0 comments: