Saturday, 23 November 2013

ZAIDI YA WATOTO 137 NA WAKINAMAMA 19 HUFARIKI DUNIA KILA SIKU

Picture
Washiriki wa semina pamoja na wawezeshaji
JUMLA ya watoto 137 na wajawazito 19 hufariki dunia kila siku nchini Tanzania kwa matatizo yanayotokana na uzazi. Vifo vya watoto pekee wanaopoteza maisha kutokana na matatizo hayo kwa mwaka hufikia 50,000 kwa nchi nzima.

Takwimu hizi za kusikitisha zimetolewa leo jijini Dar es Salaam na Meneja Mradi wa mpango wa 'Wajibika Mama Aishi', Bw. David Lyamuya toka Taasisi ya Utepe Mweupe katika semina ya wahariri na waandishi wa habari waandamizi.

Lyamuya alisema mbali na idadi hiyo kubwa ya akinamama pamoja na watoto kupoteza maisha yapo matukio mengine ya 
vifo ambayo hayaingizwi kwenye takwimu, hali inayoonesha huenda vifo hivyo ni zaidi ya takwimu halisi zilizopo.

Alisema kuna kila sababu kwa mamlaka husika kwa kushirikiana na jamii kulivalia njuga suala hilo ili kuhakikisha vifo vya mama na mtoto vinakoma. Aidha alisema licha ya uhimizaji wa wajawazito kuhudhuria klini bado idadi kubwa hasa vijijini wanajifungulia nyumbani kutokana na umbali mrefu wa sehemu zinapotolewa huduma za afya.

"...Sisi tumefanya utafiti katika Mkoa wa Rukwa kuangalia hali ya upatikanaji huduma za afya kwa wajawazito. Yapo maeneo mama aliyefikia hatua ya kujifungua (mwenye uchungu) hutakiwa atembee kilomita 94.5 ndiyo anakutana na kituo cha afya, sasa mtu aliye na hali kama hiyo hawezi kutembea umbali mkubwa kiasi hicho hivyo hulazimika kujifungua nyumbani," alisema Lyamuya.

Aidha aliongeza kuwa taasisi ya Utepe Mweupe (The White Ribbon Alliance) kwa sasa inaendesha kampeni ya miaka mitatu ya "Wajibika Mama Aishi" ikiwa ni moja ya hatua ya kushawishi kila mmoja kuwajibika kuhakikisha anakabiliana na vifo vya akinamama na watoto vinavyotokea hasa wakati wa kujifungua.

Hata hivyo aliwataka wanahabari kuhakikisha wanatumia nafasi zao kutoa mchango wa kuvishavishi vyombo husika na wanajamii kwa ujumla kupambana na vifo vya akinamama na mtoto.

*Taarifa hii imeandaliwa na kushirikishwa kwenu na mtandao wa: TheHabari.com

0 comments: