Tuesday, 19 November 2013

WALIMU WAACHA KUFUNDISHS WAKIKWEPA VIBOKO KAMA SHINIKIZO KUCHANGIA SHULE YA KATA

WALIMU wa Shule ya Msingi Iponyanholo, iliyopo Kata ya Sabasabini, wilayani Kahama, wamedai kutohudhuria vipindi vya masomo na kukimbilia mlimani ili kukwepa viboko vya sungusungu wanaosaka mchango wa ujenzi wa shule ya sekondari ya kata hiyo.

Hayo yalibainishwa juzi na Mwalimu Clement Ntarano  kwenye kikao cha Kamati ya Maendeleo ya kata hiyo na viongozi wa 
Chama Cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya kata na wilaya akiwemo Katibu wa Fedha na Uchumi wa chama hicho wilaya, Isaya Bukakiye.

Akizungumza kwa niaba ya walimu wenzake, mwalimu huyo alidai tabia hiyo ni ya kuwadhalilisha mbele ya wanafunzi wao huku tuhuma kubwa wakizielekeza kwa Diwani wa kata hiyo, Emmanuel Makashi, kuhusika kuwaagiza sungusungu hao kuwafanyia vitendo hivyo.

Hata hivyo, Diwani Makashi alisema tatizo la walimu hao kukimbia shule si la viongozi wa serikali ya kata hiyo bali ni amri ya mahakama ya kutaka wakamatwe baada ya kukaidi wito wa kwenda mahakamani.

Awali, Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Elias Mpigamanoni, aliwaambia wajumbe wa kikao hicho kuwa alichukua jukumu la kuwapeleka walimu hao mahakamani baada ya kugoma kuchanga, lakini walipopewa hati ya wito waliandika maneno ya kashfa ndipo ilipotoka hati nyingine ya kuwakamata.

Hata hivyo baada ya kutolewa hati hiyo, walimu hao walikimbia shuleni na kuwatuhumu viongozi wa kata kwamba wamewatumia walinzi wa jadi sungusungu kuwachapa viboko mbele ya wanafunzi wao wakati waliofika shuleni walikuwa ni mgambo wa Mahakama ya Mwanzo Mpunze.

Kutokana na hali hiyo, Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM Wilaya ya Kahama, Bukakiye, alisema  suala hilo haliwezi kuamriwa na chama isipokuwa atalifikisha kwa viongozi wa serikali ngazi ya wilaya akiwamo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ushetu ndiye mwenye uamuzi wa suala hilo.

Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Sabasabini ilikaa na kupitisha maazimio ya kila kaya kuchangia sh 10,000 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari ambapo walimu wa shule hiyo wapatao tisa waligoma kuchangia.

--- via Tanzania Daima

 

0 comments: