Sunday 24 November 2013

HII TAARIFA RASIMI YA ZITTO KABWE (MB) KUHUSU KUVULIWA NAFASI ZA UONGOZI NDANI YA CHAMA CHA CHADEMA

TAARIFA YA ZITTO ZUBERI KABWE (MB) KUHUSU KUVULIWA NAFASI ZA UONGOZI NDANI YA CHAMA CHANGU CHA CHADEMA

IMG_5324IMG_5252
IMG_5201 
1. Utangulizii. Katika kikao chake cha siku mbili kilichofanyika tarehe 20 ­ 22 Novemba 2013, Kamati  Kuu  ya  CHADEMA,  pamoja  na mambo  mengine,  iliazimia  kunivua nafasi zangu zote za uongozi ndani ya chama. Kwa mujibu wa taarifa ya chama iliyotolewa  katika  mkutano  na  waandishi  wa  habari  siku  ya  Ijumaa  tarehe 22 Novemba  2013,  ilielezwa  kwamba  sababu  za  kuvuliwa  uongozi  mimi  na  Dk Kitila Mkumbo ni uhaini na hujuma kwa chama kutokana na waraka unaojulikana kama mkakati wa uchaguzi 2013. Ukweli ni kwamba waraka uliotajwa si sababu ya mimi kuvuliwa nafasi zangu za uongozi kama ilivyojadiliwa katika Kikao cha Kamati Kuu . Sababu za kufukuzwa kwangu kama zilizojadiliwa katika kikao cha Kamati  Kuu  ni  tuhuma  lukuki  ambazo  si  mara  yangu  ya  kwanza  kuzisikia zikijadiliwa ndani na nje ya vikao vya chama. Hitimisho la tuhuma hizi ni kwamba mimi nimekuwa nikikisaliti chama kwa kutumika na CCM na Usalama wa Taifa.

Nitazianisha  tuhuma hizi na kuzijibu kama ambavyo nimekuwa nikizijibu katika vikao mbalimbali vyama.

ii. Ninatambua kwamba chama changu kinapita katika wakati mgumu sana sasa hivi. Nataka nitamke mapema sana kwamba
 mimi Zitto Zuberi Kabwe sitokuwa chanzo cha CHADEMA kuvunjika. Hiki ndicho chama kilichonilea na kunifikisha hivi  nilivyo.  Ningependa  chama  hiki mtoto wangu atakapokuwa mtu mzima na atakapoamua kujiunga na siasa aingie CHADEMA. Bado nina imani kubwa na chama  changu na  ninaamini ndicho kinachostahili kuendesha nchi jana, leo na kesho.

2.
Kuhusu tuhuma mbalimbali zinazo elekezwa kwangu

Zipo tuhuma nyingi ambazo zimekuwa zikirudiwarudiwa katika vikao vya chama na nje ya vikao na baadhi  ya viongozi wenzangu. Tuhuma hizi zinalenga kuonyesha kwamba  mimi  ni  mbinafsi  na  kwamba  ninapokea rushwa  ili  kukihujumu  chama changu.  Nitazianisha  tuhuma  kwa  kifupi  na  kuzijibu  kama  ambavyo  nimekuwa nikizijibu katika vikao mbalimbali vya chama.

i)  Tuhuma  kwamba  sikushiriki  kumpigia  kampeni  mgombea  wetu  wa  urais  katika uchaguzi wa mwaka 2010.   Ningependa kueleza yafuatayo kuhusu jambo hili:

● Mimi nilikuwa mgombea wa ubunge katika Jimbo la Kaskazini huko Kigoma.

● Pamoja na kuwa mgombea wa ubunge, nilifanya kampeni katika majimbo mengine 16 katika mikoa mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam, Mtwara, Pwani, Shinyanga, Mara na Rukwa. Hakuna kiongozi yeyote wa juu aliyefanya kampeni katika majimbo mengi kama mimi, ukiacha mgombea urais.

● Kote nilipopita nilimpigia kampeni wagombea wetu wa udiwani, ubunge na Rais.

● Katika Mkoa wa Kigoma nilizunguka na mgombea urais katika kata zote za Kigoma Kaskazini na majimbo yote manane ya Mkoa wa Kigoma.

ii)  Tuhuma  kwamba  katika  Mkoa  wa  Kigoma  nilishindwa  kuwapigia  kampeni wagombea  wetu  kiasi  kwamba  peke  yangu  ndiye  niliyeshinda  katika uchaguzi huo.

Ukweli ni kwamba niliwapigia sana kampeni wagombea wetu, na hivyo ndivyo wapiga kura wa Kigoma walivyoamua.

iii)  Tuhuma  kwamba  nilishiriki  kuwashawishi  wagombea  wetu  katika  baadhi  ya majimbo  kujitoa  katika uchaguzi wa mwaka 2010 ili kuwapisha wagombea wa CCM wapite  bila  kupingwa  kwa  njia  ya  rushwa.  Majimbo  yanayotajwa  ni pamoja  na Sumbawanga,  Musoma  Vijijini  na  Singida  Mjini. Kama  nilivyokwisha  kueleza  katika vikao  mbalimbali  vya  chama  jambo hili si la kweli na hakuna popote ambapo watoa tuhuma  hizi  wamewahi  kutoa  ushahidi  kwamba  nilifanya  jambo hili. Nipo  tayari  kwa uchunguzi ndani ya chama na watoa tuhuma waje na ushahidi bayana wa jambo hili. Si afya kwa chama kuendelea kurudiarudia tuhuma hizi kila mara tangu mwaka 2010 bila uchunguzi wowote kufanyika na jambo hili lifikie mwisho.

iv) Tuhuma kwamba nimekuwa sishiriki katika operesheni mbalimbali za chama: Ukweli ni  kwamba nimeshiriki sana katika operesheni mbalimbali za chama ndani na nje ya nchi. Kwa mfano, mwaka 2011 tulikuwa na operesheni kubwa katika mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na nilikwenda katika mikoa yote tuliyotembelea. Mwaka 2012 baada  ya hoja ya mkonge bungeni nilifanya ziara Mkoa wa Tanga. Mwaka 2012 kulikuwa  na  operesheni  kubwa  moja  katika  mikoa  ya  kusini  ya  Mtwara  na  Lindi.

Operesheni hii sikushiriki kwa sababu nilikuwa nchini Marekani kufungua matawi kwa mwaliko wa Watanzania wanaoishi huko.

v) Tuhuma kwamba nimekidhalilisha chama kwa tamko la PAC kwamba Hesabu za Vyama hazijakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG): 
IMG_5215
 Katika  jambo  hili  ninatuhumiwa  kwamba  mimi  kama  Naibu  Katibu nilipaswa  kuwasiliana  kwanza  na  viongozi  wa  chama  'kuwatonya'  ili  wajiandae. Kwamba kutokuwatonya kumekidhalilisha chama na kukiweka kundi moja na CCM na nastahili  kuadhibiwa  vikali  kwa  kuwa  katika  taarifa  yangu  nilikuwa  na  nia  mbaya na chama  chetu.  Maelezo  yangu  niliyoyatoa  na  ambayo  ningependa  kuyakariri  hapa kuhusu jambo hili ni kama ifuatavyo:

● Utawala  bora  hautaki  mimi  kutumia  nafasi  yangu  ya  uenyekiti  wa  PAC  kulinda chama changu na kuonea vyama vingine. Kufanya hivyo ni kuendeleza tabia zile zile ambazo tunazipinga na ambazo tunapigania kuzibadilisha

● Napenda  kusisitiza  kwamba  hakuna  chama  ambacho  kimewahi  kukaguliwa  na Mdhibiti  na  Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).  Natambua  kwamba  mahesabu  ya chama  changu  yamekuwa  yakikaguliwa  na  wakaguzi  wa  nje  kwa  utaratibu tuliojiwekea. Lakini matakwa ya kisheria ni kwamba mahesabu ya vyama vya siasa hayajakaguliwa na CAG, na hili ni kosa la kisheria, bila kujali kosa hili ni la nani.

vi) Tuhuma kwamba mimi ni mnafiki katika kukataa kwangu kuchukua Posho za Vikao

Mtakumbuka kwamba mimi nilikataa kuchukua posho tangu mwaka 2011 kama ishara ya kuonyesha kwa vitendo msimamo wa chama chetu wa kupinga posho za kukaa na matumizi  mengine  yasiyofaa  katika  fedha  za umma kama ilivyoanishwa kwenye Ilani yetu  ya  mwaka  2010­2015.  Mtakumbuka  kwamba  hivi  karibuni  Mheshimiwa  Lema amenishutumu  kwamba  kukataa  kwangu  kuchukua  posho  ni  unafiki  kwa  sababu ninapokea posho  kubwa zaidi katika mashirika ya umma ambapo mimi ni mwenyekiti wa kamati husika. Ninapenda kueleza yafuatayo kuhusu jambo hili:

● Sipokei  posho  yeyote  ya  vikao  (sitting allowance)  ndani  na  nje  ya  Bunge tangu mwaka  2011. Hii ni pamoja na vikao vyote katika Kamati za Bunge ninavyohudhuria. Mtu yeyote mwenye ushahidi vinginevyo auweke hadharani.

● Swala la kukataa posho (sitting allowance) ni swala la kiilani katika chama chetu, na kwangu  ni  swala  la  kimisingi  zaidi.  Katika  Wilaya  yangu  vifo  vya  kina  mama wajawazito ni 1900 kati ya wanawake 100,000 wenye ujauzito. Vifo hivi vinatokana na ukosefu wa huduma kwa sababu ya bajeti finyu. Ndiyo maana nilifurahi sana kwa chama  chetu  kuliweka  swala  la kupunguza  matumizi  ya  Serikali  katika  Ilani,  na kuondoa  posho  za  wabunge,  ambao  tayari  wanapokea  mishahara  mikubwa, kungesaidia sana kupatikana fedha ambazo zingeokoa vifo vingi vya kina mama.

● Jambo hili si suala la ugomvi baina yangu na Mheshimiwa Lema. Ni suala la msingi katika chama chetu.

3. Usambazaji wa Ripoti ya Siri kuhusu Zitto Kabwe

Hivi karibuni kulisambazwa waraka unaoitwa ripoti ya siri kuhusu mimi ukibeba lundo la tuhuma kwamba nimehongwa fedha nyingi ili kukihujumu chama changu. Waraka huu ulidaiwa  kuwa  umechomolewa  kutoka  makao  makuu  ya  CHADEMA.  Jambo  hili  pia lilijadiliwa katika  kikao cha juzi kwa kifupi, na majibu ya viongozi wa chama ilikuwa ni kwamba  waraka  huu  haukuandaliwa  wala  kusambazwa  na  makao  makuu.  Katika mchango wangu nililalamikia mambo matatu yafuatayo:

i. Kwamba baadhi ya waliokuwa wanasambaza waraka ule walikuwa ni viongozi wa chama  chetu.  Bahati  mbaya  hadi  leo  hakuna  hata  mmoja  ambaye amekwishachukuliwa  hatua za kinidhamu. Ninaamini kwamba kuna siku watu hao watachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu za chama chetu.

ii. Kwa kuwa chama kimekana rasmi kuhusika na waraka huu, nitaendelea na taratibu za  kisheria  ili  kuhakikisha  kwamba  wote  waliohusika  kutengeneza  hekaya  ile wanachukuliwa hatua stahiki za kisheria.

4. Hitimisho

a) Ninatambua  kwamba  kuna  watu  walitegemea  leo  ningejibu  mapigo  na ningewazodoa  watu  kwa  majina  kama  ilivyo  kawaida  katika  siasa  za  Tanzania.

Natambua pia kwamba, kama ilivyo kawaida wakati wa migogoro katika vyama vya siasa hapa Tanzania, kuna watu walitegemea leo ningetangaza 'maamuzi magumu'.

Natambua kwamba wapo ambao wangependa kupata nafasi ya kuendelea kutumia  suala  hili  katika  harakati  zao  za  kudhoofisha  mapambano  ya demokrasia  na  uthabiti  wa  siasa  za  ushindani  nchini  mwetu.  Napenda wanachama wa CHADEMA na wapenda demokrasia na siasa safi wote nchini watambue  kwamba  mimi  bado  ni  mwanachama  mwaminifu  wa  chama  hiki  na nitakuwa wa mwisho kutoka kwenye chama hiki kwa hiari yangu. Nitafuata taratibu zote ndani ya chama katika kuhitimisha jambo hili.

b) Naomba  wanachama  waelewe  kwamba  mimi  kama  binadamu  ninaumia ninapopigwa.  Tuhuma  ninazorushiwa  ni  kubwa  na  zinanikwaza.  Tuache  siasa  za uzushi  ili  tujenge chama chetu na nchi yetu, ili hatimaye tuwakomboe Watanzania wenye matarajio na imani kubwa kwa chama chetu.

c) Kama mwanasiasa kijana niliyekaa katika siasa kwa muda sasa yapo mengi mazuri  nimeyafanya.  Lakini  kuna  maeneo  nilipojikwaa  na  yapo  makosa niliyofanya kisiasa katika maisha yangu ya siasa.

d) Kinachoendelea  ndani ya chama chetu ni mapambano ya kukuza demokrasia. Ni mapambano  baina  ya  wapenda  demokrasia  dhidi  ya  wahafidhina,  waumini  wa uwajibikaji  dhidi  ya wabadhirifu  na  wapenda siasa safi dhidi ya watukuzao siasa majitaka.  Hii  ni  changamoto  kubwa  ndani  ya  chama  chetu  inayohitaji  uongozi shupavu  kuikabili.  Nitasimama  daima  upande  wa  demokrasia. Kama  alivyopata kunena  mmoja ya wanasiasa maarufu, 'kiwango cha juu kabisa cha uzalendo katika nchi ni kukubali kutofautiana kimawazo', na ninatamani huu ndio uwe utamaduni wa chama chetu.

Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Dar es Salaam.
24 Novemba, 2013

0 comments: