Mbozi. Kaimu Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Dk Charles Mkambachepa juzi alionja joto
la jiwe baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana kumtaka
arudishe haraka Sh209 milioni za Saccos ya Chama cha Walimu
zilizochukuliwa na halmashauri hiyo katika mazingira ya kutatanisha
kuanzia Mei mwaka huu.
Hali hiyo ilijitokeza juzi jioni wakati Kinana
alipozungumza na baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi
hususan walimu.
Dk Mkambachepa alilazimika kutamka wazi kwamba
atahakikisha anawalipa fedha zote ifikapo mwishoni mwa Januari mwaka
ujao na kwamba juzi hiyo aliwalipa zaidi ya Sh32 milioni kupunguza deni
hilo.
Awali Kinana alipokea taarifa ya malalamiko lukuki
ya walimu yakiwamo ya madai ya zaidi ya Sh1 bilioni na pia halmashauri
kuchukua Sh209 milioni za makato ya walimu kwa ajili ya kurudisha mikopo
ya Saccos.
Walimu walidai halmashauri hiyo chini ya
Mkurugenzi mstaafu Edson Chelewa ilichukua fedha hizo ikidai zinatumika
katika masuala ya kumpokea Rais Jakaya Kikwete kwenye sherehe za Mei
Mosi zilizofanyika kitaifa mkoani Mbeya.
Kutokana na kauli hiyo, Katibu Mkuu wa CCM alisema huo ni uzushi wa hali ya juu na kuitaka halmashauri hiyo kuacha mara moja tabia ya kuwaonea walimu kwa kusingizia viongozi mambo mabaya ya fitina.
“Kuanzia sasa CCM imeamua kuingia kati kufuatilia
matatizo ya walimu yakiwamo madai yao na kwa kweli itahakikisha
yanalipwa” alisema.
Awali akihutubia mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Baraza la Kata, Kinana aliwasihi Watanzania kuendelea kuiamini Serikali ya CCM akisisitiza inalenga kuwatetea wanyonge na kuboresha maisha.
Na Lauden Mwambona, Mwananchi
Posted Jumapili,Decemba1 2013
0 comments:
Post a Comment