Saturday 16 November 2013

KASHFA MENO YA TEMBO:MAOFISA TRA BANDARI WAKAMATWA ZANZIBAR


Kamishna wa Polisi Zanzibar,CP Mussa Ali Mussa

Polisi Zanzibar imewakamata watuhumiwa wengine watatu wakiwamo maafisa wawili wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), kituo cha Bandari Zanzibar kwa kuhusika na kashfa ya kupatikana kwa meno ya tembo yenye thamani ya mabilioni ya shilingi.

Kamishna wa Polisi Zanzibar, CP Mussa Ali Mussa, amewataja maafisa wa TRA waliokamatwa kuwa ni Omari Hamad Ali (50) na Mohammed Hija (48), wote wanafanya kazi katika Bandari ya Mtuhumiwa mwingine ni kibarua wa Mamlaka ya bandari Zanzibar, Haidar Ahmad Abdallah (54).


Kukamatwa kwa watuhumiwa hao kunaifanya idadi ya watuhumiwa waliokamatwa hadi sasa kwa kuhusika na sakata hilo kufikia watano.


Kamishna Mussa amesema watuhumiwa wengine wawili ambao ni wafanyakazi wa Kampuni ya uwakala wa mizigo ya Island Sea Food Limited, Mohammed Suleiman Mussa (45) na Juma Ali Makame (34), walikamatwa siku ya tukio kwenye Bandari ya Zanzibar.

Tayari watuhumiwa hao wamesafirishwa kwenda Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano zaidi.

Kusafirishwa kwa watuhumiwa hao, kunatokana na Zanzibar kutokuwa na sheria maalumu inayohusu wanyamapori.


Maafisa wa Idara ya Wanyamapori nchini, jana wamekamilisha kazi ya kuhesabu na kulinganisha vipande 1,023 vya meno ya tembo vilivyokamatwa juzi kwenye Bandari ya Zanzibar na kubaini idadi ya tembo waliouawa kuwa ni 305.


Meno hayo yenye uzito wa kilo 2,915  yenye thamani ya Dolla 4,775,000 sawa na Sh. 7,480,125,000 yalikamatwa yakiwa yamehifadhiwa katika magunia 98 na kuwekwa kwenye kontena la futi 40 lenye namba PCIU 857619/0 lillilokuwa tayari kupakiwa kwenye meli ya MV Kota Henning kupelekwa nchini Ufilipino.


Makachero wa Polisi wa Kimataifa Interpol  nchini, kwa kushirikiana na makachero wa Polisi Zanzibar, idara ya wanyamapori makao makuu, wanaendelea na upelelezi wa kuwabaini wale tote waliohusika na kashfa hiyo.


Jana Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Mussa Ali Mussa, alisema kuwa kazi kubwa iliyobaki ni kuhakikisha kuwa upelelezi wa kina unafanyika ili kuwakamata wote wanaohusika na mtandao huo.


Alisema hadi sasa Jeshi la Polisi bado linamsaka tajiri aliyewezesha mipango ya kukusanywa na kusafirisha shehena hiyo kutoka Tanzania Bara hadi Zanzibar ili kusafirishwa nje ya nchi.
SOURCE: NIPASHE 
By Mohammed Mhina 

0 comments: