Naibu Waziri wa Fedha,Saada Mkuya Salum
Washirika wa maendeleo wanaochangia bajeti ya serikali wameeleza kutoridhishwa na matokeo mabaya ya shule za msingi na sekondari, vita dhidi ya rushwa hasa kwenye sekta za afya, bandari na nishati; na kasi ya kupunguza umasikini nchini.
Wameitaka serikali kuelekeza rasilimali zaidi kwenye sekta za elimu, afya, maji, nishati na vita dhidi ya rushwa na kutekeleza mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Hayo yalielezwa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Washirika wa Maendeleo ambao wamekuwa wakichangia bajeti ya serikali, Balozi Lennarth Hjelmaker, kwenye mkutano wa mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya serikali.
Balozi Hjelmaker ambaye anaiwakilisha Sweden nchini, alisema Tanzania imefanya vizuri kwenye baadhi ya maeneo kama afya, miundombinu na maji kwa kuelekeza bajeti za maendeleo kwenye maeneo muhimu lakini sekta hizo zinakabiliwa na changamoto kubwa.
Alisema taarifa zinaonyesha kuwa hali ya upatikanaji wa maji safi na salama hasa vijijini ni tabu, kiwango cha ufaulu kimeshuka kwa shule za msingi na sekondari na upatikanaji wa umeme hasa vijijini umeendelea kusuasua.
“Tathmini pia inaonyesha kwamba mapambano dhidi ya rushwa yanahitajika zaidi...inaonekana kwamba bado hatua za kinidhamu na kiutawala hazichukuliwi hasa kwa makosa madogo madogo ya rushwa,” alisema.
Kadhalika, wameitaka serikali kutekeleza ufuatiliaji na utekelezaji wa mapendekezo ya CAG ili fedha zinazoelekezwa kwenye miradi ya maendeleo ziweze kuleta matokeo yanayokusudiwa.
“Tunaihimiza serikali kutekeleza kwa vitendo eneo hili na kufanya mazungumzo ya mara kwa mara ya ngazi ya juu kuhusu vita dhidi ya rushwa,” alisema.
Alisema wafadhili wameridhishwa na ongezeko la makusanyo ya kodi jambo ambalo litapunguza utegemezi wa bajeti kutoka kwa wahisani.
Awali, Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, alisema pamoja na kwamba serikali imefanikiwa kujenga shule, zahanati, miundombinu na kukuza uchumi, bado sekta hizo zinakabiliwa na changamoto nyingi hasa ukuaji wa uchumi usiolingana na kasi ya kupunguza umasikini.
“Uchumi wetu unakua kwa asilimia saba, lakini kasi ya kupunguza umaskini ni asilimia mbili na wakati huo huo, rasilimali haziongezeki lakini watu wanaongezeka, hii ni changamoto kubwa na serikali inaifanyia kazi,” alisema.
Alisema mkakati wa matokeo makubwa sasa umetilia mkazo sekta hizo ili kufikia mpango wa maendeleo wa miaka mitano.
SOURCE:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment