>>RAIS WA TFF MALINZI AHUTUBIA….!!
PATA TAARIFA KAMILI:
TAARIFA YA MAKABIDHIANO YA OFISI YA TFF YALIYOFANYIKA KATIKA OFISI ZA TFF JIJINI DAR ES SALAAM TAREHE 2 NOVEMBA 2013
Mheshimiwa Rais wa TFF,
Pongezi na Shukurani
1. Naomba nianze kwa kushukuru kwa
kukubali kufanyika kwa shughuli hii ya makabidhiano ya Ofisi. Utaratibu
huu haupo kikatiba wala katika kanuni zetu, lakini ni muhimu sana kwa
vile unatoa taswira ya uongozi endelevu na ushirikiano unaostahili
kuwepo baina ya uongozi mpya na ule wa zamani.
2. Aidha napenda, kwa mara
nyingine, kukupongeza kwa dhati wewe binafsi kwa kuchaguliwa kwako kuwa
Rais wa Shirikisho letu pamoja na kumpongeza Makamu wa Rais na Wajumbe
wa Kamati ya Utendaji kwa ushindi wao.
3. Tumeshuhudia mchakato wa
uchaguzi uliofanyika kwa uwazi, na ulio huru na wa haki. Ninawashuru
sana na kuwapongeza Wajumbe wa Kamati ya Uchanguzi kwa ueledi na kazi
nzuri walioifanya. Kwa kiwango hicho hicho ninawapongeza na kuwashukuru
Wajumbe wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi na wa Kamati za Maadili – ngazi
ya awali na ya rufani – kwa kutekeleza wajibu wao kikamilifu na vyema.
4. Nawajibika kutoa pongezi kwa
Wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa kukamilisha kazi muhimu ya kutuchagulia
viongozi wetu kwa utulivu mkubwa.
5. Utulivu wakati wa mchakato
mzima wa uchaguzi – kuanzia mwanzo hadi mwisho – ni kielelezo cha
ukomavu wa uongozi wa mchezo wa mpira wa miguu nchini. Natoa shukurani
za dhati kwa wanachama na wadau wote wa mpira wa miguu nchini kwa
mchango wao wa hali na mali katika kufanikisha zoezi hili muhimu kwa
mustakabali wa mpira wa miguu nchini.
Dira na Malengo ya Uongozi Uliopita
6. Dira ya uongozi uliopita
ilikuwa ni kujenga mazingira mazuri na endelevu ya maendeleo ya mchezo
wa mpira wa miguu nchini. Hii ilitokana na hali ya migogoro isiyoisha na
malumbano ya mara kwa mara yaliyokuwepo kabla ya kuingia madarakani.
7. Ili kufanikisha dira yetu,
uongozi uliopita ulidhamiria kujenga msingi bora wa uongozi wa mpira wa
miguu nchini, hivyo kujiwekea malengo yafuatayo:
Kutengeneza Katiba mpya na Kanuni
zitakazokidhi mahitaji ya nchi yetu ya kudumisha demokrasia na utawala
bora – uwazi, uwajibikaji, na kadhalika.
Kuhakikisha kuwa Katiba yetu na Kanuni zetu zinazingatiwa na kuheshimiwa.
Kuweka Kanuni za Fedha na kuchukua hatua
za kujenga uaminifu katika usimamizi wa ukusanyaji, utunzaji na
matumizi ya fedha. Tuliazimia kuona hesabu za Shirikisho zinakaguliwa
na wakaguzi wenye sifa za kimataifa, na taarifa ya ukaguzi kuwasilishwa
kwenye Mkutano Mkuu kila mwaka, bila ya kukosa.
Kuwa na mfumo wa mashindano utakaongeza
ushindani na kuchochea uwekezaji. Azma ilikuwa ni kuongeza idadi ya
mashindano ili kutoa fursa kwa vipaji kuonekana na kuendelezwa.
Kuweka jitihada katika mafunzo ya
wataalamu wa mpira wa miguu nchini kwa kuongeza idadi na kozi/semina za
mafunzo ya uongozi, uamuzi, ualimu na udaktari wa michezo.
Kujenga mfumo mpya wa uongozi wa timu za
taifa. Lengo lilikuwa ni kuhakikisha kuwa timu za taifa zinakuwa na
uongozi wake chini ya Mwalimu/Walimu wa timu ya taifa na kuzitofautisha
na Idara ya Ufundi, pamoja na kuhakikisha timu zetu za taifa zinashiriki
michezo mingi iwezekanavyo ya mashindano na ya kirafiki.
Kujenga uhusiano mzuri na wadau na
washirika wetu, hususan wadau wetu wakuu ambao ni Serikali na vyombo
zake; Mashirikisho ya mpira tuliyojumuika nayo - FIFA, CAF, na CECAFA;
Wadhimini na Wafadhili wetu – kampuni, mashirikia ya umma na watu
binafsi - wanaochangia maendeleo ya mpira wa miguu nchini kwa hali na
mali.
Kuwa karibu na jamii na kuisaidia jamii.
Nia ni kutumia umaarufu wa mchezo wa mpira wa miguu nchini kuhamasisha
maendeleo ya jamii, hasa katika masuala ya afya ya jamii – kampeni ya
malaria, ukimwi, kupambana na madawa ya kulevya na kadhalika. Rais
anayeondoka madarakani ni Balozi wa Malaria nchini na Rais wetu mpya ni
mjumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Kupambana na Malaria, chini ya Uenyekiti
wa Waziri wetu wa Afya, Mheshimiwa Hussein Mwinyi.
8. Utekelezaji wa Dira
tuliyojiwekea na malengo yetu ulifanyika kwa ushirikiano wa karibu na
wanachama na wadau wetu. Yaliyofanyika yanajulikana. Itoshe kusema kuwa
kazi hiyo ilifanyika kwa jitihada kubwa na uadilifu mkubwa na kwamba
malengo tuliyojiwekea yalifikiwa.
9. Katika hotuba niliyoitoa katika
Ufunguzi wa Mkutano Mkuu uliopita – Jumamosi, tarehe 26 Oktoba 2013,
niliainisha kwa kina nini kilifanyika katika kipindi cha uongozi
uliopita pamoja na mafanikio ya kazi iliyofanyika. Napenda kuimbatanisha
hotuba hiyo kama sehemu ya taarifa hii ya makabidhiano.
10. Matarajio yetu ni kuwa, baada ya
jitihada za kuweka msingi wa uongozi na wa maendeleo ya mpira wa miguu
nchini, nguvu itaelekezwa katika kukuza kiwango cha mpira wa miguu
nchini mwetu.
Tulichokifanya ni kutayarisha Mpango wa Muda Mrefu wa Maendeleo ya Mpira Miguu Nchini – 2013 hadi 2016 (Long Term Technical Development Plan – 2013 to 2016), ambayo umeambatanishwa kama sehemu ya taarifa hii ya makabidhiano.
11. Hivyo basi, uongozi mpya una
kazi ya kusimamia na kufanikisha utekelezaji wa Mpango huo. Pia, ni
matarajio yetu kuwa uongozi mpya utayadumisha mambo ya msingi
tuliyojiwekea na kuufanyia kazi upungufu uliopo.
Shukurani kwa Wanachama na Wadau wa TFF
12. Pamoja na kuwa nimeshatoa
shukurani mara kadhaa, napenda kwa mara nyingine tena kuwashukuru wote
waliotusaidia kufika hapa tulipo. Nawashukuru sana wanachama wetu, wadau
wetu wote – Serikali yetu na vyombo vyake vyote, wadhamini na
wafadhili, waandishi na vyombo vya habari, wapenzi wa mpira na wananchi
kwa ujumla kwa mchango wao wa hali na mali. Bila yao tusingefika hapa
tulipofika.
13. Shukurani maalum zimwendee
Mheshimiwa Rais wetu, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, kwa mchango wake
usiopimika. Alikuwa ni sehemu mabadiliko haya tangu mwanzo, hata kabla
ya uongozi wetu kuingia madarakani. Ametusaidia kwa kiasi kikubwa
kuzijenga timu zetu za taifa siyo tu kwa uamuzi wake wa kulipia
mishahara ya walimu wa timu ya taifa, bali pia kwa kuwahamasisha vijana
wetu kwa hali na mali wafanye vizuri. Sina hakika kuwa yupo Rais
mwingine, popote pale duniani, aliye karibu na mapenzi ya dhati kwa
vijana wa timu zake za taifa zaidi ya Rais wetu. Zaidi ya hayo,
Mheshimiwa Rais amekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha utawala bora
katika mpira wa miguu nchini na amefanya kila aliloliweza kuona kuwa
kiwango cha mchezo kinapanda na timu zetu zinafanya vizuri. Napenda
kutoa shukurani za dhati kwake kwa uongozi na msaada wake.
Wanachama, Katiba na Kanuni, Wafanyakazi, Mali na Mikataba ya TFF
14. Wanachama
TFF ina jumla ya Wanachama 44 ambao wote ni wanachama hai kama ifuatavyo:
Vyama vya Mikoa – 25
Vyama Shiriki - 5
Vilabu vya Ligi Kuu - 14
15. Katiba na Kanuni
Hivi sasa TFF ina Katiba Mpya (ya Mwaka
2013) iliyofanyiwa marekebisho ya mwisho na Mkutano Mkuu Maalum wa TFF
tarehe 13 Julai 2013.
Pamoja na Katiba TFF ina kanuni zifuatazo ambazo kwa mujibu wa Katiba ya TFF hupitishwa na kamati ya Utendaji:
Kanuni za Fedha
Kanuni za Mashindano kuanzia Ngazi ya Wilaya hadi Ligi Kuu
Kanuni za Utii
Kanuni za Nidhamu
Kanuni za Maadili
Kanuni za Uchaguzi za Uchaguzi za TFF na za Wanachama wa TFF
Kanuni zinazosimamia Uendeshwaji wa Bodi ya Ligi Kuu
Kanuni za Mashindano mengine, kama vile
Copa Coca Cola, Uhai Cup, Super 8 na Taifa Cup. Ni vyema ikafahamika
kuwa kila mashindano lazima yawe na Kanuni zinazosimamia uendeshwaji
wake.
TFF inalazimika kuzifanyia marekebisho
Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wake kufuatia marekebisho ya Kanuni za
Uchaguzi za TFF. Aidha, TFF inadeni la kutayarisha Kanuni za Chombo cha
Usuluhishi (Arbitration Tribunal) kama ilivyoainishwa katika Katiba.
Hivi karibuni, TFF imepokea Kanuni za Mfano kutoka FIFA ambayo ipo haja
ya kazi hii kukamilishwa na uongozi mpya.
16. Wafanyakazi wa TFF
Hivi sasa TFF ina jumla ya wafanyakazi 29. Kati yao yupo/wapo
Katibu Mkuu - 1
Wakurugenzi / Maofisa Mwandamizi - 5
Wafanyakazi wengine - 23
Katibu Mkuu na Wakurugenzi wapo katika
kipindi cha nyongeza cha miezi sita (6) cha mikataba yao, kinachoishia
mwishoni mwa mwezi Desemba
2013. Wafanyakazi wengine wapo katika mikataba ya miaka minne yenye
kipindi cha majaribio cha miezi sita kuanzia mwanzoni mwa mwezi Septemba
2013. Hivyo basi, uongozi mpya una nafasi ya kufanya tathmini ya
mahitaji ya TFF kisha kufanya uamuzi juu ya ajira za Wafanyakazi waliopo
kadiri utakavyoona inafaa.
TFF ilichukua hatua ya kuingia kufanya
makubaliano ya hiari na wafanyakazi wake ili kuondokana na ajira za
maisha (Permanent Employment) na kubaki na ajira za mikataba (Contract
Empoyment) kwa wafanyakazi wake wote.
Wafanyakazi wa TFF wamekuwa wakifanya
kazi ngumu na saa nyingi kuliko kawaida. Ajira ya TFF haina saa za ziada
wala siku za mapumziko. Kutokana na dhana ya kujitolea na ukweli kwamba
shughuli nyingi za TFF, kama vile michezo na mikutano hufanyika siku za
mwisho wa wiki na sikukuu, ni dhahiri kuwa Wafanyakazi wa TFF wamekuwa
wakilazimika kufanya kazi siku hizo, na mara nyingi bila malipo ya saa
za ziada. Aidha, kutokana na kukosa uwezo, uongozi uliopita ulishindwa
kupandisha mishahara yao ipasavyo.
Napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza
na kuwashukuru kwa kuihudumia TFF na mpira wa miguu katika mazingira
magumu sana. Tunauomba uongozi mpya uliangalie suala hili kwa umakini,
kama moja ya hatua za kuongeza ufanisi wa Sekretariati.
17. Mali za TFF
Hivi sasa TFF ina mali zifuatazo:
Kiwanja cha Karume Stadium, chenye hati
namba 27026 iliyotolewa tarehe 10 Novemba 1981. Kiwanja cha Karume kina
ukubwa wa ekari 8.26. Ombi la kuingezea muda hati hiyo limeshapelekwa na
linafuatiliwa.
Ndani ya Kiwanja hicho, kuna Jengo la
ofisi ya TFF, Jengo la Kituo cha Ufundi (Technical Centre) na Uwanja wa
nyasi za bandia wa Karume.
Kiwanja cha Tanga chenye ukubwa wa hekta
7.6 (ekari 19) kilichopo katika eneo zuri sana mjini Tanga. Kiwanja
hiki tayari kimeshalipiwa na hivi sasa taratibu zinaendelea kukamilisha
taratibu za kukiandikisha na kupata hati.
Magari sita (6) na Trekta moja (la
kusafishia uwanja wa nyasi bandia). Magari hayo ni: Bus kubwa aina ya
Yutong, basi dogo aina ya Coaster, magari ya aina 4WD Ford Everest, Rav
4, Suzuki Escudo na Honda CVR. Mawili kati magari hayo - Suzuki Escudo
na Honda CVR – yanatumika lakini hayapo katika hali nzuri. Ni vyema
uongozi mpya ukayafanyia tathmini magari hayo na kufanya maamuzi muafaka
kadiri utakavyoona inafaa.
Fedha taslimu Shilingi 33,518,000 na US$
1,390 zipo katika akaunti hivi sasa. Hii ni baada ya TFF kufanya malipo
ya Shilingi 158,000,000 kwa ajili ya Mkutano Mkuu (uliofanyika wiki
iliyopita) na malipo ya Shilingi 56,240,000 yaliyofanyika kwa ajili
matayarisho ya Timu ya Taifa ya Wanawake U-20 na gharama za mchezo baina
ya timu yetu ya Taifa na ile ya Msumbiji uliofanyika wiki iliyopita.
Hata hivyo, leo hii US$ 415,000 (Shilingi 664,000,000) kimehamishwa
kutoka kwenye Akaunti za TBL kwenda kwenye Akaunti za TFF. Fedha hizo
zitakuwa tayari kwenye Akaunti ya TFF ifikapo Jumanne wiki ijayo.
Malipo haya yalikuwa yafanyike karibu miezi miwili iliyopita lakini
yalicheleweshwa ili kutoa nafasi kwa zoezi la ukaguzi wa fedha za
udhamini wa TBL kufanyika. Zoezi limefanyika vyema na kufikia ukingoni,
ndiyo maana malipo yamefanyika. Malipo mengine yanayofanana na hayo, ya
US$ 420,000 (Shilingi 672,000,000) yanatarajiwa kufanyika wiki mbili
kutoka sasa - katikati ya mwezi huu wa Novemba 2013.
Hivyo basi, uongozi unaoingia madarakani
hautaanza kwa shida. Ni matarajio yetu kuwa hatua ya awali itakuwa
kurejesha fedha kwenye akaunti zilikoazimwa kinachofikia US$ 166,509 -
US$ 148,174 kutoka kwenya Akaunti za FAP na US$ 18,335 kutoka kwenye
Akaunti ya TRA - kwa ajili ya kugharimia Mkutano Mkuu na matumizi ya
Taifa Stars kwa ajili ya matayarisho na safari ya kwenda Gambia.
Ili kujiridhisha kuwa fedha za udhamini
zinatumika kama ilivyokubalika katika mikataba, TFF imetoa nafasi kwa
wadhamini kufanya ukaguzi wa fedha inazozitoa wakati wowote ule.
Utamaduni huu tumekuwa nao katika kipindi chote cha utawala wa uongozi
wetu, ili kutoa imani kwa wadhamini na kuhakikisha kuwa malengo ya
udhamini husika yanafanikiwa. Huu ni utaratibu mzuri na ni matumaini
yetu kuwa utadumishwa.
Jengo la Kituo cha Ufundi ndiyo kwa
limekamilika kukarabatiwa na bado halijafunguliwa rasmi. Ukarabati huo
umefanikisha kutengenezwa kwa mfumo wa maji machafu unaojitegemea.
Hivyo, kutohitaji kutengemea mashimo ya Jengo la Ofisi za TFF. Hatuo ya
mwisho ya kazi hiyo ni kukamilisha ukaguzi wa matumizi yaliyofanyika
katika ukarabati huo na kuiwasilisha CAF mapema iwezekanavyo. Hayo ndiyo
makubaliana kuhusiana na msaada uliotolewa na CAF – unaojulikana kama
CAF FAP 2.
Ukarabati wa Kituo cha Ufundi umefanywa,
pamoja na sababu nyingine, ili kutoa fursa kwa Mradi wa Ujenzi wa
Karume kuendelea. Kama nilivyoeleza katika Mkutano Mkuu, dhamira ni
kuwekeza katika Mradi wa Ujenzi wa jengo / majengo yenye hadhi kubwa kwa
ajili ya kukodishwa kuzunguka uwanja huo. Jengo lililo karabatiwa na
uwanja wa mpira vitabaki na kuendelea kutumiwa kama Kituo cha Mafunzo.
Jambo la muhimu ni kuhakikisha kuwa uwekezaji katika mradi huo hauhitaji
dhamana ya uwanja wetu na majengo yetu. Ni imani yetu kuwa njia muafaka
inapatikana, ikiwa ni pamoja na utaratibu wa ‘Build, Operate and
Transfer’ (BOT).
18. Hesabu za TFF
Ripoti ya Ukaguzi wa hesabu za TFF hadi
kufikia Desemba 2012 iliwasilishwa katika Mkutano Mkuu uliopita. TFF
ilipata Hati Safi ya Ukaguzi wa hesabu zake na Mkutano Mkuu ukaikubali
na kuipitisha ripoti hiyo hesabu za mwaka 2012. Aidha, taarifa ya hesabu
za TFF kwa kipindi cha kuanzia tarehe 1 Januari hadi 30 Septemba 2013
kusambazwa kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu.
Ifahamike kuwa TFF imekuwa ikipata Hati
Safi, kila mwaka katika kipindi cha miaka minane iliyopita. Hatuna shaka
kuwa hali hii itaendelea.
19. Mikataba ya Udhamini
TFF inayo mikataba ifuatayo ya udhamini na Wadhamini wafuatayo:
Vodacom – Udhamini wa Ligi Kuu
TBL – Taifa Stars
Coca Cola – Mashindano ya Copa Coca Cola
SSB & Co – Mashindano ya Uhai
Bank ABC – Super 8
Azam Media – Haki za Matangazo ya Television kwa Ligi Kuu
Aidha, baadhi ya vilabu kama vile Yanga
na Simba vinadhaminiwa na TBL, Coastal Union inafadhiliwa na Tanga
Cement na Azam FC inadhaminiwa na Azam Cola.
Changamoto zinazoikabili TFF
20. Zipo changamoto nyingi
zinazoikabili TFF lakini kubwa kwa maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu
na ambazo uongozi mpya hauna budi kuzishughulikia ni ulazima wa:
Kuendeleza sola la vijana na watoto kwa
kutoa fursa kwa watoto/vijana wengi kupata malezi mazuri ya uchezaji wa
mpira wa miguu ili kupanua wigo wa kupata wachezaji wenye vipaji. Katika
jambo hili bado tuko nyuma sana. Tulididimia sana kutokana na kufutwa
kwa michezo mashuleni. Ipo haja ya uongozi mpya kushirikiana na Serikali
kuhamisha michezo shuleni, kama hatua ya wali ya kutatua tatizo la soka
la vijana/watoto.
Kuendeleza soka la wanawake. Matatizo ya
soka la wanawake yanafanana na ya soka la vijana. Tofauti ni ndogo
sana. Kama ilivyo kwa soka la vijana, hatua muhimu kufanyika kwa
jitihada ya kuwahamasisha wasichana wacheze mpira wa miguu shuleni.
Kuhakikisha ueledi unazingatiwa katika
uongozi wa Vilabu na Vyama Wanachama wa TFF. Kinyume chake hatutaweza
kushindana na wenzetu ambao walishapiga hatua katika taaluma ya uongozi
wa michezo. Vilabu vyetu ni lazima vihakikishe kuwa vinatimiza masharti
ya ‘Club Licencing’ kama yalivyotolewa na CAF, pamoja na marekebisho
yake. Huu ni mtihani kwetu. Ni lazima tufaulu kutimiza masharti hayo,
vinginevyo tutabaki nyuma. Ipo haja ya kuuangalia kwa mfumo wa uongozi
wa Vilabu vyetu na Vyama Vyetu kwa azma ya kubuni mfumo utakaotuletea
ufanisi zaidi wa kiungozi na uendeshaji kuliko ilivyo hivi sasa.
Kuhamasisha uwekezaji katika maendeleo
ya mchezo wa mpira wa miguu nchini. Tuna upungufu mkubwa wa vifaa na
viwanja vya kuchezea. Ni vigumu kuundeleza mchezo wa mpira bila ya kuwa
na viwanja vya kuchezea na vifaa. Aidha, zinahitajika raslimali watu na
fedha katika kulea na kuwaendeleza wachezaji na wataalamu wetu. Licha ya
hapo kiasi kikubwa cha fedha kinahitajika kwa ajili ya matumizi mengine
ili timu ifanye vizuri. Kwa maneno mengine tunahitaji kufanya kila
jitihada kuhamasisha watu binafsi, makampuni na Serikali iwekeze katika
mpira, wadhamini zaidi wajitokeze na wapenzi wengi zaidi wachangie timu
zao – kwa njia mbalimbali - ili kuongeza mapato ya vilabu na vyama
husika. Vilabu vyetu na Vyama Wanachama wa TFF vinakabiliwa na upungufu
mkubwa wa fedha za uendeshaji. Mawazo au fikra kuwa kuna fedha nyingi
katika mpira wa miguu ni dhana isiyo na msingi na inayotokana na
kutofahamu gharama za uendeshaji wa vilabu na vyama vyetu. Pamoja na
ongezeko kubwa la mapato ya milangoni na mchango wa udhamini katika
kipindi cha uongozi uliopita, bado kinachopatikana hakikidhi hata
theluthi moja ya mahitaji muhimu. Haja ya kuongeza mapato ndiyo
changamoto mama. Ikitatuliwa itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza
makali ya changamoto nyingine.
Ili kuvutia uwekezaji, udhamini na
misaada kwenye mpira wa miguu, ni lazima tuhakikishe kuwa tunaendelea na
jitihada za kujenga uaminifu wa utunzaji na matumizi ya fedha ndani ya
TFF. Ipo haja ya kuhakikisha kuwa Kanuni za Fedha zinazingatiwa na
hesabu zetu zinakaguliwa mara kwa mara. Mpango wa Tiketi za Elektroniki
ni muhimu usimamiwe kwa nguvu zote kwa vile sio tu utatuongezea mapato
bali pia utatoa picha ya uaminifu na ueledi.
Uhusiano na ZFA
21. TFF haina budi kufanya kila
linalowezekana kudumisha uhusino mzuri baina yake na ZFA. TFF
inatambulika na FIFA kama msimamizi wa mchezo wa mpira wa miguu nchini
Tanzania. Lakini ukweli ni kuwa mchezo wa mpira katika visiwa vya Unguja
na Pemba unasimamiwa na ZFA. Hakuna matarajio ya hali hiyo kubadilika.
Kwa sababu hiyo, upo ulazima wa kudumisha uhusiano uliopo na kuhakikisha
kuwa ZFA inapata haki ya kupewa baadhi ya miradi inayotokana na fedha
za FIFA – FAP. Kwa vile fedha hizo hatolewa kwa njia ya miradi,
utaratibu tuliokubaliana ni kuhakikisha kuwa kila mwaka baadhi ya miradi
/ semina zinafanyika visiwani.
Wakaguzi wa Hesabu za TFF
22. Hesabu za TFF zinakaguliwa makampuni ya Ukaguzi wa Hesabu yafuatayo:
TAC Associates – kwa hesabu zote za TFF
KPMG – kwa fedha za FIFA
Bodi ya Wadhamini
23. Mkutano Mkuu wa Mwaka 2011
uliridhia kuundwa kwa Bodi ya Wadhamini wa TFF na Mkutano Mkuu uliopita
ulipitisha majina ya Wajumbe wa Bodi ya Udhamini kama ifuatavyo:
Said El Maamry – Mwenyekiti
Mh. Joel Bendera – Makamu Mwenyekiti
Dr. Ramadhani Dau – Mjumbe
Steven Mashishanga – Mjumbe
Mohamed Abdulaziz - Mjumbe
Mheshimiwa Rais, napenda kukubidhi
taarifa hii ya makabidhiano leo hii tarehe 2 Novemba 2013 kwa ufahamu na
kumbukumbu za TFF. Tafadhali jisikie huru kuomba ufafanuzi wa jambo
lolote lililomo katika taarifa hii au kuomba taarifa juu ya jambo ambalo
kwa bahati mbaya limesahauliwa. Sekretariati ya TFF inawajibika kutoa
ufafanuzi unaohitajika.
Tunakutakia wewe mwenyewe na uongozi
wako kila la heri na mafanikio katika kuingoza wa TFF kuelekea kule
kunakotarajiwa na wapenzi wa mpira wa miguu nchini. Wadau na wapenzi
wote wa mpira wa miguu wanaoitakia heri nchi yetu wapo nyuma yako.
Leodegar Tenga Angetile Osiah
RAIS WA TFF KATIBU MKUU WA TFF
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
TANZANIA FOOTBALL FEDERATION
HOTUBA YA RAIS WA TFF KWENYE HAFLA YA MAKABIDHIANO
TAREHE 02 NOVEMBA 2013
Ndugu mgeni rasmi ……..…………………………………………….
Ndugu…………………………………. Mwakilishi wa Wizara
Ndugu…………………………………. Mwakilishi wa BMT
Ndugu…………………………………. Mwakilishi wa wadhamini
Ndugu Leodegar Tenga Rais aliyemaliza muda wake
Ndugu Said El Maamry Mwenyekiti mstaafu wa iliyokuwa FAT
Ndugu Muhidin Ndolanga Mwenyekiti mstaafu wa iliyokuwa FAT
Wajumbe wa Baraza la Wadhamini
Wajumbe wa Kamati ya Utendaji
Wafanyakazi wa TFF
Wageni waalikwa
Mabibi na Mabwana
Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kuwa hapa leo.
Awali ya yote naomba nichukue fursa hii
kukupongeza Rais wetu uliyemaliza muda wako Ndugu Leodegar Tenga na
Kamati yako ya utendaji . Mliyoufanyia mpira wa Tanzania ni makubwa,
historia haitawasahau. Mmetujengea taasisi imara isiyotetereka, taasisi
inayoheshimika ndani na nje ya mipaka ya nchi hii, nawashukuru na
kuwapongeza sana.
Uchaguzi umekwisha. Mchakato ulikuwa
mrefu. Wapo walioshinda na wapo ambao kura zao hazikutosha. Wote tuna
kazi moja tu kujenga mpira. Kama tulikwaruzana kwenye kampeni
tusameheane, tuwe kitu kimoja, tuinyanyue soka yetu. Makundi hayajengi
yanabomoa, tuachane nayo.
Ndugu zangu, uongozi wetu ulioingia
madarakani alfajiri ya tarehe 28-11-2013 unakabiliwa na changamoto
nyingi. Nitaelezea changamoto chache zinazohitaji ufumbuzi wa haraka.
Mashindano yanayotukabili.
Tunakabiliwa na mashindano mbalimbali ya
kimataifa. Mfano ni mechi ya marudiano ya U/20 wanawake dhidi ya
Msumbiji wiki ijayo, Mitoano ya mashindano ya Afrika wanawake mapema
mwakani, Mashindano ya Chalenji Novemba mwaka huu, na mashindano ya
kufuzu AFCON 2015. Yote haya yanahitaji maandalizi ya haraka.
Programu ya vijana.
Ilani yangu ya uchaguzi ilielezea azma
ya Tanzania kuomba uenyeji wa fainali za vijana za Afrika U/17 mwaka
2019. Jambo hili tutalizungumzia kwenye kikao chetu cha utendaji leo.
Ili tuwe na timu nzuri ya kucheza fainali hizo tukiwa wenyeji hatuna
budi mwaka kesho kuunda timu ya Taifa ya U/12 itakayokua pamoja kuelekea
2019. Programu yetu ya vijana tutakayoiandaa sharti ijielekeze kwenye
ratiba hii.
Udhamini wa timu za vijana na za wanawake
Hii ni changamoto kubwa sana kwa TFF.
Timu zetu za Taifa kuanzia zile za wakubwa hadi za vijana ni brands, na
kama ni brands inabidi ziingizwe sokoni, ziuzwe kwa tunaodhamiria wawe
wadhamini wa hizo timu. Kitengo cha masoko lazima kiimarishwe ili
kukabiliana na changamoto hizi. Mdhamini ni mfanyabiashara, anapotoa
pesa kudhamini brand fulani anategemea matokeo mazuri kwake kwa njia ya
kukuza biashara zake. Twende kwa wadhamini tuwashawishi waone
watafaidikia nini (leverage) kwa kudhamini timu zetu. Tusisubiri waje
tuwafuate sisi.
Uwekezaji
Jitihada za haraka lazima zifanyike
kuiongezea TFF uwezo wa kiuchumi. Ni muhimu mtaalam mshauri (consultant)
atafutwe atufanyie mchanganuo wa uwekezaji katika ardhi yetu hii ya
Karume ili tuwekeze kitega uchumi kama ilivyokubaliwa kwenye mkutano
mkuu. Aidha bidhaa zenye nembo yetu zianze kuuzwa kwa utaratibu maalum
ili shirikisho lipate haki yake.
Kabla sijamaliza kuzungumza, niongelee
suala la fujo viwanjani. Mpira ni dakika tisini. Katika kipindi hicho
uamuzi wa mwamuzi unakuwa ni wa mwisho. Tusifiche upungufu wa timu zetu
kwa kujificha nyuma ya kivuli cha mwamuzi. Waamuzi wakionekana wamefanya
makosa yawe ya makusudi au ya bahati mbaya vyombo vya kuwahukumu vipo,
mahakama ya waamuzi sio mashabiki. Kitendo cha mashabiki kufanya fujo
kabla, wakati na baada ya mechi ya mpira kamwe hakikubaliki mahali
popote duniani. Kanuni za FIFA, CAF na TFF ziko wazi na adhabu
zinajulikana. Moja ya adhabu hizi ni timu husika kucheza kwenye uwanja
mtupu usio na mashabiki kama ilivyowatokea Al Ahly na Zamalek huko Misri
au kucheza nje ya uwanja wako kama ilivyowatokea Senegal ambao baada ya
vurugu Dakar, Senegal waliamriwa na FIFA mechi zao za nyumbani wachezee
nje ya nchi na wakachagua kuchezea Morocco.
Ndugu zangu yaliyotokea majuzi Mbeya na
Dar es salaam wote tumeyasikia na wengine miongoni mwetu hapa ni
mashuhuda. Ninasema iwe mara ya kwanza na y a mwisho. Kwenye masuala ya
kutekeleza mahitaji ya kanuni uongozi wangu hautaionea haya klabu
yoyote, iwe mpya au kongwe kwenye ligi yetu. Ni jukumu la viongozi wa
klabu kudhibiti wanachama na wapenzi wao. Tabia ya benchi la ufundi
kutoa matamshi yanayoweza kuamsha hisia za mashabiki ni kinyume na
taratibu na kanuni ziko wazi kuhusu jambo hili. Viongozi wa klabu na
mabenchi yao ya ufundi wakishindwa kutekeleza wajibu wao tusilaumiane.
Ndugu zangu ya kufanya ni mengi katika
kuiendeleza soka yetu. Tunashukuru Mungu kuwa uwezo wa kukabiliana na
changamoto hizi tunao na tuna ari na nia ya kusukuma mbele gurudumu la
maendeleo ya mpira. Ombi langu kwenu nyote ninaomba ushirikiano wa wadau
wote kuanzia Serikali, Halmashauri, mashirika ya umma na binafsi na
NGO’s, nina imani tukishikamana tutaifikia ndoto yetu ya kuing’arisha
Tanzania kimpira kwenye anga za dunia.
Ahsanteni nawashukuru sana.
0 comments:
Post a Comment