Wednesday 20 November 2013

SERIKARI YAKAZA UZI KATIKA MATUMIZI YA EFD

   Kamishna Mkuu wa TRA, Harry Kitilya.PICHA|MAKTABA 

Arusha/Dar es Salaam. 
 Serikali imesema kuwa mgomo wa wafanyabiashara hauwezi kubadili uamuzi wake wa kukusanya kodi kupitia mashine za elektroniki za EFD na imewataka wafanyabiashara hao kufungua maduka yao kwa sababu hata wakiyafunga watatakiwa kuwa nazo.
Hatua hiyo ya Serikali imekuja ikiwa ni siku ya pili tangu wafanyabiashara hao walipogoma kufungua maduka wakipinga kutumia mfumo huo wa ulipaji kodi.

Aidha, imeliagiza Jeshi la Polisi kusaka wafanyabiashara wanaotishia usalama wa mali za wenzao wakiwashinikiza kugoma kwa kisingizio cha kupinga matumizi ya mashine hizo.
Hata hivyo, Serikali imesikia kilio cha wafanyabiashara hao kuhusu bei ya mashine hizo na imetangaza kupunguza na sasa zitauzwa kati ya Sh600,000 hadi Sh778,000 badala ya Sh800,000 hadi 1.5milioni.
Wakizungumza kuhusu suala hilo kwa nyakati tofauti jana, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Naibu Waziri wa Fedha, Janeth Mbene waliwataka wafanyabiashara kuacha mgomo kwa kuwa ni kinyume cha sheria.
Waziri Mkuu alisema kuwa mashine hizo zilizotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iko sahihi kabisa na kuwa haiwezi kuacha kukusanya mapato kwa njia ya mashine hizo.

Akizindua miradi wa maji katika Shule ya Msingi Olomitu, Kata ya Mlangarini, Arusha, Pinda alisema mashine hizo hazina tatizo na kwamba TRA haina mpango wa kubadili msimamo wake wa kuzitumia.
Mbali ya uamuzi wa kupunguza bei, Waziri Mkuu alisema wafanyabiashara wanapaswa kukumbuka kuwa gharama za ununuaji wa mashine hizo mwishowe zitabebwa na TRA kwani watarudishiwa fedha hizo kadri watakavyokuwa wanazitumia kwa mfumo wa makato.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mbene alisema: “Hawa waliogoma si kweli kwamba hawajapata elimu kuhusiana na utumiaji wa mashine hizo ila kuna waliopata elimu na kupata msukumo kutoka kwa wenzao na wengine walipata elimu hiyo lakini haikuwasaidia.”
“Mgomo huu umeleta usumbufu mkubwa siyo hapa nchini tu, bali hata katika nchi za Afrika Mashariki na Kati kwa wale wanaotegemea maduka hayo.”

Naibu wa waziri huyo alisema Serikali kupita TRA, ilianzisha mashine hizo kwa lengo la kuondoa usumbufu wa wafanyabiashara kukatwa kodi kubwa kwa kukisia, kumrahisishia mfanyabiashara kutunza kumbukumbu na kuondoa usumbufu wa kukisia kukata kodi.

Akizungumzia mgomo huo Mbene alisema: “Tumegawana majukumu. Sisi tumeshawabaini ni wafanyabiashara wakubwa tena wala hawatoki hapa Dar es Salaam, hawa ni wakwepa kodi, wanaamua kutumia nguvu yao ya fedha kuwalazimisha wenzao kugoma tena kwa kuwatishia tumeshawasiliana na polisi kwa hatua za kisheria.”

Chanzo Na Waandishi Wetu, Mwananchi

0 comments: