Tuesday, 19 November 2013

GARI AINA YA NOAH YAUA WATU SABA,NA YAJERUHI SABA

  Wengine watatu wafa Dodoma
Watu saba waliokuwa wakisafiri kwa gari ya kubeba abiria aina ya Noah, wamefariki dunia baada ya kugongana uso kwa uso na lori aina ya Scania eneo la Wami Ranchi wilayani Mvomero Barabara kuu ya Morogoro- Dodoma huku wengine saba wakilazwa baada kujeruhiwa vibaya.

Watu 10 wamefariki dunia na wengine 20 kujeruhiwa katika ajali za barabarani zilizotokea jana katika mikoa ya Morogoro na Dodoma.

Katika tukio la kwanza, watu saba waliokuwa wakisafiri kwa gari ya kubeba abiria aina ya Noah, wamefariki dunia baada ya kugongana uso kwa uso na lori aina ya Scania  eneo la Wami Ranchi  wilayani Mvomero Barabara kuu ya Morogoro- Dodoma huku wengine saba wakilazwa baada kujeruhiwa vibaya.


Ajali hiyo ilitokea alfajiri, baada ya Noah yenye namba za usajili T 502 AUB ikitokea wilayani Gairo kuelekea Morogoro iliyokuwa ikiendeshwa na Masudi Omari ambaye pia alifariki eneo la ajali, iligongana na Scania namba T 129 AJB.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Fustine Shilogile, alithitibisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa chanzo ni mwendo kasi wa dereva wa Noah ambaye alitaka kulipita gari la mbele yake, lakini kabla hajalipita aligongana na lori hilo lilokuwa likitokea Morogoro kuelekea Dodoma.


Shilogile alisema Noah ilikuwa imebeba abiria ikitokea Gairo kuelekea Morogoro mjini na dereva wake alikuwa katika mwendokasi kwa nia ya kuwahisha abiria katika stendi kuu ya mkoa wa Morogoro.


Alisema watu saba walifariki eneo la tukio kati yao sita ni wanaume akiwemo na dereva Noah na mmoja ni mwanamke.

Majeruhi walikimbizwa katika  Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huku hali zao zikiwa mbaya.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Shilogile, miili ya watu sita imetambuliwa akiwamo dereva wa gari ndogo aliyetambuliwa kwa jina la Masudi Omary.


Wengine ni Isack Mehele (25), mfanyakazi wa kiwanda cha Tumbaku cha Allance One; mkazi wa Manispaa ya Morogoro, Sam Elisha (40),

ambaye ni daktari wa mimea na Maugo Salum (30), Sophia Hassan (20), Adini Mwisholwa (70) ambao wote wakazi wa Gairo, na mwanaume mmoja ambaye jina lake halijafahamika

Waliojeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya mkoa wa Morogoro wodi namba  moja ni pamoja na Juma Mohamed (21), mkazi wa Gairo;  Hashim Ally Dafa, (42) mkazi wa Lushoto; Junior Msenga; Selemani Hamis (20), mkazi wa Babati mkoani Manyara; Martin Msobi, mkazi wa Dumila; Festo Paulo, mkazi wa Kimara mwisho jijini Dar es Salaam na mwimgine mmoja ambaye jina lake halikutambuliwa mara moja kutokana na hali yake kuwa mbaya.


Naye Daktari Bingwa wa Upauaji wa  Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Dk Francis  Semwene, alithibitisha kupokea majeruhi saba ambao walikuwa wamejeruhiwa katika sehemu mbalimbali na kusema kuwa kati ya hao wawili halizao zilikuwa ni mbaya sana na madaktari walikuwa wakifanya jitihada za kuokoa maisha yao.

Katika tukio lingine, watu watatu wamefariki dunia na wengine 13 kujeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea kwenye kijiji cha Gulwe wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma, baada ya lori la mizigo aina ya Mistubishi Fuso kuacha njia na kupinduka kisha kuparamia kingo za daraja kabla ya kutumbukia kwenye korongo.


Mashuhuda walisema ajali hiyo ilitokea jana saa 12:00 asubuhi na kulihusisha gari namba T 469 AKS, lililokuwa limesheheni mizigo na watu likiwa linaelekea mnadani  katika Tarafa ya Kibakwe.


Waliofariki katika ajali  hiyo, ni Idd Mbelwa, Burhani Mzuza na mtu mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Bakari.


Fabian Boke, alisema gari hilo lilipofika katika mteremko lilimshinda dereva aliyefahamika kwa jina la Kapama Mohamed kisha kuparamia kingo za daraja kabla ya kutumbukia katika korongoro.


Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa, Dk. Mohamed Pathan, alisema hospitali yake ilipokea miili ya watu watatu na majeruhi 13.


Alisema majeruhi wawili walihamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kutokana na hali zao kuwa mbaya.


Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Suzan Kaganda, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo.


Imeandikwa na Ashton Balaigwa, Idda Mushi, Morogoro na Jacqueline Massano, Dodoma.

 
SOURCE: NIPASHE
19th November 2013

0 comments: