Sunday 24 November 2013

MSIBADILISHE VIONGOZI KAMA WANAFAA ASEMA -KINANA KATIBU MKUU WA CCM

Waziri wa Uchukuzi na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, akimlaki wa furaha, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, baada ya kuwasili katika bandari ndogo ya Kiwira, wilayani Kyela mkoani Mbeya akitokea Mbamba Bay mkoani Ruvuma jana. Kushoto ni Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye na Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Dk. Asha-Rose Migiro.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amesema kila mtu ana haki ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi ndani ya chama hicho na kama anafanya vizuri hakuna sababu ya wananchi kubadilisha viongozi kama shati.

Alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wananchi katika bandari ya Itungi-Kyela mara baada ya kupokelewa akitokea wilaya ya Nyasa iliyopo mkoa wa Ruvuma kwa ajili ya kuanza rasmi ziara ya kichama katika mkoa wa Mbeya.


“Tunampongeza Dk. Mwakyembe (Waziri wa Uchukuzi) kwa kazi nzuri anayofanya katika jimbo lake na kama waziri, kwa hiyo kama mtu anafanya vizuri, si vizuri kumbadilisha kama shati,” alisema. Kinana alisema suala la kuwapo kwa meli katika maziwa likiwamo Ziwa Nyasa, ni muhimu sana na kumuomba Dk. Mwakyembe kuwaeleza wananchi mkakati uliopo katika wizara yake kuhusu meli mpya.


Kwa upande wake, Dk. Mwakyembe alisema hivi sasa kuna miradi mikubwa minne ya ujenzi wa meli kwa ajili ya maziwa ya Tanganyika, Victoria na Nyasa.

Alisema meli hizo zinajengwa na Serikali ya Denmark kupitia shirika lake la misaada la Danida na pia kuna meli nyingine zitajengwa na Serikali ya Korea Kusini.

Dk. Mwakyembe alisema serikali pia imepanga kununua pantoni itakayotumika kusafirisha abiria kati ya Kyela na Matema na kiasi cha Sh. milioni 900 kimetengwa na mchakato wa ununuzi umeanza.


Aliongeza kuwa kuna mpango wa kukopa fedha katika Benki ya TIB ambazo zitatumika kununulia meli mpya itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 300 na mizigo ya tani 300.


SOURCE: NIPASHE
25th November 2013

0 comments: