Thursday 21 November 2013

KARATA YA MWISHO YA BABU YEYA NA PAPI KOCHA LEO


Mwanamuziki Nguza Vicking maarufu kama Babu Seya na mwanae.

Hatma ya kuachiwa huru au kuendelea na adhabu ya kifungo cha maisha kwa mwanamuziki  Nguza Vicking maarufu kama Babu Seya na mwanae itajulikana leo katika Mahakama ya Rufani Tanzania itakapotoa hukumu ya mapitio dhidi ya rufaa yao.

Hatua hiyo, imefikiwa baada ya mwanamuziki huyo na mwanae kuomba mahakama hiyo kufanya mapitio ya hukumu iliyotolewa  na jopo hilo na kuwaona watoto wake wengine Nguza Machine na Francis Nguza kuwa hakuna ushahidi ulioonyesha kwamba wana hatia katika makosa hayo.


Hata hivyo, mahakama hiyo iliwaona  Babu Seya na mwanae mmoja Papii Nguza wana hatia ya makosa matano ya kubaka kati ya makosa 23 yaliyokuwa yanawakabili yakiwamo ya kulawiti.


Oktoba 30, mwaka huu mahakama hiyo iliyoketi chini ya jopo la majaji watatu  likiongozwa na Mwenyekiti Jaji Nathalia Kimaro, akisaidiana na  Mbarouk Mbarouk na Salum Massati walisikiliza hoja za pande zote mbili kuhusu mapitio hayo.


Katika hoja zao kupitia wakili  Mabere Marando, Babu Seya na Papii Kocha  aliomba mahakama kuwaachia huru wanamuziki hao wanaotumikia kifungo cha maisha kwa makosa ya  kulawiti na kubaka kutokana na ushahidi uliotumika kuwatia hatiani kuwa na mapungufu ya kisheria.


Kadhalika, alidai kuwa mahakama hiyo ikijielekeza kwenye ushahidi uliotolewa na baadhi ya mashahidi wa Jamhuri kwamba haukufuata masharti ya sheria ya kupokea ushahidi wa watoto wadogo ni rai ya upande wa utetezi itupilie mbali na kuwafutia warufani mashitaka yaliyowatia hatini.


Alidai kuwa lengo la kufikisha maombi hayo mahakamani ni  kuitaka kupitia makosa yanayojionyesha kuonyesha kwamba mahakama hiyo iliteleza bila kuwaachia warufani na badala yake, ilitumia ushahidi wa watoto ambao ulikuwa na mapungufu ya kisheria.


“Katika hukumu yenu ya Februari 11, mwaka 2010 mlikubali kwamba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, ilikosea katika kupokea ushahidi wa watoto wadogo ambao hawakufuata masharti ya kupokea ushahidi huo japo uliungwa mkono na ushahidi mwingine katika kuwatia hatiani warufani,” alidai Marando.


Alidai kuwa mbali na mapungufu hayo, upande wa Jamhuri haukuita mashahidi muhimu kwenye kesi hiyo ambao walitajwa na baadhi ya mashahidi akiwamo Mangi mwenye duka jirani na nyumba ya Babu Seya.


Alidai kuwa ushahidi huru uliotumika kuunga mkono ushahidi wa watoto uliotumika kuwatia hatiani Babu Seya na mwanawe, taratibu za kisheria zilikiukwa upande wa utetezi uliomba mahakama kuwaachia huru warufani hao.


Upande wa Jamhuri uliongozwa na jopo la mawakili watano, ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Jackson Mdaki akisaidiana na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Angaza Mwipopo, Imakulata Banzi, Joseph Pande  na Wakili wa Serikali Abrimark Mabruki.


Mdaki alidai kuwa maombi yaliyowasilishwa na upande wa utetezi hayana mashiko ya kisheria kwa sababu kifungu kilichotumika kuyafungua mahakamani hapo ni cha mashauri ya madai na siyo ya jinai kama kesi hiyo iliyopo mahakamani.
SOURCE: By Hellen Mwango NIPASHE

0 comments: