Sunday 17 November 2013

CHADEMA YAMVAA RC GAMA

 
Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri wa Chadema,
John Mrema

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeitaka serikali kuondoa zuio la Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, dhidi ya wafanyabishara wazawa kusafirisha mahindi kwenda soko la Kenya, kwa kuwa ni kinyume cha agizo la Rais Jakaya Kikwete.

Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri wa Chadema, John Mrema, alisema hayo kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari mwishoni mwa wiki.


Alisema hatua dhidi ya Gama inapasa kuchukuliwa wakati huu, ambao taifa lipo kwenye mkakati wa kuondoa upungufu uliojitokeza katika kutekeleza maazimio ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).


Mrema katika taarifa hiyo pia ameitaka serikali kuondoa hodhi kwa kampuni ya Kilimanjaro Uchumi Company Limited ya kusafirisha mahindi kutoka soko la Himo hadi Kenya.


Badala yake, ametaka uchunguzi ufanywe dhidi ya baadhi ya wamiliki wa kampuni hiyo kama wameshalipa deni la Halmashauri ya Wilaya ya Moshi la Sh. milioni 106 walilokuwa wanadaiwa kupitia kampuni ya Mafubilo Trading.


Pia ametaka pawepo na jitihada za makusudi za kuwawezesha wafanyabiashara wa Kitanzania kupata mitaji na mikopo nafuu ili waweze kushindana na wale wa nchi jirani ili kuwawezesha kujiandaa kikamilifu kuingia kwenye itifaki ya soko la pamoja la EAC.


Akiwa katika ziara ya kiserikali mkoani Njombe hivi karibuni, Rais Kikwete, aliruhusu wafanyabiashara wa Tanzania kusafirisha nafaka nje ya nchi.

Baada ya zuio la Gama, wiki iliyopita madereva wa malori waligoma na kusababisha shehena za nafaka kukwama katika mpaka wa Tanzania na Kenya, eneo la Holili kutokana na mkuu huyo wa mkoa wa kuwazuia wafanyabiashara kutoka Tanzania kwenda kuuza mahindi Kenya na badala yake kuwataka waishie kwenye soko la Himo.

“Katika wakati huu ambao tuko kwenye kutafuta mtangamano mzuri baina ya nchi yetu na nchi wanachama wa EAC na wakati ambao tunaelekea kuwa na itifaki ya soko la pamoja, siyo busara hata kidogo kuwanyima fursa Watanzania kunufaika na masoko yaliyopo kwenye nchi za EAC kwani hali hiyo itaendeleza utamaduni wa kuwafanya Watanzania kuwa nyuma ukilinganisha na wafanyabiashara wa nchi nyingine,” alisema Mrema.


Akijibu tuhuma hizo, Gama alisema hazina ukweli na kwamba, zimetengenezwa na wafanyabiashara waliopewa vibali vya kusafirisha nafaka kwenye soko la Himo, ambao wamegeuka na kufanya biashara ya udalali wa kuvusha magari ya kubeba mahindi kutoka Kenya na kuyaingiza nchini.


Kuhusu deni, alisema kampuni hiyo haidawi na kwamba, inashirikiana na Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) kujenga soko la kisasa Himo.

 
SOURCE: NIPASHE By Muhibu Said

0 comments: