Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Englibert Kiondo
Watu watatu wamefariki dunia katika matukio tofauti jijini Dar es Salaam, likiwamo la Masibu Suha (38), mkazi wa Matemwe Unguja kufariki dunia baada ya kupigwa na radi na mmoja kujeruhiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Englibert Kiondo, alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 6:15 mchana katika eneo la Magogoni ufukweni mwa Bahari ya Hindi, Kigamboni.
Kiondo alisema mtoa taarifa Ussi Mcha (38), mvuvi na mkazi wa Tungi alisema akiwa maeneo hayo akiendesha Ngalawa akiwa na wavuvi sita waliotoka kuvua samaki eneo la Magogoni, ghafla mvua kubwa ikiambatana na upepo mkali ilianza kunyesha hatimaye chombo hicho kupigwa na radi na kusababisha kifo cha Masibu na kumjeruhi Makame Hasani (38) mkazi wa Matemwe Unguja.
Alisema majeruhi amelazwa hospitali ya Vijibweni kwa matibabu na wavuvi wengine wane walisalimika.
Katika tukio jingine, mkazi wa Kimara Suka Mussa Mjilya (23), ambaye alikuwa ndani ya bar iitwayo Five Inn akicheza muziki na wenzake amefariki dunia kwa kinachosadikiwa kuwa ni unywaji wa pombe kupita kiasi. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillus Wambura, alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 4:30 usiku eneo la Kimara Suka.
Alisema wakati akiwa katika bar hiyo akicheza mziki na wenzake umeme ulikatika ndipo Mussa na wenzake wakaanza kudai warudishiwe pesa zao za kiingilio, kitendo hicho kilisababisha purukushani na baada ya kuisha vurugu hizo Musa alionekana kalewa sana.
Alisema walinzi wa bar hiyo walimchukua na kumpumnzisha mapokezi na saa 12: 30 asubuhi mtu huyo alikutwa akiwa amefariki dunia huku mwili wake ukiwa hauna jeraha lolote. Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala kwa uchunguzi, hakuna aliyekamatwa na upelelezi unaendelea.
Wakati huo huo, mkazi wa Mbagala Dickson Reginal (29), ambaye ni kondakta wa gari namba T 273 ASP aina ya Toyota DCM lililokuwa likiendeshwa na Joram Mushi (43) amefariki dunia baada ya kufungua mlango na kuruka nje wakati gari likiwa kwenye mwendo kasi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, alisema tukio hilo lilitokea juzi wakati gari hilo lilikuwa likitokea Tabata kuelekea Ubungo.
Alisema kondakta huyo baada ya kuruka alipata majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake na alifariki dunia akiwa njiani akipelekwa katika Hospitali ya taifa Muhimbili(MNH).
Alisema dereva wa gari hilo amekamatwa, mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na upelelezi unaendelea.
SOURCE:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment