Dar es Salaam. Familia ya
Waingereza, Kirstie Trup na Katie Gee, wote wenye umri wa miaka 18,
waliomwagiwa tindikali huko Zanzibar, wameiomba Serikali ya Uingereza
kuishinikiza Tanzania kuharakisha kuwawajibisha waliohusika na tukio
hilo.
Waingereza hao ambao walikuwa walimu wa kujitolea katika shule ya St Monica, Tomondo, Zanzibar, walimwagiwa tindikali na watu wawili wasiojulikana wakati walipokuwa kwenye matembezi ya jioni katika eneo la Mji Mkongwe Agosti 7, mwaka huu.
Baada ya tukio hilo lililowajeruhi kiasi kikubwa katika maeneo ya kifua na mikononi, walipewa matibabu katika hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam, kisha wakarudishwa kwao kwa matibabu zaidi.
Alipowatembea wasichana hao hospitalini, Rais Jakaya Kikwete alisema tukio hilo limetia aibu kwa mataifa ya nje na kuliamuru Jeshi la Polisi kuhakikisha linawakamata na kuwafungulia mashtaka wote waliohusika.
Taarifa iliyosambazwa kwenye mtandao wa habari wa
Polisi wa Kimataifa (Interpol) Kanda ya Tanzania, inaeleza kuwa familia
ya wasichana hao hairidhishwi na namna Serikali ya Tanzania
inavyolishughulikia suala hilo kwa kuwa hadi sasa imeshindwa kuwatambua
wahusika.
Mtandao huo umemnukuu baba yake Trup, Marc
alipokuwa akizungumza na Redio 4 ya BBC, kuwa kuna wingu zito
lililotanda kuhusu kesi hiyo, kwa kuwa hadi sasa Serikali ya Zanzibar
imeshindwa kuonyesha picha za wahusika ili zitambuliwe na wasichana hao,
ingawa imekwisha kuwahoji watu kadhaa.
“Picha haziwezi kutumwa katika muundo bora
unaokubaliwa na Interpol au Mamlaka za Uingereza, kutokana na sababu
hizo hakuna hata mmoja ameshaziona hizo picha,” alisema Marc.
Naye baba mlezi wa Gee, Doug Morris, alisema:
“Kama Wizara ya Mambo ya Nje na Ofisi ya Jumuiya ya Madola wako makini
kusaidia watu hao kufikishwa mbele ya sheria kwa niaba ya raia wa
Uingereza, tulitegemea wafanye kila linalowezekana, lakini hakuna dalili
zozote zinazoonekana za kutaka kuharakisha jambo hili.”
Aliongeza:“Kama wanamaanisha wanachokisema na ni
muhimu kwao kuwatafuta waliotekeleza kitendo hicho ili wawafikishe
kwenye vyombo vya sheria, basi watusaidie kwa kila njia ambayo wanaweza.
“Kila mtu ameanza kufikiri kuwa wanatuchezea, kila
wiki tunakatishwa tamaa. Huu ni uharibifu ambao hauwezi kupita tu bila
mtu kuadhibiwa kwa manufaa ya wasichana wale au mtu mwingine yeyote.
“Aina gani ya ujumbe unaoletwa, kwamba unaweza kufanya jambo baya halafu usifanywe kitu chochote?”
Alisema kuwa wangependa suala hilo lifike mwisho haraka iwezekanavyo ili haki itendeke.
Chanzo mwananchi
Na Mwandishi Wetu
Chanzo mwananchi
Na Mwandishi Wetu
0 comments:
Post a Comment