Sunday, 26 January 2014

FABIO DA SLIVA NA WILFRIED ZAHA KWENDA CARDIFF, YOHAN CABAYE KUTUA OLD TRAFFORD??

 
>>KWENYE MALENGO YA MAN UNITED YUPO PIA TONI KROOS!
TONI_KROOSFABIO DA SILVA na Wilfried Zaha wapo mbioni kupelekwa Cardiff City kwa Mkopo wakati Klabu yao Manchester United ikiongeza juhudi za kunasa Kiungo mwenye hadhi ya Kimataifa huku Yohan Cabaye wa Newcastle na Toni Kroos wa Bayern Munich wakitajwa sana huko England kwamba ndio walengwa.
Cardiff City, ikiongozwa na Nguli wa zamani wa Man United, Ole Gunnar Solskjaer, ipo katika hatua za mwisho kuwanasa Vijana wa Man United, Fabio na Zaha, ili wacheze kwa Mkopo hadi mwishoni mwa Msimu.
Zaha, ambae alinunuliwa kutoka Crystal Palace, ameichezea Man United Mechi 4 tu Msimu huu na kwenda kwake Cardiff kutampa nafasi ya kuchezea Timu ya kwanza.
Nae Fabio, ambae Msimu uliopita alikuwa QPR kwa Mkopo, anahitaji pia kucheza mara kwa mara tofauti na Pacha mwenzake, Rafael, ambae hucheza Timu ya Kwanza ya Man United.
Mapacha hao, wenye Miaka 23, walijiunga na Man United Mwaka 2008 wakitokea Klabu ya kwao Brazil, Fluminese.ZAHA-MAN_UNITED
Cardiff, ambao Jumanne watatua Old Trafford kucheza na Man United kwenye Mechi ya Ligi, pia wapo hatua za mwisho kumsaini Kenwyne Jones kutoka Stoke City kwa kubadilishana na Peter Odemwingie ambae atakwenda Stoke.
WAKATI HUO HUO, zipo ripoti kuwa Man United wanatafakari kumnunua Kiungo toka Ufaransa anaechezea Newcastle, Yohan Cabaye, ambae anathaminiwa kuwa na Dau la Pauni Milioni 25.
Lakini Cabaye pia yumo kwenye macho ya Arsenal na Paris Saint-Germain ingawa Klabu hizo zinadaiwa kumtaka kwa Dau hafifu.
PSG inasadikiwa iko tayari kumnunua kwa Pauni Milioni 17 wakati Arsenal wameshawahi kukataliwa Ofa yao ya Pauni Milioni 10.2 waliyotoa mwanzoni mwa Msimu.
Mbali ya Cabaye, Meneja wa Man United, David Moyes, pia anadaiwa kuwa na nia ya kumchukua Kiungo wa Bayern Munich, Toni Kroos, ambae alikwenda kumtazama akicheza wakati Bayern Munich inaifunga Borussia Monchengladbach Bao 2-0 Juzi Ijumaa huku Moyes akinaswa akiongea na Wakala wa Kroos, Sascha Breese.
Hivi sasa Kroos, ambae Mkataba wake na Bayern unamalizika mwishoni mwa Msimu ujao, yupo kwenye mvutano na Klabu yake kuhusu Mkataba mpya na inaaminika anaweza kuihama hivi sasa kwa Dau la kati ya Pauni Milioni 20 hadi 25.

0 comments: