Saturday 23 November 2013

MWASISI WA CHEDEMA ASEMA WATAENDELEA KUWAFUKUZA WASALITI WA CHAMA

Mtei: Tutaendelea kuwafukuza wasaliti 

Mwasisi wa Chadema Edwin Mtei anamtaka Saidi Arfi aache kulalamika kwani “kama alikuwa na ndoto kwamba siku moja atakuwa mwenyekiti wa Chadema taifa alipaswa kujichunguza kwanza.” PICHA | MAKTABA 
  


Arusha. 
 Mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edwin Mtei amesema kuwa chama hicho kitaendelea kuwafukuza wote wanaokihujumu huku akieleza kwamba, anaunga mkono kuvuliwa uongozi kwa Zitto Kabwe na Dk Kitila Mkumbo.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili, nyumbani kwake jana, Mtei aliyewahi kuwa Gavana wa Benki Kuu (BOT) na Waziri wa Fedha katika utawala wa awamu ya kwanza wa Mwalimu Julius Nyerere, aliweka wazi kuwa daima ataunga mkono dhamira ya kukisimamia chama hicho aliyoitaja kuwa ni safi.

 “Naunga mkono uamuzi wote wa Kamati Kuu, kuwasimamisha na kuwavua uongozi Naibu Katibu Mkuu wetu Zitto Kabwe na Dk Kitila Mkumbo. Na kwa sababu Chadema inataka kusonga mbele, lazima iwafukuze mafisadi na wezi wanaoshirikiana kukihujumu chama,” alisema Mtei.
Bila kufafanua zaidi au kutaja majina, mwenyekiti huyo wa kwanza wa Chadema alisema: “Hatuwezi kuendesha chama wakati viongozi wengine wanapokea pesa na kuzihifadhi kwenye akaunti za siri.” Alisisitiza kwamba kwa nafasi yake akiwa mwasisi wa Chadema ni lazima ahakikishe anaunga mkono dhamira safi ya kukisimamia chama.

Kuhusu Arfi kujiuzulu
Akizungumzia hatua ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Saidi Arfi kujiuzulu, Mtei alisema kuwa inafaa kiongozi huyo ajitazame upya na kujisahihisha badala ya kuwa mlalamikaji kila siku.
“Aache kulalamika kwa sababu, wakati alipochaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti mimi nilisimamia uchaguzi. Kama alikuwa na ndoto kwamba siku moja atakuwa mwenyekiti wa Chadema taifa alipaswa kujichunguza kwanza,” alisema.

Mtei aliongeza kuwa iwapo kuna watu wanadhani Chadema itakufa hiyo ni dhana potovu, lakini kwa sasa chama hicho kimejipanga kuchukua dola na tayari wamejiimarisha kimkakati.
“Katika suala la kushughulikia watu wanaokihujumu chama  hakuna ‘compromise’ (mjadala),” alihitimisha Mtei.   Juzi Chadema ilitangza uamuzi wa Kamati Kuu yake kuwavua uongozi Zitto Kabwe na Dk Kitila, huku Arfi akitangaza kujiuzulu nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema Tanzania Bara.
Mtei amewahi kumkemea na kumwonya Zitto katika mambo mbalimbali aliyofanya ndani ya Chadema, moja ikiwa Oktoba mwaka jana ambapo mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini, alipotangaza kuwania urais mwaka 2015.

Alisema kuwa hatua hiyo itasababisha mzozo na mpasuko ndani ya chama,  huku akiongeza kwamba amekuwa akimshauri Zitto mara kwa mara kuhusu hatua yake hiyo akimtaka kuwaunganisha wana-Chadema na siyo kuwagawa au kuwavuruga.
“Hakuna shida kuonyesha hisia, lakini unatengeneza mzozo mkubwa sana ukitangaza sasa. Mimi nimeshamshauri sana Zitto, ahakikishe anakiunganisha chama na siyo kukigawa wala kukivuruga,” alisema Mtei.
 
Na Thomas Mashalla, Mwananchi
Posted  Jumapili,Novemba24  2013

0 comments: