Mbunge wa Ubungo, John Mnyika
Mbunge wa Ubungo, jijini Dar es Salaam, John Mnyika, amepinga hatua iliyochukuliwa na Rais Kikwete ya kuwapongeza mawaziri wake wanne kwa maamuzi waliyoyachukua ya kujiuzulu nyadhifa zao.
Akilihutubia taifa wiki iliyopita usiku kutoa salamu za mwaka mpya wa 2014, Rais Kikwete, alisema mawaziri hao wameonyesha ukomavu wa kisiasa na kiuongozi wa hali ya juu na moyo wa uzalendo kutokana na hatua yao ya kuachia nyadhifa walizokuwa nazo.
Pia alisema ataunda Tume ya Uchunguzi itakayoongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu na kwamba uchunguzi wa kina utafanywa kuhusu madai yaliyotolewa katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
“Makosa yaliyofanyika yataainishwa na waliofanya kutambuliwa ili wachukuliwe hatua zipasazo kwa mujibu wa sheria na kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma. Ni muhimu kufanya hivi ili haki itendeke ipasavyo,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Mtindo wa mzigo wa makosa ya watumishi wa umma kubebwa na viongozi wa kisiasa pekee, tena wasiokuwa na hatia ya moja kwa moja, siyo sahihi. Lazima kila mtu abebe mzigo wake inavyostahili. Ni matumaini yangu pia kwamba katika siku za usoni kunapotokea matatizo ya namna hii uchunguzi uwe wa kina ili wale hasa waliohusika na kutenda makosa wawajibishwe.”
Akizungumza na NIPESHE, Mnyika, alisema, Rais Kikwete hakupaswa kuwasafisha mawaziri hao, kwani aliyekuwa Waziri wa Maliasili Balozi Hamisi Kagasheki pekee ndiye aliyetangaza kujiuzulu huku wengine wakikataa na kuondoka kimyakimya.
Kwa mujibu wa Mnyika, Kikwete alipaswa kusema wazi kwamba, Kagasheki ndiye aliyetangaza wazi kuachia wadhifa wake na kuwataka mawaziri wengine waliobaki kutakiwa kufanya kama alivyofanya mwenzao.
Kuhusu uchunguzi, Mnyika, alisema, tatizo siyo kuunda tume bali ni kuchukuliwa hatua kwa watumishi wa serikali wanaokiuka maaadili ya utumishi.
SOURCE:
NIPASHE
7th January 2014
0 comments:
Post a Comment