Monday, 6 January 2014

UGONJWA ULIOMUUA WAZIRI WAFEDHA DK WILLIAM MGIMWA WATAJWA

Dk. Servacius Likwelile, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha
Umati wa wakazi wa jiji la Dar es Salaam ulijitokeza jana kuuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, huku ugonjwa uliosababisha kifo chake ukitajwa kuwa ni figo kushindwa kufanya kazi.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile, alibainisha hayo wakati wa kuuaga mwili huo katika viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam jana wakati akisoma wasifu wa marehemu Dk. Mgimwa aliyefariki dunia Januari Mosi, mwaka huu katika Hospitali ya Kloof Medi-Clinic, Pretoria, Afrika Kusini.


“Dk. Mgimwa alikwenda Afrika Kusini Novemba 3, mwaka jana kwa ajili ya uchunguzi wa afya na madaktari baada ya kumchunguza walimshauri alazwe baada ya kugundua afya yake siyo nzuri, na alifariki Januari 1, mwaka huu kwa ugonjwa wa figo,” alisema Dk. Likwelile.

Viongozi wa serikali waliohudhuria shughuli hiyo, ni Rais Jakaya Kikwete; Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal; Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue; Spika wa Bunge, Anne Makinda; Waziri wa Fedha wa Uganda, Aston Kajara na mke wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Mama Maria Nyerere.

Wengine ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe; Mweneyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba; Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia; Makamu Mwenyeki CCM (Bara), Philip Mangula na Katibu Mkuu CCM, Abdulrahman Kinana.

Kadhalika alikuwapo Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange; Inspecta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu na Kamishina Jenerali wa Magereza, John Minja.
Wengine ni Mawaziri, Makatibu wa Wizara, Wabunge, Mabalozi, Wakuu wa idara mbalimbali na wakuu wa mikoa.

Mwili wa marehemu Dk. Mgimwa uliwasili katika viwanja hivyo saa 4:40 asubuhi ukiwa katika gari maalumu la kubebea maiti lenye namba za usajili T. 607 BYX, na kushushwa katika gari saa 4:46 na askari maalumu wa Bunge.


Waziri wa Fedha wa Uganda, Aston Kajara, akizungumza kwa niaba ya mawaziri wa fedha wa Afrika Mashariki, alisema mchango wa marehemu ulikuwa mkubwa hususani katika mchakato wa kupatikana kwa sarafu moja.


Alisema Dk. Mgimwa alikuwa na mchango mkubwa walipokuwa wanakutana mawaziri wa Afrika Mashariki (EA) katika masuala mbalimbali ya uchumi.

Mwakilishi wa Washiriki wa Maendeleo (DPs), Dk. Alberic Kacou, alisema kifo cha Dk. Mgimwa ni pengo kwa taifa.

Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alisema enzi za uhai wa Dk. Mgimwa hakuwahi kugombana na chama chochote, wala hakuendekeza uadui, ugomvi katika siasa na kutaka mazuri yake yaigwe.


Katibu wa wabunge wa CCM, Jenister Mhagama, alisema Dk. Mgimwa alikuwa kiongozi makini aliyekuwa anatoa mawazo mazito.


Spika wa Bunge, Anne Makinda, alisema Dk. Mgimwa alikuwa ni mtu mwelewa na kama kungewapo na uwezo wa kumbadilisha mtu ili Dk. Mgimwa arudi angefanya hivyo, na kueleza kuwa mbegu alizopanda hazitaharibika.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mohammed Aboud, alisema kifo cha Dk. Mgimwa siyo pigo kwa Tanzania Bara tu bali hata Zanzibar, na kumweleza alikuwa mtu mwaminifu.


Kaimu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, alisema Dk. Mgimwa alikuwa kielelezo, kiongozi shupavu, anayeheshimu mawazo ya kila mtu na mwalimu kwa miezi 20 waliyofanya naye kazi.


Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, James Mbatia, alisema Dk. Mgimwa alikuwa ni mtu mchapakazi na alikuwa anafanya kazi zaidi ya saa 16, na kueleza kuwa usikivu wake, uweledi wake pamoja na elimu yake lakini hakujigamba nayo.


Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Dk. Stergomena Tax, alisema Dk. Mgimwa alikuwa na mchango mkubwa katika vikao vya SADC haswa katika uhamasishaji wa sera za bajeti na mipango ya fedha.


Mwili wa marehemu Dk. Mgimwa uliondolewa katika viwanja hivyo saa 8: 40 alasiri kuelekea Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere kwa safari ya Iringa ambako leo shughuli za kuuzika zitafanyika kijijini kwake.


PINDA AKAGUA MAANDALIZI YA MAZISHI

Wakati mwili wa Dk. Mgimwa ukiagwa Dar es Salaam, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, jana asubuhi aliwasili mkoani Iringa na kwenda katika kijiji cha Magunga, tarafa ya Kiponzelo, wilayani Iringa, kukagua maandalizi ya mazishi.

Dk. Mgimwa anatarajiwa kuzikwa leo nyumbani kwake kwenye makaburi ya familia.

Baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Nduli mkoani Iringa jana, mwili huo ulipokelewa na viongozi wa mkoa, Waziri Mkuu kabla ya kusarishwa hadi Magunga umbali wa kilomita 66 kutoka Iringa mjini.

Akiwa kijijini hapo Waziri Mkuu aliwapa pole mama mzazi wa marehemu, Consolata Semgovano, wajomba zake na wafiwa wengine.


Pia alikagua kazi ya ujenzi wa kaburi atakamozikwa Dk. Mgimwa, uwekaji wa mahema pamoja na eneo la kufanyia ibada ya mazishi.


Vilevile, alikagua mahali mwili wa marehemu ungelazwa jana usiku ukisubiri taratibu za mazishi leo.


Baada ya shughuli hiyo, Waziri Mkuu alirejea mjini Iringa ili kuusibiri mwili ambao uliwasili Uwanja wa Ndege wa Nduli jana jioni na kwenda kuagwa na wakazi wa Iringa kwenye ukumbi wa ‘Siasa ni Kilimo’ kisha ukapelekwa kijijini kwake Magunga.


MWILI WAWASILI, IRINGA YAZIZIMA

Mji wa Kalenga ambako ndipo alikozaliwa Waziri Mgimwa, umesitisha shughuli zake kwa siku ya pili baada ya serikali kutangaza kwamba mwili wake utalala katika kijiji cha Magunga.

Jana NIPASHE ilishuhudia maduka na sehemu nyingi za biashara katika jimbo hilo zikiwa zimesimama huku mji wa Iringa na viunga vyake ukizizima kutokana na msiba huo.


Makundi ya wananchi yalionekana yakiwa yamejikusanya kandokando ya barabara kuu ya Iringa-Ruaha yakisubiri kushuhudia mwili huo ukiwasili ukitokea Uwanja wa Ndege wa Nduli.


Ibada ya mazishi hayo itaongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Iringa, Tarcius Ngalalekumtwa ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).

Katika hatua nyingine, vilio na simanzi vilitanda jana jioni baada ya mwili wa Dk. Mgimwa kuwasili mjini Iringa saa 10:30 na kupokelewa na mamia ya wakazi wa mji huo.

Mamia ya watu walijitokeza kwa wingi uwanjani hapo wakiwamo viongozi mbalimbali wa serikali, dini pamoja na wanasiasa kwa ajili ya kutoa sheshima za mwisho katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo huku walielezea masikitiko yao kuwa taifa limepoteza kiongozi msikivu na anayejua kujishusha mbele ya umma.


Ilipofika saa 12:10 jioni shughuli za usafirishaji katika mji wa Iringa zilisimama wakati mwili huo ulipopitishwa ukielekea kijiji cha Magunga kwa mazishi yatakayofanyika leo. 
SOURCE: NIPASHE 
By Mwandishi wetu \
 6th January 2014

Related Posts:

0 comments: