Friday, 15 November 2013
HOME »
» MAWAZIRI EAC SASA KUJADILI KENYA,UGANDA NA RWANDA
MAWAZIRI EAC SASA KUJADILI KENYA,UGANDA NA RWANDA
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, Dk Emmanuel Nchimbi.PICHA|MAKTABA
Bujumbura.
Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki,linatarajiwa kukutana Kampala,Uganda mwishoni mwa mwezi huu kujadili suala la Kenya,Uganda na Rwanda kufanya vikao bila kushirikisha nchi zingine.
Kikao hicho pia kitahitimisha vikao kadhaa vya kutafuta mwafaka wa masuala mengi yaliyoibua mivutano kati ya viongozi ndani ya EAC likiwamo mvutano kati ya Rwanda na Tanzania.
Akichangia mada katika mkutano wa pili wa amani na usalama ndani ya jumuia hiyo, unaoendelea mjini Bujumbura jana,Naibu Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya EAC, Charles Njoroge alisema kikao hicho ni mfululizo wa juhudi za kumaliza sintofahamu iliyoibuka kuhusu suala hilo.
“Ingawa mkataba wa EAC unaruhusu nchi moja,mbili au zaidi kukutana,kujadili na kutekeleza miradi ya maendeleo yaliyoko kwenye mipango ya EAC kwa namna wanavyoona inafaa,ni busara kulitafutia ufumbuzi suala hili kupitia majadiliano,”alisema Njoroge
Kuhusu uhusiano kati ya Tanzania na Rwanda, Naibu Katibu Mkuu huyo alisema, hali ni shwari na kurejea kauli na picha za wakuu wa nchi hizo walipokutana nchini Uganda.
Nchi za Kenya,Uganda na Rwanda zimefanya vikao kadhaa kujadili na kufikia uamuzi bila kuzishirikisha Tanzania na Burundi, hali
iliyozua mjadala mkubwa kiasi cha kuibua hofu ya uwezekano wa Jumuiya hiyo kuyumba katika malengo yake ya ushirikiano.
Awali,mmoja wa watoa mada katika mkutano huo, Peter Edopu kutoka Uganda alisema,kuna umuhimu wa suala hilo kujadiliwa baada ya baadhi ya nchi kuhisi kutengwa katika mazungumzo na maamuzi ya kutekeleza baadhi ya miradi iliyo katika mipango na ratiba ya EAC.
Alisema kuacha kujadili suala hilo kunaweza kuathiri ushirikiano miongoni mwa nchi wanachama wa EAC baada ya mjadala huo kuanza kushirikisha wananchi ambao wanaonekana kuchukua mkondo wa kuunga msimamo wa viongozi wa nchi zao.
Akizungumza nje ya ukumbi wa mikutano, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, Dk Emmanuel Nchimbi anayehudhuria mkutano huo alisema malalamiko ya Tanzania na Burundi kuhusu kutengwa na Kenya,Uganda na Rwanda ni ishara ya upendo na moyo wa ushirikiano wa dhati ndani ya EAC.
“Ukiona rafiki anamlalamikia rafiki yake kumtenga katika jambo lolote ni ishara kuwa anapenda urafiki huo uendelee. Huo ndiyo msimamo wetu katika suala hili kwamba tunajiuliza kwanini wenzetu wasitushirikishe?”alisema Nchimbi
Wakati huo huo, EAC inakusudia kuunda Baraza la Usalama la Ukanda huo iwapo baraza la mawaziri na wakuu wa nchi hizo watapitisha mapendekezo na mchakato utakaowasilishwa na Sekretarieti ya EAC kuhusu jambo hilo.
CHANZO Na Peter Saramba na
Rosemary Mirondo,Mwananchi
0 comments:
Post a Comment