Wednesday 27 November 2013

USAJILI DIRISHA DOGO KUFUNGWA DESEMBA 15, KLABU ZAONYWA!

>KILI STARS YATUA NAIROBI, KUCHEZA MACHAKOS NA ZAMBIA ALHAMISI!
>>MECHI YA TANZANITE SASA KUCHEZWA DAR SI MWANZA!
>>MICHUANO YA UHAI YAHAMIA CHAMAZI
PATA HABARI KAMILI:
Release No. 201
TFF_LOGO12TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Novemba 26, 2013
USAJILI DIRISHA DOGO KUFUNGWA DESEMBA 15
Wakati dirisha dogo la usajili linafungwa Desemba 15 mwaka huu, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) tunazikumbusha klabu zote kuheshimu kanuni na kuzingatia muda uliowekwa.
Pia tunakumbusha kuwa kupeleka mchezaji kwa mkopo katika klabu nyingine hakutoi nafasi ya kusajili mchezaji mpya. Kama klabu ilisaji wachezaji 30 maana yake ni kuwa haina nafasi ya kuongeza wachezaji.
Kwa upande wa wachezaji wa kigeni (foreign players), tunakumbusha kuwa kuanzia msimu ujao 2014/2015 watakuwa watatu tu badala ya watano wa sasa.
Kuhusu usajili wa wachezaji kutoka nje mpaka sasa hakuna hata klabu moja imeshaingia kwenye TMS kuomba uhamisho. Itakapofika Desemba 15, system ya TMS itafunga.

MECHI YA TANZANITE SASA KUCHEZWA DAR
Mechi ya kwanza ya raundi ya michuano ya Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika kwa wanawake chini ya miaka 20 kati ya Tanzania (Tanzanite) na Afrika Kusini iliyokuwa ichezwe Mwanza sasa itafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Baada ya ukaguzi uliofanywa na maofisa wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imebainika uwanja huo unatakiwa ufanyiwe marekebisho ambayo hayawezi kuwahi Desemba 7 mwaka huu, siku ambayo ndiyo mechi hiyo inatakiwa kuchezwa.
Vyumba vya wachezaji vya uwanja huo ndilo eneo ambalo linatakiwa  kufanyiwa marekebisho makubwa.

KILIMANJARO STARS YATUA SALAMA NAIROBI
Timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) imewasili salama Nairobi, Kenya tayari kwa mashindano ya Kombe la Chalenji yanayoanza kesho (Novemba 27 mwaka huu) katika Uwanja wa Nyayo.
Kilimanjaro Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager iliwasili saa 3 usiku kwa ndege ya RwandAir, na imefikia katika hoteli ya Sandton iliyoko katikati ya Jiji la Nairobi.
Kwa mujibu wa programu ya Kocha Mkuu Kim Poulsen, Kilimanjaro Stars leo (Novemba 26 mwaka huu) ni mapumziko ambapo kesho itafanya mazoezi kujiandaa kwa mechi yake ya kwanza dhidi ya Zambia itakayochezwa Novemba 28 mwaka huu Uwanja wa Machakos.

MICHUANO YA UHAI YAHAMIA CHAMAZI
Michuano ya Kombe la Uhai imeingia hatua ya robo fainali ambapo sasa mechi zinachezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Uamuzi wa kuhamisha mechi hizo kutoka viwanja vya Karume na DUCE ni kuziwezesha zote kuoneshwa moja kwa moja (live) na Azam Tv.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) tunaomba radhi kwa washabiki ambao watakuwa wameathirika kutokana na uamuzi huo.

RAMBIRAMBI MSIMBA WA ANDREW KILOYI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mwamuzi wa zamani wa FIFA, Andrew Kiloyi kilichotokea mjini Iringa.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Mkoa wa Iringa, Ramadhan Mahano, Kiloyi alifariki dunia juzi (Novemba 24 mwaka huu) kutoka na ugonjwa wa fangasi ya ubongo, na marehemu amesafirishwa kwenda kwao Kigoma ambapo atazikwa.
Kiloyi alizaliwa Mei 5, 1968. Alijiunga na uamuzi wa mpira wa miguu mwaka 1988 ambapo alipata beji ya FIFA mwaka 2001 akiwa mwamuzi msaidizi. Alistaafu uamuzi mwaka 2009, na hadi anafariki akiwa mjumbe wa Kamati ya Waamuzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Iringa (IREFA).
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pole kwa familia ya marehemu, IREFA, ndugu, jamaa na marafiki kutokana na msiba huo na kuwataka kuwa na moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hicho cha majonzi. Mungu aiweka mahali pema roho ya marehemu Kiloyi.
Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

0 comments: