Sunday 17 November 2013

BAADA HARAMBEE KUINGIA MITINI SASA TAIFA STARS KUCHEZA NA ZIMBABWE JUMANNE

..JUMANNE TAIFA STARS KUCHEZA NA ZIMBABWE 

SH. 5,000/- NDIYO KIINGILIO CHA KUISHANGILIA STARS!!

...HARAMBEE STARS ‘WAINGIA MITINI!’

KILI_MABINGWA Release No. 197
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Novemba  17,2013

TAIFA STARS SASA KUIKABILI ZIMBABWE J4

Taifa Stars sasa inacheza na Zimbabwe mechi ya Kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA)- FIFA Date itakayofanyika keshokutwa Jumanne (Novemba 19 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Awali Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ilikuwa icheze na Kenya (Harambee Stars), lakini Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya (FKF) lilituma taarifa jana jioni (Novemba 16 mwaka huu) likieleza kuwa timu yake haitacheza tena mechi hiyo.
Kikosi cha Zimbabwe chenye msafara wa watu 30 kinatarajia kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kesho (saa 3 asubuhi) tayari kwa mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 11 kamili jioni.
Waamuzi wa mechi hiyo wanatoka Uganda wakati Kamishna atakuwa Leslie Liunda wa Dar es Salaam. Mwamuzi wa mezani ni Oden Mbaga pia wa Dar es Salaam.
Stars chini ya Kocha Kim Poulsen ipo kambini tangu Novemba 12 mwaka huu kujiwinda kwa mechi hiyo. Kim amejumuisha kwenye kikosi chake wachezaji watano wanaocheza mpira wa miguu nje ya Tanzania.
…5,000/- NDIYO KIINGILIO CHA KUISHANGILIA STARS
Kiingilio katika mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya wenyeji Tanzania (Taifa Stars) na Zimbabwe ni sh. 5,000 wakati tiketi zitaanza kuuzwa Jumatatu (Novemba 18 mwaka huu) kwenye vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Mbali ya kiingilio hicho cha sh. 5,000 ambacho ni kwa viti vya bluu na kijani, viingilio vingine ni sh. 30,000 kwa VIP A, sh. 20,000 kwa VIP B, sh. 15,000 kwa VIP C wakati viti vya rangi ya chungwa ni sh. 10,000.
Tiketi zitauzwa katika magari maalumu katika vituo vya; Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, mgahawa wa Steers uliopo Mtaa wa Ohio na Samora, Sokoni Kariakoo, Dar Live Mbagala, OilCom Ubungo, BMM Salon iliyopo Sinza Madukani, Uwanja wa Uhuru, mgahawa wa Brake Point uliopo Kijitonyama, na kituo cha mafuta Buguruni.
Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

0 comments: